Mahojiano Maalum na Padre Charles Kitima, Katibu Mkuu wa TEC
Na Mwandishi Maalum, Dar es Salaam.
Padre Charles Kitima, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, tarehe 3 Juni 2025, aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ulinzi na tunza yake ya daima na hatimaye kumrejeshea afya yake. Hii ni Ibada ya Misa iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili lililopo TEC Kurasini, Jimbo kuu la Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wafanyakazi wa Sekretariet kuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki. Padre Charles Kitima, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), katika mahojiano maalumu na Jambo TV, amesema tukio la yeye kushambuliwa na watu wasiojulikana linafahamika vizuri na vyombo vya dola, na kwamba hatua zaidi kuhusu uchunguzi na haki zipo katika vyombo hivyo vya usalama. Padre Kitima amesema kuwa tayari amehojiwa na maofisa wa usalama ambao walipata maelezo yake, na sasa anasubiri hatua zao.
“Vyombo vya dola vimekuja kunihoji, nimewaeleza niliyodhani kwa wakati ule waliyahitaji. Wenyewe wanajua, wanalijua hili tukio vizuri… mbele ya Mungu wanalijua vizuri,” amesema Padre Kitima. Ameeleza kuwa haitakuwa vyema kwa vyombo vya dola kufanya kwa Watanzania wengine kile alichokumbana nacho yeye, na ameonesha masikitiko yake kuhusu ukimya wa kisheria licha ya tukio hilo kujulikana vyema kwa mamlaka husika. "Nisingependa Mtanzania yeyote vyombo vinavyolifanya kazi suala langu wanavyonifanyia mimi wawafanyie wengine hivyo, nisingependa wafanye hivyo.”