ĐÓMAPµĽş˝

Askofu Mkuu Mkwande akiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Suluhu Hassani wakati wa Kongamano la Bujora,Mwanza liitwalo "Bulabo." Askofu Mkuu Mkwande akiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Suluhu Hassani wakati wa Kongamano la Bujora,Mwanza liitwalo "Bulabo."  (©TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Tanzania,Kongamano la Bujora:Bulabo-sherehe ya mavuno ya Wasukuma na imani

Kila mwaka linafanyika Kongamo liitwalo Bulabo lililoanzishwa na Padre David Clement aliyekuwa Paroko wa kwanza wa Bujora.Pamoja na kuanzisha Makumbusho alipata wazo la kuunganisha sherehe ya mavuno ya Wasukuma na imani.Kiutamaduni Wasukuma,Mwanza walitoa shukrani kwa mtemi kwa asilimia kadhaa ya mavuno"kushosha nsikule."Ni katika muktadha huo,Juni 21 Mgeni rasimi wa tukio hilo alikuwa Rais wa Tanzania na kupokelewa na Askofu Mkuu Nkwande.

Na Pd.Barnabas Ntulugu Mathias – Jimbo Kuu,Mwanza na Angella Rwezaula – Vatican.

Jimbo Kuu katoliki la Mwanza nchini Tanzania kwa mara nyingine limefanya Kongamano katika Parokia ya Bujora Jumamosi tarehe 21 Juni 2025. Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, akiwa na mwenyeji wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu katoliki la Mwanza, Renatus Nkwande na wadau  wengine walioshiriki katika hafla hiyo inayosikika sana, zaidi ikiwa ni  katika muktadha wa Mkesha wa Sherehe ya Mwili na Damu ya Yesu,  Dominika tarehe 22 Juni 2025. Askofu Mkuu Mkwande akitoa hotuba, awali alimpongeza Rais wa nchi ya Tanzania “kwa shughuli  zinazofanywa kwa ajili ya watanzania.” Pamoja na hayo pia alimpatia “pole kwa changamoto anazokabiliana nazo,” na kwamba “kama kiongozi lazima ziwepo pia.” 

Tamaduni za  kisukuma nchini Tanzania na imani
Tamaduni za kisukuma nchini Tanzania na imani   (©TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

'Utambuzi wa nafasi za utamaduni wa kiafrika'

Askofu Mkuu Nkwande alielezea pia  jinsi ambavyo Rais wa nchi  aliungana nao katika matukio mbali mbali ya huko  Mwanza na kibinafsi alimshukuru: “kwa utayari wake, hasa kwa ajili ya utoaji wa vibali katika kituo  cha makumbusho hapa Bujora. Hili ni jambo jema linaloonesa utambuzi wa nafasi ya utamaduni wetu wa kiafrika. Utayari ulio nao daima wa kukutana na hata kuwakutanisha na kuwawezesha viongozi wa jadi, watemi, machifu na wa maeneo yote hapa Tanzania.” Katika hotuba hiyo aliendelea Askofu Nkwande kusema kuwa: “Uwepo wa viongozi wetu wa jadi ni kielelezo tosha kuwa hata sisi waafrika tupo na tulikuwapo hata kabla ya ujio wa wageni waliotufikia kutoka nje ya Tanzania na Afrika. Dhana ya kubeza mambo ya kwetu na kuhusudu kila kilicho cha kigeni ni mawazo potofu."

Tunawaenzi viongozi wetu hawa, kila tunapowaona tukumbuke tulikotoka na tukumbushwe jinsi tulivyoishi. Tuliishi kwa upendo, tuliishi kwa amani hata kama kulitokea chochote, kimsingi katika historia, unaona yalikuja machafuko baada ya wageni kufika. Tuwatumie viongozi hawa kujikumbusha jadi zetu, njema ili tudumishe maadili yaliyo mema ya taifa letu la Tanzania,” alisisitiza kiongozi wa Kanisa kuu la Mwanza. Kwa kuhitimisha, Askofu Mkuu alimtakia  â€śBaraka nyingi za Mwenyezi Mungu” na kwamba anamwombea  â€śheri katika jitihada zako njema. “ Tuombee na uchaguzi wetu uende vyema, na wewe tunakuombea ili ushiriki vyema katika zoezi hilo. Mungu ibariki Tanzana, Mungu awabariki nyote Asanteni sana.”

Historia Fupi ya Uinjilishaji Mwanza

Jimbo Kuu la Mwanza katika historia yake ya imani, iliinjilishwa  na Wamisionari wa Afrika (White Fathers). Kwa mara ya kwanza, Wamisionari hawa walifika Mwanza kunako tarehe 23 Desemba 1878 katika kijiji kimoja kinachoitwa Malya (Parokia ya Malya kwa sasa na kituo cha hija). Walishangaa kusikia jina hilo kwa sababu lilifanana na Maria hata wakasema, watu hawa wana imani sana mpaka jina la kijiji limepewa kwa heshima ya Bikira Maria bila kujua kuwa kwa Wasukuma Malya maana yake ni kula/ulaji. Sababu kubwa ilikuwa ni kupumzika kutokana na uchovu wa safari pia ikiwa ni maandalizi ya adhimisho la Noeli ambapo walisali mkesha na siku yenyewe ya sherehe. Hii ikaweka alama isiyofutika kwamba kwa mara ya kwanza Misa iliadhimishwa katika Kanda ya Ziwa na viunga vyake.

Hii ni nyumba katika makumbusho ya Wasukuma Bujora.Imejangwa kwa mtindo wa kigoda kuonesha kiti cha Mtemi.Pembeni zimeandikwa temi zote za Kisukuma.Ndani yake kuna vifaa maalum vya kitemi.
Hii ni nyumba katika makumbusho ya Wasukuma Bujora.Imejangwa kwa mtindo wa kigoda kuonesha kiti cha Mtemi.Pembeni zimeandikwa temi zote za Kisukuma.Ndani yake kuna vifaa maalum vya kitemi.   (©TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

 

Baada ya hapo waliendelea na safari mpaka eneo la Kageye(Magu) ambapo kulikuwa na Bandari ndogo ya kuvusha watumwa. Hapo wamisionari walikuwa wakitafuta njia kuelekea Uganda na walifanikiwa kufika huko kunako tarehe 17 Februari 1879. Madhulumu ya Kabaka na changamoto zingine ziliwafanya wafikirie tena kurudi Mwanza. Safari yao, ilikamilika kunako mwaka 1883 walipotulia rasmi katika eneo la Bukumbi (Parokia na kituo cha hija kwa sasa). Bukumbi ikawa Makao makuu (Kanisa kuu) la Vikarieti ya Nyanza ikibeba maeneo ya Mwanza, Shinyanga, Musoma, Kagera yote, Rwanda, Burundi na Uganda Kusini  na ndiyo maana kunako mwaka 1885 (Septemba au Oktoba), Watakatifu Mashahidi wa Uganda walikuja kumtembelea Askofu wao kabla ya kurudi na kuuawa.

Wasukuma: Watu wenye Msimamo wa Imani zao

Baada ya utulivu na neema ya Roho Mtakatifu ikiwaongoza, waliweza kufungua misheni nyingi. Maeneo mengi hasa ya Buhaya na Ukerewe, Wamisionari walipokelewa kwa moyo sana isipokuwa katika eneo la Usukuma. Mapokeo yanaeleza kuwa, walikuwa radhi kuwapa wamisionari vyakula, maeneo ya kuishi na kila aina ya ukarimu isipokuwa kusali na kuacha msimamo wa imani zao. Hii iliwapa changamoto wamisionari kiasi kwamba wakafikiria wafanye nini?

Fanana naye ili Uishi naye kwa Utamadunisho: Zao la Bulabo

Mwanzoni mwa miaka ya 1950, wamisionari walifaulu kupata misheni nyingine ya Bujora (Kisesa) ndipo yaliyopo makumbusho ya Kisukuma. Kwa sababu walikuwa wamejua utamadani kwa Wasukuma na walitaka kufanana nayo kwa kila hali ili kusudi kuleta utamadunisho. Kwa njia hiyo yapo mambo mengi, ambayo yangeweza kuhusu historia hiyo lakini kwa leo tuakisi suala la Bulabo.

Mwanzilishi wa kwanza alikuwa ni Padre David Clement “Fumbuka” aliyekuwa Paroko wa kwanza wa Bujora. Yeye pamoja na kuanzisha Makumbusho haya alipata wazo la kuunganisha sherehe ya mavuno ya Wasukuma na imani. Kipindi cha mwezi June hadi wa Julai, kiutamaduni Wasukuma walikuwa wanafanya matendo ya kurudisha shukrani kwa mtemi kwa kupeleka vyakula na asilimia kadhaa ya mavuno “kushosha nsikule” kama ilivyokuwa inajulikana kwa lugha yao,  kwa sababu kabla yake, mtemi alikuwa akibariki mbegu na mashamba kabla ya kuanza kilimo. Hivyo walitakiwa kutoa shukrani hiyo. Pia, ilikuwa sehemu ya kwenda kuweka hakiba ili njaa ikija, watu wa utemi huo wapatiwe chakula kutoka kwenye hazina kuu ya utawala(tunaweza kufikiria au kufananisha huko Misiri - Mwanzo 42:1-25).

Hili ni Kanisa la Parokia ya Bujora.Limejengwa kwa mtindo wa Msonge kama ilivyokuwa nyumba ya Wasukuma.Ni ishara ya kutamadunisha na kuzipatia maana ya kijamii.
Hili ni Kanisa la Parokia ya Bujora.Limejengwa kwa mtindo wa Msonge kama ilivyokuwa nyumba ya Wasukuma.Ni ishara ya kutamadunisha na kuzipatia maana ya kijamii.   (©TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Kwa njia hiyo, kucheza na maonesho ya ngoma yaliambatana kwa karibu. Lakini katika miezi hiyo hiyo, Sherehe ya Mwili na Damu ya Yesu Kristo ilikuwa inaangukia. Kilichomwongoza Padre  Klementi ni kutamadunisha hili suala maana lilikuwa na nguvu kiasi cha kufifisha Sherehe ya Ekaristi. Akafanya tafsiri kwamba, kama ambavyo watu walikuwa wanabarikiwa mbegu zao na Mtemi kabla kilimo, iwepo hata Misa Takatifu ya kubariki mbegu. Kama walivyoleta mavuno ya shukrani, hivyo hivyo wamletee Mfalme wao Yesu Kristo aliyewabariki kabla ya kilimo.

Bulabo na sherehe ya Ekaristi

Kwa sababu kulikuwa na kucheza na shangwe, akaunganisha kwamba siku ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu watu wasali misa halafu baadaye wafanye maonesho ya ngoma za kila aina. Kwa sababu hiyo katika maandamano, watoto hurusha maua huku wakimsifu Yesu wa Ekaristi, hapo hata jina la bulabo (maua) lilipata maana na kuanza kuitwa Sherehe ya Bulabo.  Mpaka sasa jina la Sherehe ya Ekaristi limefunikwa na jina la Bulabo katika maeneo mengi ya Wasukuma.  Hata hivyo ikumbukwe pia kuwa neno Ekaristi limetokana na neno  la Kiyunani (Kigriki) “eucharistia” likiwa na maana ya “kushukuru,” kumbe kushukuru ikawa katika Mtemi kwa maana ya Yesu, Mfalme wa Wafalme na Bwana wa Mabwana. Toka hapo, limekuwa likipata umaarufu wa kijamii na kisiasa kwa sababu pia liko katika eneo muhimu na kitovu cha Utamaduni.

Rais wa Tanzania akitazama maonesho ya makumbusho huko Bujora
Rais wa Tanzania akitazama maonesho ya makumbusho huko Bujora   (©TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Nini manufaa yake?

Kongamano hili la Bulabo kama ilivyoelezwa limefanikiwa kuwavuta zaidi na zaidi watu kwa Kristo kwa njia rahisi na inayoeleweka katika mazingira yao. Kristo hakuja kutangua torati bali kutimiliza (rej Mt 5:17-20), kwa maana hiyo Bulabo imekuwa ni njia ya kuheshimu mwanzo mzuri wa Wasukuma waliokuwa wanamtukuza Muumbaji wao kwa kuwasimamia salama katika kazi zao kwa mwaka mzima. Kuadhimisha Ekaristi kama shukrani ni kilele cha maadhimisho yote katika Kanisa (Sacrosanctum Concilium, 10).

Kongamano la Bulabo, linakuwa muktadha mzuri wa Mama Kanisa kuendelea kujipambanua kwamba kweli yeye ni mama wa wote anayekumbatia wote kutoka kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, lakini wote wakiwa wamesimama katika kiti cha enzi, na mbele ya Mwanakondoo (rej.Ufunuo 7:9). Ni wajibu Mtakatifu unaoliangukia Kanisa hasa katika mtindo wake mpya wa utume kwa njia ya utamadunisho (enculturation and contextualization).

Changamoto

Pamoja na nia njema iliyokuwepo toka mwanzo, Kongamano hili katika historia yake limekuwa likipata changamoto kadhaa. Zipo za ndani na za nje, baadhi ya waamini kujali zaidi maandalizi ya nje na sherehe kuliko Misa yenyewe. Hii inafifisha umaana wake uliolengwa toka mwanzoni. Kwa sababu ya msingi wake kugusa jamii, kuna changamoto ya watu wasiojua msingi wake kuingia na kulazimisha liwe na muono wa kidunia zaidi kuliko wa kiimani hasa katika mlengo wa kisiasa  na  kwa upande wa fursa ni Kanisa kufungua mlango wa ushirikiano na serikali.

Ekaristi Takatifu chanzo cha Uzima wetu
Ekaristi Takatifu chanzo cha Uzima wetu   (@Vatican Media)

Tunaweza kuthibitisha kwamba Yesu Kristo katika Ekaristi, ni nuru ya kuangazia ulimwengu, akawe nuru kwa kila mmoja huku akiendelea kutulisha sisi tulio mahujaji wa  matumaini kwa Mwili na Damu yake ili tupate nguvu hadi tuufikie uzima wa milele mbinguni.

Sherehe za Bulabo huko Bujora nchini Mwanzo
23 Juni 2025, 15:41