ĐÓMAPµĽş˝

Njoo Roho Mtakatifu. Njoo Roho Mtakatifu. 

Pentekoste 2025,Ask.Mkuu Amani:Roho Mtakatifu ni chombo cha mawasiliano na amani!

Katika fursa ya Sherehe ya Pentekoste itakayoadhimishwa Juni 8,Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha,Tanzania,ametoa salamu zake kupitia video:“Siku ya Pentekoste,Roho Mtakatifu alirudisha lugha moja. Watu mbalimbali wakaweza kusikilizana.Lugha ni chombo cha mawasiliano. Huleta umoja,maelewano na mafanikio ya pamoja.Tumuombe Roho Mtakatifu aziponye familia zenye migogoro,jumuiya,mataifa yanayozozana yawe na fikra za kuacha uhasama."

"Tunapotamani ufalme wa Mungu ufike, tunapaswa kuukaribisha Ulimwengu na uinuke kwa tarajio la uhakika la Mbingu mpya na Dunia mpya. Nguvu za uovu zishindwe ili utukufu wa Mungu udhihirike milele katika taasisi zetu na ulimwenguni kote. Nguvu za uovu zitashindwaje tusipozipiga vita na kuzishinda? Utukufu wa Mungu utadhihirikaje tusipoukumbatia kwa sala,sakramenti na kulitii neno la Mungu? Wakati wa wokovu ni sasa. Tunaalikwa tubadilike sasa,tusingoje kesho.” Kanisa limetuandaa kwa Novena ya siku tisa na Kongamano pia ili tuweze kuadhimisha Pentekoste vizuri. Huu ni wakati wa neema ni wakati maalum wa kukuza na kuimarisha imani. Kwa namna ya pekee mwaka huu tunaadhimisha Jubilei ya miaka 2025 ya ukristo. Jubilei hii yatukumbusha sisi kuwa ni mahujaji wa matumaini. Je unaiona Jubilei kuwa fursa ya wokovu au ni tukio la kawaida tu kwako?" Haya na Mengine mengi yamo kwenye Salamu za Pentekoste zilizochapishwa tarehe 4 Juni 2025 kwenye ukurasa wa "Jimbo Kuu Katoliki Arusha Online TV" na Askofu Mkuu Isaac Amani, wa Jimbo Kuu la Arusha nchini Tanzania. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inachapisha tafakari nzima na kuambatanisha Video hiyo.

Askofu Mkuu Isaac Amani

Tumsifu Yesu Kristo!

Mimi ni Askofu Mkuu Isaac Amani wa Jimbo kuu Katoliki la Arusha na ninayo furaha kuja tena mbele yenu wapendwa, wapenzi wa Mungu familia ya Mungu, Wakristo na wasio wakristo, kukutakieni ujumbe na salamu za Pentekoste. Tumejiandaa kwa ajili ya kuadhimisha siku ambapo Kanisa lilizaliwa na tunamshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kuona siku hii ya leo. Wengi walitamani kuiona lakini basi, kwa namna mbalimbali wameshindwa kuiona. Kabla ya kupaa mbinguni kwa Bwana wetu Yesu Kristo, mwenyewe aliahidi kwamba angempeleka Roho Mtakatifu ambaye ni msaidizi wa kuwa nasi ambaye atakaa nasi na atakaa ndani mwetu. Alituambia yeye ni roho wa ukweli na roho huyo ulimwengu hauwezi kumpokea kwa sababu hauwezi kumuona wala kumjua. Lakini ninyi mnamjua kwa sababu anabaki nanyi na yu ndani yenu(rej Yh 14: 17.) Katika Pentekoste tunashangilia kutimia kwa ahadi ya kupewa zawadi ya Mungu roho Mtakatifu na mwanzo rasmi wa Kanisa.

Nawatakieni wote herini na baraka za Pentekoste. Inafaa basi tuombe neema ya kumtii huyu Roho Mtakatifu ambaye ndiye msaidizi wetu sasa na siku zote. Siku ya Pentekoste jambo la kawaida lilikuwa tu watu wakutane kwa hali ile walikuwa kwenye hali ya hofu. Lakini siku ile ya Pentekoste Roho Mtakatifu alipoishukia jumuia ya wafuasi, walikuwa wamejificha wamekusanyika ndani. Upepo wa nguvu ulijaza nyumba walimokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana na wote wakajazwa Roho Mtakatifu. Mambo matatu yalifanyika siku hiyo ya kipekee. Kwanza, wote walijazwa Roho Mtakatifu. Pili, mitume walibadilika tabia zao za hofu wakawa na ujasiri wa ajabu. Wakatoka mafichoni na kuhubiri Injili na kuishuhudia kwa ujasiri wa ajabu. Na la tatu, waamini walibadilika wakawa na umoja na uelewano uliowavutia watu wengi wakajiunga nao. Ndivyo ahadi ya Yesu ilivyotimia kwamba Roho Mtakatifu awe ndani ya wafuasi wake na kati yao. uwepo wake ndani yetu huonekana katika mabadiliko kama vile upepo uvumavyo na kutikisa mimea, vichaka na miti. Tujikabidhi basi kwake ili atubadilishe tuwe bora zaidi.

Kanisa limetuandaa kwa Novena ya siku tisa na Kongamano pia ili tuweze kuadhimisha Pentekoste vizuri. Huu ni wakati wa neema ni wakati maalum wa kukuza na kuimarisha imani. Kwa namna ya pekee mwaka huu tunaadhimisha Jubilei ya miaka 2025 ya ukristo. Jubilei hii yatukumbusha sisi kuwa ni mahujaji wa matumaini. Je unaiona Jubilei kuwa fursa ya wokovu au ni tukio la kawaida tu kwako? Katika sala ya Jubilei tunamuomba Baba wa mbinguni imani aliyotujalia kwa mwanaye Yesu, Kristo ndugu yetu iamshe ndani yetu tumaini lenye baraka la kuja kwa ufalme wake. Ni mwali wa upendo unaowashwa mioyoni mwetu na Roho Mtakatifu uweze pia kuamsha ndani yetu tumaini lenye baraka la kuja kwa ufalme wake. Neema yako itubadilishe kuwa wakulima wenye bidii wa mbegu za kiinjili zinazofanya ubinadamu. Tunaomba kuzaliwa upya. Tunaomba kujitambua kuwa tumeteuliwa kuwa taifa la Mungu lenye kuunganishwa na Roho Mtakatifu. Palipo na Roho kuna upendo, umoja na uponyi. Roho Mtakatifu ndiye nguvu mpya ya utendaji katika safari ya matumaini ya kwenda mbinguni.

Askofu Mkuu Isaac Amani akitoa salamu za Pentekoste 2025

Mapaji yake saba yakifanya kazi katika maisha yetu na mahusiano yetu matokeo yake ni mabadiliko ya ndani ya kutoa na kuomba msamaha, kuwajali wengine tukiwafikiria na kuwatendea kwa haki na kuwatetea walio dhaifu tunaposafiri kuiendea tamati ya ubatizo wetu yaani mbinguni. Roho Mtakatifu ni Mungu asimamiaye mabadiliko ya ndani ili tutoke kwenye ubaya wa uhasama, chuki, ufisadi, kisasi, wivu, ukatili, hofu, udanganyifu na kutojali kuteuliwa na kukombolewa kwetu. Tukizingatia wito wa kuwa chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu, yatupasa tuombe msaada wa Roho Mtakatifu ili tuweze kutimiza wito wetu sawasawa. Chumvi isipoyeyuka haitakoleza chakula. Taa isipokuwa na mafuta haitaangaza. Vivyo hivyo maisha ya mkristo ni ya mapambano dhidi ya maovu ndani mwake na katika jamii inayomzunguka. Yesu mwenyewe aliyeionesha njia hiyo kwa mateso, kifo na ufufuko wake kisha akampeleka Roho Mtakatifu ili atuwezeshe kuifuata njia ya wokovu kwa ujasiri. Watu walipoungana kwa kiburi kujenga mnara wa kufika mbinguni ili wajipatie jina, Mungu alivuruga lugha yao wakashindwa kujenga Mnara wa Babeli.

Siku ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alirudisha lugha moja. Watu mbalimbali wakaweza kusikilizana. Lugha ni chombo cha mawasiliano. Huleta umoja, maelewano na mafanikio ya pamoja. Tumuombe Roho Mtakatifu aziponye familia zenye migogoro, jumuiya, mataifa yanayozozana yawe na fikra za kuacha uhasama na kutafuta maendeleo ya pamoja kwa ustawi wa mwanadamu. Tunapotamani ufalme wa Mungu ufike, tunapaswa kuukaribisha Ulimwengu na uinuke kwa tarajio la uhakika la Mbingu mpya na Dunia mpya. Nguvu za uovu zishindwe ili utukufu wa Mungu udhihirike milele katika taasisi zetu na ulimwenguni kote. Nguvu za uovu zitashindwaje tusipozipiga vita na kuzishinda? Utukufu wa Mungu utadhihirikaje tusipoukumbatia kwa sala, sakramenti na kulitii neno la Mungu? Wakati wa wokovu ni sasa. Tunaalikwa tubadilike sasa, tusingoje kesho.

Tukitafakari hali halisi katika jamii tunashuhudia kupotea kwa imani na kushamiri kwa uvunjifu wa haki na amani kwa namna mbalimbali za kutisha. Tarajio la Mbingu mpya na Dunia mpya sio la kimuujiza. Furaha na amani ya mkombozi haitashuka kimuujiza. Ufalme wa Mungu huja kwa mwaliko wa Mungu na muitiko wa mwanadamu. Yesu aliweka wazi. “Roho ndio iletayo uhai, mwili hauwezi kitu. Maneno niliyowaambia ni roho na uhai. Hakuna awezaye kuja kwangu asipowezeshwa na Baba yangu”(rej.Yh 6:63 na 65). Kama mkiyazingatia mafundisho yangu mtakuwa kweli wanafunzi wangu. Mtaujua ukweli nao ukweli utawapeni uhuru(rej. Yh 8:31- 32.) Anayetupatia uhuru wa kweli ni Mungu. Tunamhitaji Roho wa Mungu afanye kazi ndani mwetu ili tuifikie tamati itokayo kwa Mungu. Nabii Yoeli, alieleza ukarimu wa Mungu wa kumimina roho yake juu ya binadamu wote. “Watoto wenu wa kike na wa kiume watatabiri. Wazee wenu wataota ndoto na vijana wenu wataona maono(Yoeli 2:28). Tunajiuliza je watoto wetu wanapata malezi na mafundisho ya kuwasaidia kuchagua yaliyo bora na ya kudumu katika maisha ya sasa na ya uzima wa milele wakiongozwa na Roho Mtakatifu? Je vijana wetu wanapenda kazi na kutumia muda wao kujifunza namna mbalimbali za kukabili maisha wakiongozwa na Roho Mtakatifu? Je wazee wanasimulia na kurithisha ujasiri wa kuishi na kueneza Injili kwa maisha yao binafsi na kwa utendaji wao?

Pentekoste inatukumbusha utabiri wa nabii Yoeli wa mafundisho ya roho wa Mungu ulivyotimizwa katika mioyo na akili za watu ili wabadilike waweze kuwa rafiki wa Mungu na wa watu. Anachotaka Mungu kwetu ni utukufu wake uonekane katika maisha yetu, katika familia na jumuia zetu, katika vigango na Parokia zetu, katika Jimbo na Taifa letu na katika Kanisa lake lote na ulimwenguni mzima. Yesu aliyetuombea umoja wa kimungu ambao huletwa na Roho Mtakatifu. “Wote wawe na umoja kama wewe Baba ulivyo ndani yangu. Nami ndani yako hao nao wawe ndani yetu ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao nawe ndani yangu ili wawe wamekamilika katika umoja ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi”(rej.Yh 17: 21-23.)

Kwa kumalizia, umoja anaotuombea Yesu ndiyo ushuhuda wa mapendo na nguvu ya utume wetu. Tunazo fursa nyingi za kuimarisha umoja na mapendo. Tuimarishe umoja na mapendo nyumbani na jumuiani kwanza. Tuimarishe umoja na mapendo katika vyama, mashirika na jumuiya za Kitume. Tuimarishe umoja na upendo katika uchumi, siasa na hasa kuuombea na kujipanga vizuri kwa uchaguzi mkuu ulio mbele yetu. Tukifanya hivyo tutakuwa tumempa Roho Mtakatifu nafasi ya kutubadilisha, kutujenga na kutuponya. Tukifanya hivyo furaha na amani ya mkombozi vitadhihirika katika safari ya matumaini. Nawatakieni heri na baraka za Roho Mtakatifu katika kujitambua, kuwajibika na kushirikiana katika Kristo kwa matendo.

Mimi katika Kristo Askofu Amani.

Herini kwa siku kuu ya Pentekoste!

Njoo Roho Mtakatifu
Njoo Roho Mtakatifu
05 Juni 2025, 11:13