MAP

Mitume Petro na Paulo ni mashuhuda wa Injili kiasi hata cha kumwaga damu yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Mitume Petro na Paulo ni mashuhuda wa Injili kiasi hata cha kumwaga damu yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa.   (@Vatican Media)

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Umoja, Ushuhuda na Gharama ya Ufuasi!

Sherehe hii inatufakarisha juu ya, “Umoja na Ukatoliki wa Kanisa, Ushuhuda wa Imani ya Mitume na Gharama ya Ufuasi wa Kweli kwa Kristo Yesu.” Katika Sherehe hii, tuliombee Kanisa liendelee kudumu katika umoja na msingi imara kwa mafundisho ya Mitume hawa wa Kristo, licha ya tofauti zetu. Tuwaombee viongozi wote wa Kanisa, Papa Leo XIV, Maaskofu na Mapadre ili waendeleze wajibu huu wa Mitume wa kuliongoza Kanisa; Kufundisha na kuhubiri Injili ya Kristo Yesu

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, Petro, Mchungaji imara wa kundi la Kristo na Khalifa wa kwanza wa Kristo, na Paulo Mtume Hodari wa Injili ya Kristo kwa watu wa mataifa. Ijapokuwa Mitume hawa walikuwa na utofauti mkubwa katika historia zao, wote walikua na mapendo makubwa kwa Kristo na kujitoa bila woga katika kumtangaza Kristo hata wakafa kifo dini. Sherehe hii inatufakarisha juu ya, “Umoja na Ukatoliki wa Kanisa, Ushuhuda wa Imani ya Mitume na Gharama ya Ufuasi wa Kweli kwa Kristo Yesu.” Katika Sherehe hii, tuliombee Kanisa liendelee kudumu katika umoja na msingi imara kwa mafundisho ya mitume hawa wa Kristo, licha ya tofauti zetu watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa. Tuwaombee viongozi wote wa Kanisa, Baba Mtakatifu wetu Leo XIV, Maaskofu na Mapadre ili waendeleze wajibu huu wa Mitume wa kuliongoza Kanisa; Kufundisha na kuhubiri Injili kwa watu wa Mataifa na kuendelea kuwatakatifuza watu wa Mungu. Tujiombee nasi sote ili tudumu imara katika umoja licha ya tofauti zetu. Tuwaombee pia wale wote wanaofanya utume katika mazingira magumu, wanaoteseka kwa ajili ya Imani yao kwa Kristo ili kamwe wasikate tamaa bali kwa maombezi ya Watakatifu hawa waendelee kumtangaza Kristo bila woga. Tumshukuru Kristo ambaye alipenda kulijenga kanisa lake juu ya misingi imara ya mitume, ambao waliishuhudia imani yao kwa maneno na kwa matendo na Damu yao iliyomwagika ikawa mbegu na chachu ya kukua na kuenea kwa Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa yote.

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo nguzo za Kanisa
Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo nguzo za Kanisa   (@Vatican Media)

Mitume Petro na Paulo: Mtume Petro alikuwa ni mvuvi huko Betsaida katika Galilaya. Ni mwana wa Yona na ndugu wa Andrea. Alipoitwa na Kristo aliacha vyote na kumfuata (Mt 4:18-22; Lk 5:1-11) akiongozwa kuja kwa Kristo na nduguye Andrea. Ni mtume wa kwanza kumuungama Kristo akimwambia, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai” (Mt 16:16, Lk 9:20). Kristo alimweka kuwa mchungaji wa kundi lake, yaani Kanisa (Mt 16:18). Baada ya Pentekoste aliwaongoza na kuwabatiza watu wengi, akalisimamia Kanisa la Antiokia na kisha akahamia Roma na kuwa Askofu wa kwanza wa mji huo.  Mnamo mwaka 66, Kaizari Nero aliutia moto mji wa Roma, akawasingizia wakristo kuwa ndio waliouchoma moto. Akaamuru wakamatwe na watakaokataa kukana dini na imani yao wauwawe. Petro na Paulo walitiwa gerezani, wakawa wakifundisha na kubatiza humo humo gerezani. Tarehe 29/06 mwaka 67 yeye pamoja na mtume Paulo waliuwawa. Mt Petro aliomba asulubiwe kichwa chini miguu juu, kwa kuwa aliona hana mastahili ya kusulibiwa kama Mkombozi wake. Mtume Paulo, yeye alikuwa hapo mwanzo mtesi wa Kanisa na Wakristo. Lakini badae alikutana na Kristo Mfufuka akiwa njia kuelekea Damasko kuwatesa Wakristo. Neema ya Kristo ilimbadilisha na akaanza kwa nguvu kuhubiri Injili. Watu wote walishangaa na kusema, “Si huyu aliyekuwa akiwafunga na kuwatesa wakristo? Lakini Paulo aliendelea kuhubiri Injili bila kujali wala kuogopa kutukanwa na kuteswa kwa ajili ya Kristo, akihubiri Injili kwa Wayahudi hali kadhalika kwa watu wa Mataifa. Mwishoni alitiwa gerezani huko Roma pamoja na Petro na kisha kuuwawa na Kaizari Nero kwa kukatwa kichwa.

Maaskofu wakuu 54 wamevishwa Pallio Takatifu
Maaskofu wakuu 54 wamevishwa Pallio Takatifu   (@Vatican Media)

Somo la Injili: Ni Injili ya Mathayo 16:13-19. Katika somo hili la Injili Takatifu, Kristo Yesu akiwa Kaisaria Filipi, ilipokuwa kitovu cha watu wa Mataifa, anawauliza Mitume wake swali msingi sana. Anawauliza juu ya utambulisho wake kwa watu, lakini kwa namna ya pekee anataka kujua nao wanamtambua yeye kuwa ni nani. Mitume wanatoa majibu mbalimbali. Mtume Petro kati ya Mitume wengine wote, anamkiri Kristo na kumtambua kuwa yeye ni Masiya mwana wa Mungu. Kristo katika kumjibu, anadhihirisha nafasi na utume wa Petro kati ya Mitume wenzake na katika kanisa la Mwanzo kama “Mwamba”, msingi imara ambapo juu yake Kristo atalijenga kanisa lake (Mt 16:16-19.) Kristo Yesu anamdhirishia Petro kuwa nguvu hiyo ya kumkiri kwa hakika haikua yake bali ni Baba yake aliye mbinguni, kwa kuwa Petro alikua pia dhaifu kibinadamu. Mtume Petro anapewa funguo, anapewa uwezo wa kufunga na kufungua, ishara ya Mamlaka (Authority). Kristo anaahidi kuwa pamoja na Kanisa lake, ambalo licha ya mahangaiko mbalimbali bado litabaki imara chini ya Kristo, chini ya msingi imara wa Mitume hawa wa KRisto. Somo la Kwanza: Ni kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume 12:1-12. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaelezea maisha na utume wa Kanisa la Mwanzo sanjari na maisha ya Mitume wa Yesu baada ya Yesu kuteswa, kufa na kupaa kwake mbinguni, na utume na maisha ya jumuiya hii ya kwanza baada ya Pentekoste. Katika picha hiyo, somo la kwanza tulilolisikia, kutoka kitabu cha matendo ya Mitume laeleza tukio la kukamatwa na kuwekwa gerezani Mtume Petro. Tukio hili lilitokea wakati wa utawala wa Herode Agrippa (41-44 AD) aliyekuwa mtawala wa dola ya kirumi wakati huo. Somo hili latupa picha ya maisha halisi ya Mitume hawa wa kwanza wa Kristo, kanisa na wakristo wa kwanza, namna walivyokuwa tayari kuteseka kwa kuiishi, kuishuhudia na kuifundisha Imani yao. Herode Agrippa alikwisha kumwua Yakobo ndugu yake Yohane, aliyekuwa mtume wa kwanza kufa kifo dini. Sura hii ya 12 ya kitabu cha matendo ya Mitume yasimama kama Daraja kati ya utume wa Mtume Petro huko Yerusalemu, na utume wa Mtume Paulo kwa watu wa mataifa. Ijapokuwa somo hili laezea zaidi kuhusu Mtume Petro lakini latupa picha ya utume mpana zaidi wa kanisa ambao ulifanywa na Mtume Paulo na kulifanya kanisa kuendelea kusambaa na kuwapokea watu wote (Universality/Catholicity) na ndio sababu somo hili linasomwa katika Sherehe hii ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume.

Watakatifu Petro na Paulo Ni Mahujaji  wa imani, matumaini na mapendo
Watakatifu Petro na Paulo Ni Mahujaji wa imani, matumaini na mapendo   (@Vatican Media)

Somo la pili: Ni Waraka Pili 2 Tim 4:6-8, 17-18: Waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Timoteo unasemekana kuwa ndio waraka wa mwisho wa Mtume Paulo ambao aliuandika akiwa gerezani kule Mjini Roma mnamo mwaka 67 AD, muda mchache kabla ya kukatwa kichwa na kufa kifo dini. Anaeleza namna alivyoachwa na watu wengi isipokua watu wachache tu ambao walibaki karibu naye katika nyakati za mwisho za maisha na utume wake. Anasadiki kuwa amefanya yake ya kitume vyema na kwa uaminifu mkubwa, kwa hivyo anajua hakika kuwa Mungu atampa tuzo. Somo hili linaweka mbele yetu katika Sherehe hii ya Watakatifu Petro na Paulo kuonesha namna Mtume Paulo alivyobaki mwaminifu kwa Kristo hata akakubali kufa kifo dini kwa ajili ya Injili. Ndugu mpendwa katika Sherehe ya Mitume Petro na Paulo tuna mambo yafuatayo ya kujifunza.  Kwanza: Kristo anapotuita, anatuita kuacha vyote na kumfuasa. Mtume Petro aliitwa na Kristo kutoka katika kazi yake ya kawaida kabisa, kazi ya kuvua Samaki huko Bethsaida. Aliacha vyote na akawa tayari kumfuata Kristo. Mtume Paulo hali kadhalika alikua hapo Mwanzo akilitesa na kuliumiza kanisa la Kristo. Alipokutana na Kristo akiwa njiani kuelekea Damasko, aliongoka, akaacha maisha yake ya zamani na akamfuasa Kristo kwa nguvu, ari na nguvu mpya, akawa mtume Hodari wa Injili kwa watu wa mataifa yote. Ndugu mpendwa, Sherehe hii ya Watakatifu Petro na Paulo inatukumbusha nasi sote juu ya wito wetu wa ufuasi kwa Kristo, tukiwa sote kila mmoja kama kiungo cha mwili wa Kristo yaani kanisa. Kwa nafasi ya wito wetu wa kwanza kama Wakristo kwa njia ya ubatizo, tunaachana na maisha ya zamani na kuanza maisha mapya ndani ya Kristo, ambapo tunavua utu wetu wa kale, yaani maisha ya dhambi na kuanza maisha mapya ndani ya Kristo. Wito wa mtume Petro watukumbusha wajibu wetu wa kujikatalia, kukubali kuacha ndugu, jamaa, marafiki, familia na kuitika wito wa Mungu kila mmoja kwa namna ambayo Kristo anataka tumtumikie. Tunapoitika wito wa Mungu na bado tumejishikamanisha na malimwengu hatuwezi kumtumikia vyema Kristo vile inavyopaswa.

Maaskofu 54 wamevikwa Pallio Takatifu mjini Vatican
Maaskofu 54 wamevikwa Pallio Takatifu mjini Vatican   (@Vatican Media)

Tunapaswa kumpa Kristo nafasi ya kwanza, kisha mambo mengine tutayafanya vyema na kwa baraka zake nyingi. Tunapoamua kumfuata Kristo tunakuwa tayari kuacha mambo ya kale, mawazo yetu, fikra zetu, matamanio yetu, hofu na mashaka yetu, kukata tamaa kwetu, na kuweka matumaini yetu yote kwa Kristo aliyetuita kumtumikia. Ni katika wito wa ndoa Takatifu, mtegemee Kristo aliyekuita, ni katika Utawa, mtegemee Kristo, ni katika upadre, mtegemee Kristo aliyekuita, ni katika kutafakari juu ya hatima ya maisha na wito wako, mtegemee Mungu. Weka matumaini yako yote kwake kwamba, atakutegemeza. Pili: Je, Kristo ni nani kwangu? Kristo anawauliza mitume akitaka kujua watu wanasema kuwa yeye ni nani, anapowauliza, “Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Lakini muhimu zaidi, anataka kufahamu kutoka kwa kila mmoja wao kwamba yeye ni nani kwao? Ndipo hapo mtume Petro anakiri kuwa, “Wewe ndiwe Kristo mwana wa Mungu aliye hai” Petro anamkiri Kristo kama masiya, kama mkombozi. Kumbe kukiri imani ni msingi imara wa ufuasi wa kweli kwa Kristo, imani ambayo inalindwa, inatetewa, imani inayopaswa kuwa hai, imani inayoishi. Ndugu mpendwa, katika somo la Injili Takatifu, mwinjili Mathayo anaweka msisitizo katika neno, “ὑμεῖς” yaani, “Nanyi”, akimaanisha kuwa swali hili ni letu sisi sote tulio wafuasi wa Kristo. Je, Kristo ni nani kwangu? Swali hili lagusa moja kwa moja mahusiano yangu binafsi na Kristo. Ninamtambua na kumkiri Yesu kwa maneno, kwa imani thabiti na matumaini hai kama Kristo, kama Masiha, Bwana na mkombozi wetu?

Watakatifu Petro na Paulo ni Mashuhuda wa Umoja na Damu
Watakatifu Petro na Paulo ni Mashuhuda wa Umoja na Damu   (ANSA)

Mara kadhaa ninakua na imani thabiti pale mambo yanapokuwa shwari, ila zijapo changamoto, yajapo magonjwa, zijapo dhiki na mahangaiko mengine ya maisha ninaanza kuwa na hofu na kusita juu ya imani yangu kwa Kristo, na ndicho atakachoonesha Mtume Petro mara baada ya Kristo kutabiri juu ya mateso na kifo chake. Wakati mwingine tumekuwa wepesi na warahisi kutafuta suluhisho la haraka la changamoto zetu mbalimbali, kutafuta majibu ya haraka ya maswali yetu na kusahu kuwa Kristo anajua yote, anafahamu mambo yote tunayopitia katika maisha yetu ya ufuasi. Pengine nimekuwa na picha ya Kristo anayetenda miujiza, anayejibu kwa wakati, anayenibariki kwa wakati na kusahau kuwa Kristo anayatenda hayo yote kwa wakati wake, sio kwa mapenzi yetu sisi. Mitume hawa wa Kristo licha ya kwamba walikua dhaifu, waliimarishwa na Roho Mtakatifu na kweli walimkiri Kristo hata kuwa tayari kutoa maisha yao na kufa kifo dini. Tumwombe Roho Mtakatifu azidi kutuimarisha kila mmoja ili tumtambua na kumkiri daima Kristo katika hali zote. Tatu: Nguvu ya kumkiri Kristo inatoka kwa Mungu mwenyewe. Baada ya Petro kumkiri Kristo kuwa ni Mwana wa Mungu aliye juu, Yesu anamwambia kuwa si mwili na damu vilivyomfunulia hayo bali ni Baba wa Mbinguni. Nguvu ya mitume hawa wa Kristo ya kumkiri Kristo, kuiishi na kuishuhudia imani yao ilitoka kwa Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu waliyempokea siku ya Pentekoste. Walipata ujasiri wa kumkiri Kristo hata kuwa tayari kufa kifo dini. Ndugu mpendwa, nguvu ya kumkiri Kristo haitoki kwetu sisi wenyewe bali ni Roho Mtakatifu anayekaa ndani mwetu anayetusaidia kumkiri na kumshuhudia Kristo kwa wengine. Tunapaswa kumruhusu daima Roho Mtakatifu ambaye tumeimarishwa naye kwa sakramenti ya kipaimara ili atuongoze katika kuikiri imani ya kweli kwa Kristo mbele ya wengine, bila hofu, bila mashaka yoyote hata kama itatugharimu maisha yetu kama ilivyokuwa kwa mitume hawa Petro na Paulo na mitume wengine wa Kristo Yesu!

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani.
Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani.   (@VATICAN MEDIA)

 Nne: Kristo amelijenga Kanisa lake juu ya msingi wa Mitume. Mtume Petro anaambiwa na Kristo, “Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda”. Petrus, yaani mwamba ni ishara ya msingi imara na mamlaka. Petro anawekwa na Kristo kuwa Kiongozi wa Kanisa, jumuiya mpya ya waamini. Ni kanisa ambalo litapita katika madhulumu na mateso mengi, licha ya hayo, litabaki imara kwa kuwa Kristo ndio kichwa cha kanisa imara alilolijenga juu ya misingi ya Mitume. Ndugu mpendwa, wajibu na nafasi hii ya Mtume Petro ndiyo nafasi ya Baba Mtakatifu hata sasa kama Khalifa wa Mtume Petro. Pamoja na maaskofu ambao wanachukua nafasi ya mitume, kazi ya kuitangaza Injili ya Kristo kwa watu wote inafanyika kwa nguvu, moyo na ari hata sasa. Siku hii tunaalikwa kumwombea Baba Mtakatifu wetu Leo XIV, khalifa wa mtume Petro, mwamba imara aliyekabidhiwa funguo na Kristo mwenyewe, ishara ya mamlaka, ya kufundisha, kuongoza, kuilinda imani na kuadhimisha sakramenti mbalimbali ambazo zinawasaidia taifa la Mungu kufunguliwa mlango wa mbinguni. Tuwaombee Maaskofu wetu ili wawe imara katika kusimamia mafundisho ya kanisa kama ilivyokuwa kwa mitume hawa wa kwanza wa Kristo, wawe na moyo na ari ya kulichunga kundi la Kristo bila kuchoka, kusema ukweli, kutetea haki na amani katika ulimwengu wa leo ambao umejaa kila aina ya changamoto ambazo pia zinalishambulia kanisa. Tujiombee na sisi sote ili daima tutambue kuwa imani yetu imani hii ya mitume ndio imani yetu sisi tulio wafuasi wa Kristo leo hii. Tumejengeka juu ya mwamba imara, hatuna hofu, hatuna mashaka kwa kuwa Kristo ndiye kichwa cha kanisa ambamo sisi sote tumeitwa kuwa viungo ya mwili wake. Hatuna mashaka, hatuna hofu kwa kuwa Kristo yupo nasi daima mpaka ukamilifu wa dahari. Tuziweke familia zetu mikononi mwake, shughuli zetu za kila siku mikononi mwake, watoto wetu mikononi mwake, tuweke hali zetu mbalimbali tunazopitia mikononi mwake, tumwombe atuongezee imani ili tuendelee kuwa imara ndani yake aliye Bwana na mwalimu wetu.

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani.
Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani.   (@Vatican Media)

Tano: Kristo analilinda Kanisa lake, anawalinda watumishi wake, anatulinda sisi sote. Katika somo la kwanza, tumesikia namna Mtume Petro, alivyotolewa gerezani na Mungu mwenyewe. Somo hili latuonesha dhahiri kuwa, Mungu aweza kutenda yote na daima yupo tayari kuwasaidia wale wote wanaomtumainia. Kristo mwenyewe alimwambia Petro kwamba, hata nguvu za kuzimu hazitaweza kulishinda kanisa, akitambua kuwa kuna nyakati mitume watapita katika nyakati ngumu ila Kristo yupo pamoja nao. Ndugu wapendwa Kristo daima anatulinda, dhidi ya hila na mitego ya mwovu shetani. Anatulinda dhidi ya yale yote yanayoweza kutudhuru. Yupo daima ndani mwetu, katika Neno lake na katika sakramenti. Anatupa nguvu, anatupa ulinzi thabiti. Tunaalikwa kuweka matuini yetu yote kwake kama Mtume Petro alivyoyaweka matuamaini yake yote kwa Kristo, na Kristo akamlinda na kumwokoa kutoka gerezani ili aendelee na kazi ya kuitangaza Injili. Kristo anatulinda kwa kuwa anajua bado tuna kazi ya kufanya kwa ajili ya familia zetu, kwa ajili ya kanisa, kwa ajili ya wokovu wetu na wokovu wa wengine. Yesu ninakutumania, iwe sala yetu kila siku. Yesu atafanya jambo hata pale ambapo kibinadamu inaonekana haiwezekani kwa kuwa anatupenda na anatulinda. Sita: Kanisa ni moja licha ya tofauti zetu, tumeunganishwa sote. Mitume Petro na Paulo walikua na historia tofauti kabisa, waliitwa kwa nyakati tofauti. Licha ya tofauti zao, wote walifanya kazi kubwa katika kanisa. Mtume petro kama khalifa wa Kristo na Mtume Paulo kama mtume wa Injili ya Kristo kwa mataifa. Walifanya kazi hii kubwa, wakahubiri Injili kwa nguvu na kuwafanya watu wa mataifa yote kuwa wanafunzi wa Kristo. Licha ya utofauti wao, walifanya kazi ya kuliunganisha kanisa, likawajumuisha hata watu wa mataifa. Wakafungua milango na kuwapokea wote ndani ya kanisa, na ndivyo limekua katika historia na ndivyo lilivyo sasa. Ndugu mpendwa, sifa hii ya Mitume hawa wawili wa Kristo iwe chachu ya kutuleta pamoja kama ndugu licha ya tofauti zetu. Katika familia zetu huenda imekua ngumu kupokeana katika mazuri na madhaifu yetu. Huenda tofauti zetu zimekuwa chanzo cha migogoro, vita, chuki, wivu, visasi na vinyongo katika familia zetu, na katika jumuiya zetu. Huenda tofauti ya Mawazo, itikadi na mitazamo imekua chanzo cha ugomvi na uhasama katika jamii yetu, katika nchi zetu nk. Tuwaombe watakafu Petro na Paulo watuombee ili daima tofauti zetu ziwe utajiri wetu badala ya kuwa chanzo cha utengano.

Watakatifu Petro na Paulo Ni Mahujaji  wa imani, matumaini na mapendo
Watakatifu Petro na Paulo Ni Mahujaji wa imani, matumaini na mapendo   (@Vatican Media)

Saba: Gharama ya ufuasi wa kweli, kuteseka kwa ajili ya Kristo. Katika somo la Pili, mtume Paulo anaandika waraka wake wa mwisho, ni waraka wa pili kwa Timoteo. Anasema kwamba karibu anamiminwa na wakati wa kufariki kwake umekaribia. Aliandika waraka huu akiwa gerezani na baada ya muda si mrefu aliuwawa kwa kukatwa kichwa na kaisari Nero. Mitume na wakristo katika kanisa la Mwanzo walipitia katika mateso na magumu mengi kwa ajili ya imani yao. Mateso na madhulumu yalikua ni sehemu ya ufuasi wao, wengi walikufa kifo dini. Kwa njia ya mateso na madhulumu, kanisa likaendelea kusambaa na kukua. Ndugu mpendwa, Mitume Petro na Paulo wanatufundisha kuwa, mateso, changamoto, madhulumu, ni sehemu ya ufuasi wetu, ndio msalaba wetu na ndio Gharama ya ufuasi wetu. Ufuasi wetu si lelemama, twapaswa kusimama imara. Tunaweza tusiwekwe gerezani kama ilivyokuwa kwa Mitume hawa wa kwanza, tunaweza tusiteseke kama Mitume hawa wa kwanza walivyoteseka, ila tunaishi katika ulimwengu ambapo tunahitaji kutoa ushuuda wa kweli wa maisha. Ulimwengu unaohitaji upendo, twapaswa kupenda kwa mapendo ya kweli, ulimwengu unaohitaji msamaha, twapaswa kusamehe na kutafuta kuwa na amani na watu wote, ulimwengu ambapo mafundisho ya uwongo yanapigiwa chapuo kuliko misingi ya kweli ya utu, tunapaswa kusimama na kupaza sauti, ulimwengu ambapo hakuna haki na usawa kati ya watu, tunapaswa kuwa mabalozi wa haki na usawa. Hii siyo kazi rahisi hata kidogo, inatudai majitoleo makubwa na uthubutu. Watakatifu hawa watuombee ili nasi tuwe mashuda wa Injili bila woga. Hitimisho: Katika Sherehe hii, tujiombee sote ili tudumu imara katika umoja licha ya tofauti zetu. Tuwaombee pia wale wote wanaofanya utume katika mazingira magumu, wanaoteseka kwa ajili ya Imani yao kwa Kristo ili kamwe wasikate tamaa bali kwa maombezi ya Watakatifu hawa waendelee kumtangaza Kristo bila woga. Tumshukuru Kristo ambaye alipenda kulijenga kanisa lake juu ya misingi imara ya mitume, ambao waliishuhudia imani yao kwa maneno na kwa matendo na Damu yao iliyomwagika ikawa mbegu na chachu ya kukua na kuenea kwa Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa yote. 

Maaskofu 54 wamevishwa Pallio Takatifu
Maaskofu 54 wamevishwa Pallio Takatifu   (ANSA)

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo ni Siku maalum ambayo imetengwa na Mama Kanisa ili kuonesha moyo wa upendo na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kuchangia kwa hali na mali ili kusaidia utekelezaji wa Injili ya huduma ya upendo, huruma na ukarimu inayomwilishwa katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mchango huu unalenga kufanikisha jitihada za huruma ya Mungu ambazo kimsingi zinafumbatwa katika Sakramenti za Kanisa na kumwilishwa katika huduma ya ukarimu na upendo kwa watu wanaosiginwa, utu, heshima na haki zao msingi kutokana na umaskini, ujinga na maradhi; kwa wakimbizi na wahamiaji; kwa watu wanaokumbwa na majanga pamoja maafa mbalimbali kwa sasa. Mchango huu unamwezesha Khalifa wa Mtakatifu Petro kuwa ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Pallio takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachotengenezwa na manyoya ya kondoo wachanga; na kinavaliwa mabegani na Baba Mtakatifu, Maaskofu wakuu wa majimbo makuu ya Kanisa Katoliki wanapokuwa katika majimbo yao pamoja na Mapatriaki. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Januari anaadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Agnes, Bikira na Shahidi, aliyeuwawa kunako karne ya tatu; akaonesha upendo wa pekee sana kwa Kristo Yesu mchumba wake wa daima, kiasi cha kuyasadaka maisha yake, ili asiuchafue ubikira wake. Yesu mwenyewe alitambulishwa na Yohane Mbatizaji kama Mwana Kondoo wa Mungu anayebeba na kuondoa dhambi za ulimwengu.

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Nguzo za Kanisa
Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Nguzo za Kanisa   (@VATICAN MEDIA)

Ni Mapokeo ya Kanisa kwamba, katika Sikukuu ya Mtakatifu Agnes, wanabarikiwa kondoo ambao manyoya yao yatatumika kutengenezea Pallio Takatifu, wanazovishwa Maaskofu wakuu katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, Mchungaji mwema, hata Maaskofu wakuu wanahamasishwa kuwabeba kondoo wao kama kielelezo cha wachungaji wema; daima wakikumbuka kwamba, wameteuliwa si kwa ajili ya masitahili na mafao yao binafsi, bali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya kondoo wa Kristo. Maaskofu wakuu wapya wanapaswa pia kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Pallio takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baada ya mabadiliko yaliyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2015, tangu wakati huo, Maaskofu wakuu wapya wamekuwa wakivishwa Pallio Takatifu na Mabalozi wa Vatican majimboni mwao, ili kuwashirikisha watu wa Mungu kutoka katika majimbo yanayounda Jimbo kuu husika tukio hili adhimu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Lakini, Baba Mtakatifu Leo XIV Dominika tarehe 29 Juni 2025 amerejea tena katika Mapokeo ya Mama Kanisa ya kuwavisha Pallio Takatifu Maaskofu wakuu na Mapatriaki 54 wakati wa Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

29 Juni 2025, 15:20