MAP

Mkutano Mkuu wa  46 wa WAWATA unanogeshwa na kauli mbiu “Saidia ambatana na kutia moyo familia.” 14-18 Juni 2025 Mkutano Mkuu wa 46 wa WAWATA unanogeshwa na kauli mbiu “Saidia ambatana na kutia moyo familia.” 14-18 Juni 2025 

Mkutano Mkuu wa 46 Wa WAWATA, Taifa: Hotuba ya Ufunguzi

Familia ni Kanisa dogo la nyumba, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii.

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, - Dar Es Salaam

Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni msingi wa Mafumbo yote yanayosherehekewa na Kanisa kwa nyakati mbalimbali. Hili ni Fumbo la imani na la maisha ya Kikristo. Ni Fumbo la Mungu ndani yake Mwenyewe. Mwenyezi Mungu katika historia na Mpango wa ukombozi amejifunua kuwa ni Mungu mmoja katika Nafsi Tatu. Baba Mungu Mwenyezi Mwumba mbingu na nchi, na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Kanisa linasadiki kwa Kristo Yesu, Mwana wa pekee, wa Mungu aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Ni Mungu aliyetoka kwa Mungu, Mwanga kwa mwanga. Mungu kweli kwa Mungu kweli. Aliyezaliwa bila kuumbwa, Mwenye umungu mmoja na Baba. Ndiye aliyeshuka kutoka mbinguni kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kanisa linasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana na mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa na Baba na Mwana: Aliyenena kwa vinywa vya Manabii.

Mkutano wa 46 wa WAWATA Taifa 14-18 Juni 2025
Mkutano wa 46 wa WAWATA Taifa 14-18 Juni 2025

Ni katika muktadha huu Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, katika maadhimisho ya Fumbo la Utatu Mtakatifu wamefungua Mkutano mkuu wa 46, katika Kituo cha Kiroho cha Msimbazi Center, Jimbo kuu la Dar es Salaam, mkutano unaonogeshwa na kauli mbiu “Saidia ambatana na kutia moyo familia.” Mkutano umeanza tarehe 14 na unahitimishwa tarehe 18 Juni 2025. Kanisa tangu mwanzo limekuwa likitoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa familia, kwa kutambua kwamba, Familia ni Kanisa dogo la nyumba, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii.

WAWATA katika Ubora wao, Misa ya Ufunguzi wa Mkutano mkuu
WAWATA katika Ubora wao, Misa ya Ufunguzi wa Mkutano mkuu

Ifuatayo ni hotuba ya ufunguzi iliyotolewa na Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti WAWATA, Taifa, Dominika tarehe 15 Juni 2025. Mhasham Baba Askofu Edward Mapunda, Askofu Mwenyekiti Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania – TEC na Askofu wa Jimbo la Singida, Padre Clement Kihiyo - Baba Mlezi, Wakurugenzi wa Majimbo, Masista walezi wa majimbo, Kamati Tendaji ya WAWATA Taifa, Viongozi wote wa Majimbo na watendaji wetu wa Ofisi, Tumsifu Yesu Kristo! Kwa furaha, unyenyekevu na shukrani tele, namshukuru Mungu kwa kutuwezesha kukutana tena kama familia ya WAWATA katika mkutano huu muhimu wa kitume. Ni zawadi isiyo ya kawaida kupewa nafasi ya kukutana uso kwa uso – kusali pamoja, kutafakari pamoja, kupngezana, kutiana moyo na kusonga mbele pamoja. Zaidi tumshukuru Mungu kwa namna ya pekee kwa kupata nafasi ya kuwatumikia na kuwawakilisha wengine tukitambua sisi sio bora kuliko wengine. Hebu kila mmoja wetu atafakari, jimbo lake lina WAWATA wangapi? Parokia, Je? Tanzania? 

Uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha huduma ya upendo
Uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha huduma ya upendo

Napenda kutoa shukrani za dhati kwa kila mmoja wenu kwa kujitoa, kwa kujisadaka bila kujibakiza katika utume huu. Nawapongeza kwa moyo wenu wa kujitoa – wengi wenu mmefanya safari ndefu, mkaacha familia zenu, mkiitikia mwaliko wa Kristo wa kutafuta kwanza Ufalme wa Mungu. Mungu awabariki kwa majitoleo yenu na asiwapungukie kamwe. Napenda kumshukuru Askofu mwenyekiti Baba Edward Mapunda na Idara ya kichungaji chini ya uongozi wa Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Baba Charles Kitima, Mlezi wetu Baba Benno Kikudo pamoja na Baba Clement Kihiyo ambao tumefanya nao kazi kwa mwaka huu. Shukrani pia kwa Kanisa – kwa kututambua na kuturuhusu wanawake kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kama ilivyoelezwa katika Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Wajumbe wa Mkutano mkuu wa WAWATA wakishiriki kikamilifu
Wajumbe wa Mkutano mkuu wa WAWATA wakishiriki kikamilifu

Nimshukuru Mungu na kutoa pole kwa Baba Benno na Baba Kitima, sote ni mashuhuda wa ukuu wa Mungu katika maisha ya Mababa hawa. Tuendelee kuwaombea Maklero wote na kuwatia moyo katika utume wao. Ni Dhahiri kila mmoja wetu anamhitaji Veronica wa kupangusa jasho na Simoni Mkirene wa kubeba nae msalaba. Mungu ametupatia Msaidizi, Roho Mtakatifu na Mama Bikira Maria, Mama wa kanisa na muombezi wetu. Pamoja na hawa, sisi sote tunaweza kuwa msaada kwa wengine na kusindikizana kwa upendo katika utume wetu. Nawaalika kila mmoja kuwa sehemu ya sababu ya kila mmoja wetu kuufurahia utume wetu.

Wajumbe wa WAWATA, wakiwa kwenye maandamano tayari kushiriki Ibada
Wajumbe wa WAWATA, wakiwa kwenye maandamano tayari kushiriki Ibada

Mkutano wetu mwaka huu wa 2025 una uzito wa kipekee kwa sababu ya mambo mawili: Moja: Mkutano wetu unafanyika ndani ya Mwaka wa Jubilei yenye kauli Mbiu – ‘Mahujaji wa Matumaini.’ Mkutano huu pia unafanyika ndani ya Kituo cha Hija cha Padre Pio eneo la neema, mahali pa kusikilizana, kutafakari na kusali. Ni kwa sababu hiyo, nawasihi kila mmoja wetu atenge muda wa kufanya tafakari binafsi. Tusali kwa ajili ya utume wetu, tusali kwa ajili ya kila mmoja wetu, tusali kwa ajili ya Taifa na uchaguzi mkuu ujao. Tafakari “Kwa nini mimi ni kiongozi katika WAWATA?” Ni wito wa kujichunguza ndani mwetu na kumwachia Roho Mtakatifu atufunde namna ya bora ya kuwatumikia wengine. Tunakutana wakati ambapo dunia inalia. Mabadiliko ya tabia nchi yanaleta madhara kwa familia zetu – ukame, mafuriko, magonjwa. Vita na migogoro vimeibua wimbi kubwa la wakimbizi na wanawake wanaoishi katika hofu na ukatili. Unyanyasaji wa kijinsia unaongezeka, na misingi ya malezi ya familia inaendelea kutikiswa. Katika yote haya, mwanamke anabeba mzigo mzito zaidi. Haya yatupe sababu ya kushikamana zaidi kama viongozi.  Ni wakati ambao makundi mengi ya wanaharakati yanapigania haki sawa. Ni kweli tunahitaji sauti ya mwanamke katika kanisa na taifa. Kama wanawake wakatoliki tuna swali la kujiuliza, Je, ni kweli tunataka usawa au tunataka ulimwengu ambao unaheshimu tofauti zetu kama wanawake na kutambua ukweli kuwa Mungu alituumba tofauti na wanaume ili kutumia utofauti huo kukamilishana – “complimentary for each other.” Ulimwengu ambao unawainua Wanawake kwa Kutambua Tofauti Zao za Kipekee, si kwa Kupigania usawa tu.

Mkutano mkuu ni muda wa sala, tafakari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari
Mkutano mkuu ni muda wa sala, tafakari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari

Bi Stefania Brancaccio, Katibu Mkuu wa UCID (Umoja wa Wakristo Wafanyabiashara na Viongozi wa Viwanda), amekuwa sauti muhimu katika kuhimiza uwezeshaji wa wanawake kwa kuenzi mchango wao wa kipekee badala ya kulenga tu usawa wa kijinsia kwa mtazamo wa kawaida ambao hautabadili uhalisia wa kuwa mwanamke katu hatakuwa sawa na mwanaume – ka mfano, mwanaume hawezi kubeba mimba, hatapewa likizo ya uzazi ya miezi mitatu kunyonyesha n.k. Katika makala yake yenye kichwa “Sisi wanawake viongozi, dhidi ya ubaguzi na kutokuwepo kwa usawa kazini,” Brancaccio alisisitiza kuwa uongozi haupaswi kufungiwa katika mipaka ya jinsia. Anaeleza kuwa kuna umuhimu wa kuleta mizani ya nguvu za kike na kiume katika nafasi za uongozi, na kwamba wanawake – hasa wale wanaorejea kazini baada ya likizo ya uzazi – mara nyingi huonyesha uwezo mkubwa zaidi wa kiuongozi.

WAWATA: Jengeni utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana: Kanisa la Kisinodi
WAWATA: Jengeni utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana: Kanisa la Kisinodi

Ni kwa Muktadha huu tunahitaji mikutano kama huu – ya kutiana moyo, kusikilizana, kupongezana, na kuwa pamoja kwa upendo. Tusiogope kusema ukweli kwa upendo, na tusiwe wepesi wa kuhukumu bali wa kuelewa. Tukumbuke: tunatoka sehemu tofauti, lakini tunaunganishwa na Roho mmoja – Roho Mtakatifu, anayefanya yote kuwa mapya. Pili: Kwa neema ya pekee, tunatarajia kukutana na kuzungumza na Maaskofu wote – tarehe 17 Juni, mchana. Hii ni nafasi ya baraka na ya kipekee. Tukaiandee kwa sala, tukija tukiwa na mioyo iliyo tayari kusikiliza na kushirikiana kwa namna mpya na ya kina. Kwa hayo machache, narudia tena kuwasihi kuuendea mkutano wetu kwa upendo, uwazi, kuchukuliana, kutiana moyo, na kupongezana. Tusafishe nia zetu, tuombee mwelekeo wa WAWATA kwa miaka ijayo, na tuombe ili kila mmoja wetu awe chombo cha amani, haki, na matumaini katika familia, Kanisa, na taifa. Maisha yetu yaakisi maneno. Mtakatifu Inyasi wa Loyola “Tufanye kazi kana kwamba, kila kitu kinatutegemea sisi, lakini tumtegemee Mungu kikamiloifu, kwa sababu kila kitu kina mtegemea Yeye.”

Wajumbe wa WAWATA: Ni wakati wa kusema ukweli katika upendo
Wajumbe wa WAWATA: Ni wakati wa kusema ukweli katika upendo

Sala: “Pokea, Bwana, hiari yangu yote. Pokea kumbukumbu, akili na utashi wote. Vyovyote nilivyonavyo au kuvimiliki nimejaliwa na wewe: nakurudishia vyote na kuukabidhi utashi wako uvitawale. Unijalie tu upendo wako na neema yako, nami nitakuwa tajiri vya kutosha, nisitamani kitu kingine chochote.” Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa.

WAWATA 2025
16 Juni 2025, 14:03