ĐÓMAPµĽş˝

Mintarafu mauaji, utekaji na kupotea kwa baadhi ya watu nchini Tanzania katika mazingira ya kutatanisha, Askofu Msonganzila amesisitiza uchunguzi wa kina ili kurejesha amani na utulivu kwani si haki kunyamaza.  Mintarafu mauaji, utekaji na kupotea kwa baadhi ya watu nchini Tanzania katika mazingira ya kutatanisha, Askofu Msonganzila amesisitiza uchunguzi wa kina ili kurejesha amani na utulivu kwani si haki kunyamaza.   (© TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Askofu Msonganzila: Waamini Tangazeni na Kushuhudia Ukweli na Amani

Askofu Msonganzila, amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutumia ndimi zao kusema na kutangaza ukweli juu ya vitendo viovu vinavyotokea katika jamii hasa vyenye viashiria vya uvunjivu wa amani bila kuogopa chochote. Mintarafu mauaji, utekaji na kupotea kwa watu nchini Tanzania katika mazingira ya kutatanisha, Askofu Msonganzila amesisitiza uchunguzi wa kina ili kurejesha amani na utulivu kwani si haki kunyamaza. Ukweli usemwe!

Na Sarah Pelaji, - Vatican.

Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma nchini Tanzania, ameelezea Sherehe ya Pentekoste kuwa ni siku ya hamsini, hitimisho la Sherehe ya Pasaka ya Bwana, Roho Mtakatifu anawashukia Mitume na hivyo kushirikishwa kama Nafsi ya Mungu; kutoka katika utimilifu wake Kristo Yesu, Bwana anammimina Roho kwa wingi. Hii ni siku ambayo Fumbo la Utatu Mtakatifu linafunuliwa kwa ukamilifu. Toka siku hiyo, ufalme uliotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu uko wazi kwa ajili ya wale wanaomwamini na kumsadiki, katika hali ya unyenyekevu na imani wanashiriki ushirika wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni paji la Mungu na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu waamini wanaweza kuzaa matunda ya Roho Mtakatifu ambayo: ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Pentekoste ni mwanzo wa Kanisa. Rej. KKK 731-747. Kwa kushukiwa na Roho Mtakatifu, Mitume wakapata ujasiri wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; akawaimarishia umoja na ushirika, kiasi kwamba, Mitume wakaanza kuzungumza kwa lugha mbalimbali, matendo makuu ya Mungu yaliyowawezesha kuungama imani moja. Roho Mtakatifu aliwajalia Mitume kuzungumza ukweli ambao ni Mungu mwenyewe.

Watanzania dumisheni haki, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa
Watanzania dumisheni haki, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa   (AFP or licensors)

Katika Ulimwengu mamboleo, waamini ambao ni wakristo waliobatizwa na kumpokea Roho Mtakatifu wanaowajibu wa kutangaza na kushuhudia kweli ya Mungu na kuiishi katika mazingira yao. Akirejea kwa yale ambayo yanaendelea nchini Tanzania na kulitia taifa la Tanzania doa la kuendelea kuitwa kisiwa cha amani ni lazima kusimamia ukweli ili Mungu aweze kuliponya taifa la Tanzania. Askofu Msonganzila, amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutumia ndimi zao kusema na kutangaza ukweli juu ya vitendo viovu vinavyotokea katika jamii hasa vyenye viashiria vya uvunjivu wa amani bila kuogopa chochote. Mintarafu mauaji, utekaji na kupotea kwa baadhi ya watu nchini Tanzania katika mazingira ya kutatanisha, Askofu Msonganzila amesisitiza uchunguzi wa kina ili kurejesha amani na utulivu kwani si haki kunyamaza.  “Kama mauaji yanatendeka na ni kweli watu wamepoteza waume, watoto na ndugu zao, lazima kuweka wazi kuwa yanatendeka; kisha tutafute wanaoyatekeleza na kuwapeleka kwenye mikono ya sheria, ili sheria iweze kushika mkondo wake.  Kwanini tunakuwa na kigugumizi kukiri kuwa mauaji yanatendeka? Anayethubutu kusimama kuzungumza ili yasiendelee kutendeka kwanini anashutumiwa kama amefanya jambo baya?” amehoji Askofu Msonganzila.

Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano
Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano   (© TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

 Amewataka waamini na wote wenye mapenzi mema kuishi Ujumbe wa Pasaka ambao ni amani akisisitiza kuwa amani pia haiwezi kupatikana bila haki. Aidha amehoji kwanini mauaji hayo yanatokea mara kwa mara huku akirejea mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ambayo wauaji walipatikana kwa urahisi. sana kwanini hawa hawapatikani.” Walimu waliofanya fujo na kudanganya, wahujumu uchumi walipatikana wengi tu wakati wa Sokoine sasa leo hawa wasipatikane kwanini? Roho Mtakatifu anataka tuwe wakweli na tusiogope kusema ukweli,” amesisitiza. Amesema Kanisa la Kipentekoste ni la waamini ambapo wanatumwa na Kanisa kwenda kusimamia ukweli bila woga. Kwamba Roho Mtakatifu amewajaza ndimi za moto za kutangaza Kweli ya Mungu na kutenda haki, hivyo washirikiane na jamii kusema ukweli endapo wanafahamu wauaji hao ili washitakiwe kwenye vyombo vya sheria. “Bebeni ukweli, msamaha, upendo, chukieni dhambi kuweni watu wa huru kwa Kristo ambao wako tayari kuumia kwa ajili ya haki, ukweli, amani na upendo,” alisema.

Waamini wajisadake katika haki, ukweli, amani na upendo
Waamini wajisadake katika haki, ukweli, amani na upendo   (© TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Akizungumzia kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Mwezi Oktoba 2025 Askofu Msonganzila aliwasisitoza watanzania kukataa rushwa ili wawe huru kuchagua kiongozi anayewafaa.  “Hizi fedha za kuhonga zitawapeleka motoni kadhalika na wewe unayekubali kuhongwa fedha hiyo pia itakupeleka motoni. Kataeni rushwa kwani ni dhambi,” alisisitiza askofu Msonganzila. Amesema kwa sasa zipo siasa za kujipendekeza ambazo zinaleta udhaifu katika kupata viongozi imara watakaojizatitit katika kulijenga taifa. Askofu Msonganzila amewataka waamini walei kutumia ndimi zao kusema ukweli juu ya vitendo vyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani kwani ukweli siku zote unamuweka mtu huru na mkristo aliyebatizwa anatumwa kutangaza injili ili ya haki na kweli ili kurejesha matumaini kwa wale waliopoteza matumaini.

Askofu Msonganzila amezindua Kikanisa cha Ibada Kwa Moyo Mt. wa Yesu
Askofu Msonganzila amezindua Kikanisa cha Ibada Kwa Moyo Mt. wa Yesu   (© TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Msimamizi wa Kituo cha Hija Kitaifa cha Huruma ya Mungu, Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma, Padri Wojciech Adam, na Paroko wa Parokia ya Kiabakari amesema umefika wakati kwa Wakristo na watu wenye mapenzi mema nchini Tanzania kushikama kwa kusali na kummwomba Mwenyezi Mungu aepushe matendo maovu yanayotendeka ndani ya jamii kwani wanaotendewa ni binadamu wenzetu  Paroko huyo amemshukuru Askofu Michael Msonganzila kwa kufika katika Parokia hiyo na kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa waamini zaidi ya 270, sanjari na kuzindua rasmi Kikanisa cha Ibada cha Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu pamoja na kupanda mti maalum kwa ajili ya kumbukumbu ya Papa Leo XIV. Viongozi wa Halmashauri ya Walei wa Parokia hiyo wamemshukuru Askofu Msonganzila kwa kukubali ombi lao la kuwapatia waamini wao sakramenti hiyo na kufanya shughuli mbalimbali za kiroho na kimwili katika Parokia hiyo hali ambayo imeonyesha upendo mkubwa kwao.

Askofu Msonganzila Pentekoste
12 Juni 2025, 15:45