Watanzania Tafuteni Mlango wa Matumaini Ili Muonje Huruma na Upendo wa Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia, JWWI, inaundwa na watumishi wa Mungu zaidi ya 300 wakiwemo Mapadre, Mashemasi, Watawa na Mafrateri ambao wanasoma katika vyuo mbalimbali na wanatoa huduma ya maisha ya kiroho nchini Italia. Kama sehemu ya utaratibu wa maisha yao, Jumamosi tarehe 15 Februari 2025 wamekutana na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya Bikira Maria wa Salette, kwa heshima ya Bikira Maria Malkia wa Mitume. Ibada hii imeongozwa na Padre William Bahitwa kutoka Jimbo Katoliki la Musoma, ambaye amemaliza muda wa masomo yake na hivyo kupewa Shahada ya Uzamivu katika Taalimungu ya Maandiko Matakatifu kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kilichoko Roma. Katika mahubiri yake, Padre William Bahitwa aliwakumbusha watu wa Mungu kutoka Tanzania kwamba, Mji wa Roma umebahatika kuwa na milango mingi: Kuna mlango wa furaha tangu Januari hadi Desemba; Mlango wa Sala na Tafakari ya Neno la Mungu; Kuna Mlango wa mateso na mahangaiko; kuna mlango wa watu waliotopea katika dhambi na kukengeuka; watu ambao wako mbali na neema pamoja na uwepo wa Mungu katika maisha yao. Kumbe, mkutano wa watanzania ni muda muafaka wa kushirikishana changamoto, fursa, matatizo, magumu ya maisha na matumaini. Watanzania wajitambue kwamba, wameingia mjini Roma kwa kutumia mlango gani? Kuna mlango wa malalamiko, uonevu, nyanyaso na ubaguzi, kiasi cha mtu kukata tamaa ya maisha.
Padre Bahitwa amewataka watanzania kuingia mjini Roma kwa mlango wa matumaini, ili kuweza kukabiliana na magumu, changamoto na fursa mbalimbali zinazoendelea kujitokeza mbele ya macho yao, daima wakiwa tayari kupiga moyo konde na kusonga mbele, huku wakitambua na kuambata neema ya Mungu katika maisha yao, ili hatimaye, siku moja waweze kukamilisha masomo na utume wao. Wamwombe Mwenyezi Mungu awakirimie uwezo wa kupitia mlango wa matumaini, kwa kujitambua jinsi walivyo na hali yao ya maisha. Hii iwe ni fursa ya kujitafakari na hivyo mtu kuangalia hali yake halisi ilivyo katika maisha. Pale ambapo wameteleza na kuanguka waombe neema na baraka za kusimama tena kwa toba na wongofu wa ndani tayari kumrudia Mungu. Watanzania wajitahidi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa ajili ya wao wenyewe pamoja na jirani wanaowazunguka, ili wote kwa pamoja waweze kuona uwepo wa Mungu na neema yake; wema, huruma na upendo wa Mungu kwa watu wote.
Padre William Bahitwa alichota tafakari yake kutoka katika Liturujia ya Neno la Mungu, kutoka katika Kitabu cha Mwanzo 3:9-24 na Injili kama ilivyoandikwa na Marko 8: 1-10. BWANA Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Katika nafasi ya kwanza, swali hili anaulizwa mtu aliyepotea, mtu ambaye yuko katika eneo lisilojulikana. Adamu baada ya anguko lake alitoka eneo la uwepo wa Mungu, akaenda nje, mbali na neema ya Mungu. Mwenyezi Mungu ndiye aliyekuwa wa kwanza kutaka kuanzisha tena mahusiano na mafungamano na Adamu aliyekuwa amepotea kutoka katika eneo la neema, akataka kurejesha tena mahusiano haya. Mungu ndiye anayechukua nafasi ya kwanza. Pili swali hili si kutaka kujua eneo ambalo Adamu alikuwa amejificha, bali ni kutaka kufahamu hali yake baada ya anguko lake, licha ya tahadhari na maonyo aliyopewa na Mungu! Swali la uko wapi ni kutaka kumkumbusha Adamu kwamba, umepata nini kwa kutokuamini na kutii kwake; kwa kushindwa kujiaminisha mbele ya Mungu. Mwenyezi Mungu alitaka kufahamu hali yake kwa kutema uwemo wa Mungu na kuchagua kudadisi. Mwenyezi Mungu alimpatia nafasi ya kutubu, lakini akashindwa kuitumia vyema na matokeo yake akajificha kwa kuwatuhumu Hawa na Nyoka. Lengo kuu la swali hili lilikuwa ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, lakini Adamu alikuwa na shingo ngumu, wala hakutambua kile alichotenda.
Padre William Bahitwa amewakumbusha watanzania wanaoishi ughaibuni “kwenye magorofa ya wazungu”, wapende kujikita katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu utakaowasaidia wito na utume wao na kamwe wasimezwe na kishawishi cha kukaa mbali, bali wajitahidi kuishi katika uwepo na neema ya Mungu, daima wakijitahidi kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini. Mungu ni mwema kwa kila mtu ndiyo maana katika Injili, Kristo Yesu anasema “Nawahurumia mkutano kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala hawana kitu cha kula.” Mk 8:2. Watanzania wamesali kwa ajili ya kuwaombea viongozi wa Kanisa na kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu Francisko ambaye tangu tarehe 14 Februari 2025 amelazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, mjini Roma. Waamini waimarishwe ili hatimaye wawe ni mashuhuda na vyombo vya matumaini. Mwenyezi Mungu apende kuwaimarisha katika masomo na utume wao. Wameombea pia miito mbalimbali, ili Mwenyezi Mungu apende kulijalia Kanisa lake, watumishi waamini, watakatifu na wachapa kazi katika shamba lake. Mwenye Mungu awe ni faraja na matumaini kwa watu walioko kwenye nchi zenye vita, athari za mabadiliko ya tabianchi, wagonjwa, wakimbizi na wahamiaji. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, apende kuwakirimia maisha na uzima wa milele marehemu wote. NB. Licha ya mkutano huu kufana sana, lakini jambo moja, limewaacha watanzania wengi wakiondoka na majonzi, kwa kukosa “vitumbua.”