MAP

Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake na mwongozo wa maisha adili na matakatifu.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Sita ya Mwaka C wa Kanisa: Heri za Malimani

Tafakari Dominika ya Sita ya Mwaka C wa Kanisa: Heri Nane za Mlimani au Hotuba ya Malimani ni: Muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Hii ni Katiba ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Mama Kanisa anawakumbusha watoto wake kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani ufunuo wa Kristo Yesu.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Utangulizi: Mpendwa msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 6 ya Mwaka C wa Kanisa. Karibuni tumshukuru Mungu kwa yote aliyotujalia katika juma lililopita. Tunapomtukuza Mungu aliye Muumba wa vitu vyote, tumwombe atujalie baraka zake zitakazotusaidia kutekeleza mapenzi yake katika juma linalokuja. Tumkabidhi shida zetu Yeye ambaye tunajua kwamba anatupenda na yupo tayari kutujalia yale tunayomwomba. Basi nawaalikeni tutafakari pamoja juu ya dhamira hii: Amebarikiwa mtu yule anayemtumainia Bwana. Heri Nane za Mlimani au Hotuba ya Mlimani ni: Muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Hii ni Katiba ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Mama Kanisa anawakumbusha watoto wake kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani ufunuo wa Kristo Yesu. Kristo Yesu ni Bwana wa historia na viumbe vyote na hatima ya yote haya ni ufalme wa Kristo aliyedhalilishwa kwa kukamatwa, kuteswa na hatimaye kufa Msalabani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Heri za Mlimani ni dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo yanayopaswa kusimikwa katika utakatifu na uadilifu. Rej. Mt 5:1-12. Kristo Yesu anawaonesha wafuasi wake Heri za Mlimani kama: hekima na njia salama wanayopaswa kuifuata kama dira ya uongozi. Upole, unyenyekevu na huruma, mambo msingi yanayomwezesha kiongozi kuwa mkweli, mnyenyekevu na mtu wa haki. Viongozi wanapaswa kuondokana na unafiki pamoja na hali ya kujikweza, ili kuona boriti machoni pao, tayari kuwasaidia jirani zao kuondoa vibanzi vilivyomo machoni pao!

Heri za Mlimani ni dira, mwongozo na muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu
Heri za Mlimani ni dira, mwongozo na muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu   (Vatican Media)

Ufafanuzi: Katika somo la Injili tulilolisikia hivi punde, tunamsikia Yesu akionesha kutambua thamani ya mtu aliye maskini kwa kusema: Heri ninyi mlio maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu.  Sasa maskini ni nani? Au umaskini ni nini?  Maskini ni mtu asiyekuwa na pato la kutosha; ni mtu fukara, mtu asiye na mali. Mtu ‘maskini’ kadiri ya Biblia ni mtu ambaye ni mnyenyekevu na mtu asiye na msaada wowote zaidi ya msaada kutoka kwa Mungu. Matumaini yake yote ameyaweka kwa Mungu. Ni mtu yule ambaye anajiona kuwa kwa nguvu zake mwenyewe  bila msaada kutoka kwa Mungu, hawezi kufanya lolote. Katika kila aina ya uhitaji, katika kila shida yeye anamwendea Mungu kuomba msaada; huyo ni mtu maskini. Hivyo umaskini anaousifia Yesu ni ile hali ya mtu kujitambua kuwa yeye ni kiumbe dhaifu na anabaki katika kumtumainia Mungu katika kila kitu; ni mtu ambaye moyo wake haushikamani na mali za kidunia, ni mtu ambaye moyo wake ameufungua, ameuweka wazi mbele ya mpango wa Mungu wa ukombozi. Ndugu zangu, umaskini wa kutokuwa na mali au chochote kitakacho msaidia mtu kuendesha maisha yake, ni kitu kibaya. Umaskini si jambo zuri na si jambo la kujivunia. Ni umaskini ambao lazima tuupige vita. Ndio maana wenzetu Waisraeli waliona umaskini ni mapato ya dhambi: ziwe ni dhambi za mtu husika, dhambi za viongozi, au dhambi za jamii nzima. Umaskini wa kutokuwa na fedha au mali sio kigezo cha mmoja kuingia mbinguni. Maana unaweza ukawa maskini na bado ukawa na moyo mgumu katika kuitegemeza jamii yako au kanisa lako hata kwa mawazo mazuri; pia unaweza ukawa tajiri na bado ukawa na moyo wa ukarimu.

Heri za Mlimani ni Mwongozo wa maisha
Heri za Mlimani ni Mwongozo wa maisha   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Katika mwendo wa kawaida wa maisha yetu tunavipimo tulivyojiwekea ambavyo pengine vinatusaidia kupanga mambo, vitu na hata watu. Kwa mfano mtu akiwa na mali nyingi tunamwona kama ni mtu aliyependelewa na Mungu. Au tunapoona tunaandamwa na umaskini na maradhi tunaona kuwa tumelaaniwa na Mungu. Umaskini au utajiri mbele ya Mungu si lolote; jambo la msingi ni hili: katika hali yako ya umaskini, au katika hali yako ya utajiri, Mungu ana nafasi gani katika maisha yako. Je, lengo kubwa la maisha yetu tumeliweka katika mali, fedha, starehe, biashara, kazi, siasa au kitu chochote kinachopingana na Mungu? Vyote hivyo na yote tufanyayo hapa duniani viwe kwetu kama  daraja la kutupeleka kwenye ufalme wa Mungu. Tuishi maisha ya kusaidiana huku tukimtumainia Mungu. Maskini anapata mastahili mbele ya Mungu kwa kumtumainia Mungu. Na tajiri naye anapata mastahili mbele ya Mungu kwa kumtumainia Mungu huku akiwasaidia maskini kwa mali zake. Sote ni lazima tubaki katika kumtumainia Mungu. Matumaini kwa Mungu yanahusisha uvumilivu. Tunapoona na kushawishika kwamba Mungu hajanipa kile ninachomwomba, pengine tunaona kumtumainia Yeye inakuwa ni vigumu. Tuepuke kufikiri kuwa Mungu ametuacha. Hatuna budi kuvumilia.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025: Mwaka wa Matumaini
Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025: Mwaka wa Matumaini   (Vatican Media)

Matumaini kwa Mungu yanahitaji ustahimilivu. Tunapopatwa na magumu tusikate tamaa. Mungu anatupatia kile ambacho kinatufaa sisi.Tukiamini katika ahadi zake, tumkabidhi Mungu mipango yetu ya kila siku kwa kuwa ili tupate ulinzi wake hatuna budi kuwa na Mungu katika mambo yote tufanyayo. Basi tuzidi kumtumainia Mungu katika mambo yote. Tujikabidhi katika ulinzi wake ili siku ya kiyama, siku tutakapotakiwa kutolea hesabu ya maisha yetu, Kristo atuambie heri ninyi mliobarikiwa na Baba yangu ingieni katika ufalme wake.Hivyo, tusali kwa imani ili Mungu atujalie neema na nguvu za kumtumainia Yeye katika maisha yetu. Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji katika matumaini.” Matumaini ya waamini yako katika Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu aliyezaliwa katika Familia Takatifu iliyopata baraka ya kuwa na Mungu yaani Emanueli kati yake.

Liturujia D6 ya Mwaka C
14 Februari 2025, 15:03