MAP

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Sita ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Katika maisha, Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza. Heri za Mlimani ni Dira na Mwongozo wa Utakatifu wa maisha. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Sita ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Katika maisha, Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza. Heri za Mlimani ni Dira na Mwongozo wa Utakatifu wa maisha.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tafakari Dominika ya Sita Mwaka C wa Kanisa: Heri na Ole Katika Maisha

Liturujia ya Neno la Mungu inatufundisha kuwa, “furaha ya kweli inapatikana katika kuungana kabisa na Mungu” Nabii Yeremia anatupa faida za mtu yule aliyeungana kabisa na Mungu na kumfanya Mungu kuwa tegemeo lake, na hasara za mtu aliyemwacha Mungu na kutumaini mtu, mali au hata anasa za ulimwengu huu. Wanaomtumainia Mungu, wanaoishi kadiri ya sheria, Agano, amri na mapenzi ya Mungu, hao ndio wenye heri ndio watapata thawabu ya uzima wa milele.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., - Salzburgy, Austria

 Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya Sita ya Mwaka C wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika ya Sita ya Mwaka C wa Kanisa inatufundisha kuwa, “furaha ya kweli inapatikana katika kuungana kabisa na Mungu” Katika somo la kwanza, Nabii Yeremia anatupa faida za mtu yule aliyeungana kabisa na Mungu na kumfanya Mungu kuwa tegemeo lake, na hasara za mtu aliyemwacha Mungu na kutumaini mtu, vitu, mali au hata anasa za ulimwengu huu.  Wanaomtumainia Mungu, wanaoishi kadiri ya sheria, Agano, amri na mapenzi ya Mungu, hao ndio wenye heri (μακάριος, makarios), ndio watapata thawabu ya uzima wa milele na kinyume chake ndizo ole (οủαι, ouai) ambazo Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha katika somo la Injili Takatifu. Mtume Paulo katika somo la pili anamalizia kwa kutuasa kuwa, heri ya kweli, furaha ya kweli na ya kudumu inapatikana mbinguni. Bwana wetu Yesu Kristo kwa ufufuko wake anatuhakikishia njia ya kwenda mbinguni, ambapo tutapata furaha isiyo na mwisho kwa kuungana kwa daima na Mungu aliyetuumba na kutukomboa. Katika Dominika ya leo tumshukuru Mungu ambaye alituumba ili tumjue, tumpende, tumtumikie tukiwa hapa duniani ili mwisho turudi kwake mbinguni. Tumshukuru Mungu ambaye ametushirikisha neema zote za kimungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Tuombe neema ya kutambua nafasi ya Mungu katika maisha yetu, tuhangaikapo kutafuta mahitaji yetu ya hapa duniani yanayopita, tusisahau kumtafuta kwanza Mungu ambaye hatapita kamwe. Tuombe neema pia ya kuwashirikisha wengine neema na baraka tupokeazo bure kutoka kwa Mungu na mwisho tupewe thawabu ya kuishi milele na Kristo baada ya maisha yetu ya hapa duniani.

Heri za Mlimani ni dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu
Heri za Mlimani ni dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu   (Vatican Media)

Somo la Kwanza: Ni kitabu cha Nabii Yeremia 17:5-8. Somo la kwanza tulilolisikia, ni kutoka katika kitabu cha Nabii Yeremia. Mazingira ya somo hili (Setz im Leben), Nabii Yeremia alifanya kazi ya unabii katika nyakati za mwisho mwisho za wafalme wa Yuda (586 BC) yaani, Yosia, Yeoahazi, Yehoakim, Yehoakin na Zedekia. Ni muda mchache kabla ya taifa la Yuda kupelekwa utumwani Babeli. Katika kipindi hiki, taifa Yuda lilikua na mmomonyoko mkubwa sana wa maadili. Katika mambo ya kiroho, walimwacha Mungu wa kweli na kuabudu sanamu (idolatry), miungu ya watu wa mataifa, kisiasa walianza kufanya urafiki (political alliances) na watu wa mataifa mengine ili kujilinda na kujihakikishia usalama dhidi ya adui zao, wakitegemea taifa la Misri na taifa kubwa la Babeli kama ulinzi na tegemeo lao. Kijamii, kulikua na unyanyasaji mkubwa sana kwa maskini, dhuluma, na ukosefu wa haki (social injustices). Ni katika mazingira hayo, Nabii Yeremia anatumwa na Mungu kuwakemea na kuwakumbusha kuwa walipaswa kumtegemea Mungu peke yake. Nabii anawasisitiza juu ya hasara apatayo mtu yule amtegemeaye na kumfanya mwanadamu kuwa kinga yake, ilihali moyoni mwake amemwacha Mungu. Anasisitiza pia faida azipatazo yule amtegemeaye Mungu, ambaye amemfanya Bwana kuwa tumaini lake. Je, mimi na wewe tu katika kundi lipi? Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo matatu ya kujifunza.

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Sita ya Mwaka C wa Kanisa: Heri na Ole
Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Sita ya Mwaka C wa Kanisa: Heri na Ole   (Vatican Media)

Kwanza: Ulinzi, amani, furaha na usalama wa kweli haupo katika watu au mali (reliance of earthly mammon provides no true security). Taifa la Yuda walimwacha Mungu wa kweli, Mungu wa Israeli, aliyewatendea mambo makuu katika historia ya ukombozi wao, kisha wakaweka matumaini yao katika nguvu za kijeshi na ushirikiano kati yao na mataifa mengine. Hali kadhalika, walimwacha Bwana kwa kutenda mambo yaliyo kinyume na amri na maagizo yake. Hofu na mashaka ni kinyume cha Imani thabiti kwa Mungu. Hata hivyo, hawakufanikiwa kupata furaha, wala ulinzi na usalama wa kweli na matokeo yake wakaishia kupelekwa utumwani Babeli. Ndugu wapendwa, mara nyingi mafaniko yetu yanaweza kutufumba macho tukaona kana kwamba Mungu hana nafasi katika maisha yetu ya kila siku. Utajiri na mali vyaweza kutufanya tukakosa Imani kwamba usalama wetu, furaha yetu, amani yetu na utulivu wetu wa ndani unatokana na kuunganika kwetu kabisa na Mungu. Matokeo yake tunaingiwa na hofu juu ya mali zetu, juu ya familia zetu, juu ya biashara zetu, mipango na matarajio yetu. Tunapaswa kufahamu kuwa vitu vyote tulivyo navyo ni mali ya Mungu hata sisi wenyewe. Tukitambua hilo hatutakua na mashaka juu ya mali, wala chochote tulicho nacho katika ulimwengu huu. Pia tunapaswa kufahamu kuwa tukishikilia mambo yote mikononi mwetu tutayapoteza yote, ila tukiyaweka yote mikononi mwa Mungu, tutayamiliki yote na zaidi sana uzima wa milele baada ya maisha haya ya ulimwengu huu unaopita.

Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza katika maisha
Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza katika maisha   (Vatican Media)

Pili: Tunapomwacha Mungu, tunashindwa kuzaa matunda (spiritual barrenness results from misplaced trust). Nabii Yeremia anamfananisha mtu aliyemwacha Mungu na kichaka kilichopo jangwani palipo na ukame, katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Mwandishi ametumia neno “kichaka” (shrub/arōʿēr), mmea ambao hauna mizizi mirefu unaomea mara nyingi katika jangwa. Mmea  huu hauwezi kuzaa matunda yoyote kwa kuwa kwanza, mazingira yake hayaruhusu kuweza kuzaa matunda (chumvi na ukame) na pili kwa kuwa haupati virutubisho kutokana na kuwa na mizizi mifupi (life without spiritual nourishment). Ndugu wapendwa, mara kadhaa kwa sababu mbalimbali tunakua mbali na Mungu. Huenda changamoto zetu mbalimbali zikatufanya kuona kama Mungu hawezi kuwa msaada wetu na hivyo kuweka matumaini yetu kwa watu, hali au vitu. Hali kadhalika, shughuli zetu na majukumu mengi ya kila siku vyaweza pia kutufanya tukamsahau Mungu na kutegemea nguvu na uwezo wetu sisi wenyewe utokanao na vitu au watu (misplaced trust).

Heri na Furaha ya kweli inapatikana mbinguni
Heri na Furaha ya kweli inapatikana mbinguni   (Vatican Media)

Ndugu wapendwa, matokeo ya kuwa mbali na Mungu ni kutindikiwa kiroho, kuwa na ukame na upungufu mkubwa wa kinga rohoni mwetu. Tunapokosa kinga na virutubisho rohoni ni dhahiri kuwa hatuwezi kuzaa matunda mengi na mema. Hatuwezi kuona udhaifu ndani mwetu na kujibidiisha kujipatanisha na Mungu, hatuwezi kuona wema na uzuri wa Mungu wetu ndani ya nafsi za wenzetu. Tumwombe Mungu atusaidie kuwa na Imani thabiti kwake hata wakati wa magumu na changamoto nyingi. Tatu: Imani na tumaini kwa Mungu vitatufanya kustahimili katika hali zote na kuzaa matunda (faith and hope lead to resilience). Nabii Yeremia anamfananisha mtu anayemtegemea Mungu kama mti uliopandwa kando ya maji. Tofauti na kichaka kisichokuwa  na mizizi mirefu wala mazingira rafiki, mtu huyu atazaa matunda mengi, hataona hofu wakati magumu yatakapokuja, hatapungukiwa chochote kwa kuwa Imani na matumani yake vimejengeka kwa Mungu pekee. Ndugu zangu, Imani na matumaini yetu vyapaswa kujengeka katika Mungu peke yake. Tunapokuwa na Mungu tuna hakika kuwa tutakuwa daima salama mikononi mwake. Changamoto zitakapotujia tutakua na hakika kuwa ni za muda na za kupita kwa kuwa Mungu hawezi kutupa jaribu ambalo hatustahimili. Hata katika magumu tutastahimili tukijua hakika kuwa ni njia yetu ya kutufikisha kwenye heri na furaha ya kweli tutakayoipata kwa kuungana kabisa na Mungu baada ya maisha haya ya hapa duniani. Ndugu mpendwa, tunaunganika kabisa na Mungu kwa njia ya sala, kuabudu Ekaristi Takatifu, kusoma Neno la Mungu na kutenga muda binafsi kukaa na Yesu, kupokea Ekaristi Takatifu na kujipatanisha naye kila mara tunapotenda dhambi. Kwa njia hiyo, tutaweza kupata virutubisho msingi kwa ajili ya ustawi wa roho zetu, ambavyo kwavyo tutakua imara daima katika Imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na kwa Jirani zetu.

Injili inapaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wote wa Mataifa
Injili inapaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wote wa Mataifa   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Somo la Injili: Ni Injili ya Luka 6:17, 20-26. Somo la Injili Takatifu kutoka katika Injili ya Luka ni hotuba ya Bwana wetu Yesu Kristo akiwa Nyikani, sehemu tambarare, sawa na Hotuba ya mlimani kama ilivyoandikwa na mwinjili Mathayo katika sura ya 5-7. Kwa nini mwinjili Luka anatupa habari za Yesu akitoa hotuba katika nyika, mahali tambarare? Hii ni msisitizo wa Luka kwamba Yesu anapatikana kwa watu wote, ikizingatiwa kwamba Mwinjili Luka aliandika Injili hii kwa watu wa mataifa yote akisisitiza ukombozi uletwao na Kristo ni kwa watu wa mataifa yote (Univesality of salvation). Mwinjili Mathayo anamwonesha Yesu kama Musa mpya, akitoa sheria ua mwongozo kwa taifa la Mungu. Tukumbuke kuwa Mwinjili Mathayo aliandika Injili yake kwa Wayahudi. Somo hili latupa picha kuwa, wanaomtumainia Mungu, wanaoishi kadiri ya sheria, Agano, amri na mapenzi ya Mungu, hao ndio wenye heri (μακάριος, makarios), ndio watapata thawabu ya uzima wa milele na kinyume chake ndizo ole (οủαι, ouai) ambazo Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha katika somo la Injili Takatifu. Katika somo hili la Injili dominika ya leo tuna mafundisho manne ya kujifunza. Kwanza: Yesu ameshuka chini kabisa kwa ajili yetu sisi sote (accessibility and inclusivity). Mwinjili Luka anatupa habari kuwa, “Yesu alishuka pamoja nao, akasimama mahali pa tambarare, pamoja na wanafunzi wake wengi, na makutano makubwa ya watu waliotoka Uyahudi wote na Yerusalemu, na pwani ya Tiro na Sidoni waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao” (Lk 6:17). Ni wazi kuwa Yesu aliwapokea watu wote, alishuka chini na kukaa kabisa na watu ili kuwasaidia na kusimika ufalme wa Mungu kati yao. Ndio sababu yatajwa hapa maeneo yaliyokaliwa na wa wayahudi (Yerusalemu) hali kadhalika na watu wa mataifa (Tiro na Sidoni). Ndugu mpendwa, Bwana wetu Yesu Kristo amekuja kwa ajili yetu sisi sote. Ameshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi sote. Amekubali kukaa kati yetu, ameshiriki ubinadamu wetu ili atushirikishe umungu wake. Tuna furaha, tuna amani, tuna matumaini kwa kuwa Yesu hamwachi hata mmoja katika mpango wake wa ukombozi. Yesu amekuwa mwema kwa watu wote, wenye dhambi hali kadhali na watakatifu, Yesu anatupenda sote na anataka sote tuupate uzima wa milele.

Jengeni mahusiano mema na Yesu kwa: Kwa Sala, Neno, Ekaristi na Huduma
Jengeni mahusiano mema na Yesu kwa: Kwa Sala, Neno, Ekaristi na Huduma   (Vatican Media)

Pengine tunapitia katika changamoto nyingi maishani mwetu, huenda zinatukosesha amani na furaha ya kweli. Yesu amekuja kwako, ameshuka chini kabisa kwa ajili yako, kwa ajili ya familia yako, kwa ajili ya watoto wako, kwa ajili ya ndoa yako, kwa ajili ya kazi na biashara yako. Kuwa na tumaini kwamba hatakuacha kamwe, na kwamba upo katika mpango wa neema na baraka alizoahidi kwa ajili yako. Jipe moyo, upo mikono salama. Yupo kati yetu kila siku katika Neno lake, tunampokea katika Ekaristi Takatifu, yupo daima altareni katika Tabernaklo. Tumshirikishe Yesu changamoto zetu, atatupa nguvu na njia ya kuendelea kusonga mbele zaidi. Mtumaini Yesu, ni rafiki mwema. Amekuja kwa ajili yako. Pili: Yesu anatufundisha kutumia mali na utajiri wa dunia hii kwa ajili ya kujipatia ufalme wa Mbinguni (use of earthly resources for God’s kingdom).  Yesu anatoa heri nne katika Injili hii ya Luka, na zote zaonesha mtazamo wa kuwa maskini kwa ulimwengu huu kwa ajili ya kutajirisha kwa ulimwengu ujao. Kuwa maskini wa Roho ni kutambua nafasi ya Mungu katika maisha. Kutambua kuwa hatuna kitu bali vitu vyote vyatoka kwa Mungu, nasi tunapaswa kuvitumia kwa ajili ya Mungu na ufalme wake. Ndugu mpendwa, Yesu anatufundisha kuwa, utajiri wa kweli ni kutambua nafasi ya Mungu katika maisha yetu. Sio kwamba Yesu anatukataza kuwa matajiri katika ulimwengu huu, la hasha. Sio kwamba anatukataza kutafuta mali na mahitaji yetu ya dunia hii. Anatufundisha kuwa, tunapaswa kutambua kuwa Mungu ana nafasi ya kwanza katika maisha yetu, na kwamba kila alichotupa tunapaswa kukitumia kwa busara kwa ajili ya kuwasaidia wengine. Kati yetu wapo wengi wenye uwezo, wapo pia ambao hawana uwezo, ni maskini, wagonjwa, wazee, wajane, watoto wa mitaani nk. Tunapowatazama hao kwa jicho la huruma na upendo, tunamtazama Yesu mwenyewe. Tunapowasaidia maskini na wenye shida, tunamsaidia Yesu mwenyewe na mwisho atatuambia, njooni mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa kwa ulimwengu (Mt 25:34).

Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha
Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha   (Vatican Media)

Tatu: Furaha ya kweli dhidi ya faraja ya kidunia (true joy vs. worldly comfort).  Yesu anatuonya juu ya kutafuta furaha katika mambo ya dunia hii ambayo ni ya kupita tu. Furaha ya kweli kumbe ipo katika kumtafuta Mungu, kuishi na Mungu na kufa katika Mungu. Tunapotafuta furaha ya kweli kwa Mungu, hatutaumizwa na mateso na msumbuko, wala madhulumu ya dunia hii kwa kuwa tunajua furaha yetu ni katika Mungu peke yake. Ndugu mpendwa, kila mmoja ajiulize leo hii kwamba ni wapi roho yangu inapata furaha ya kweli? Ni wapi roho yangu inapata amani ya kweli? Je, ni katika mahangaiko ya kutafuta mali na fedha, vyeo na mamlaka, heshima na utukufu katika maisha haya yapitayo? Huenda nyakati fulani biashara zinanibana mpaka nakosa nafasi ya kwenda kuhudhuria misa takatifu, au jumuiya ndogondogo pamoja na wenzangu, au sala za pamoja katika familia, au muda wangu binafsi pamoja na Yesu. Tukumbuke kuwa anasa, mali, utajiri wa dunia hii vitapita lakini Yesu na ufalme wake hautapita kamwe. Tumwombe Mungu atukumbushe wajibu wetu wa kumtafuta Yesu na kuitafuta furaha ya kweli ipatikanayo katika kuunganika naye. Nne: Yesu anatufundisha kusimama imara katika Imani yetu (standing firm in faith). Yesu anawafundisha Mitume wake kwamba, kuwa mfuasi wake kweli sio kazi rahisi. Katika somo la kwanza Nabii Yeremia alimfananisha mtu amtegemeaye Mungu kama mti uliopandwa karibu na mto, kwamba hautaona hofu wakati wa hari ujapo, yaani aliye na Mungu ana ujasiri wa kuvumilia yajapo magumu na shida. Ndugu mpendwa, kuwa mfuasi wa Kristo sio kazi rahisi. Kuna nyakati tutakutana na magumu, tutakatishwa tamaa, tutakataliwa na kurudishwa nyuma, tutajiuliza maswali mengi sana juu ya Imani yetu. Yesu anatufundisha kuwa, tukubalipo kuteseka kwa ajili ya Kristo hatuwezi kupotea kamwe, kwa kuwa thawabu yetu ipo mbinguni. Ndugu mpendwa, hata ije changamoto gani, usimwache Mungu. Ije njaa, yaje magonjwa, uje ufukara, yaje manyanyaso, ukatishwe tamaa, urudishwe nyuma, ukataliwe na watu, upate hasara na mitihani katika maisha, kamwe usimwache Mungu. Mtumanie Mungu. Weka yote mikononi mwa Mungu, utayamiliki yote. Mtume Paulo anatuambia hakuna kitu chochote kitachoweka kututenga na upendo ulio ndani ya Kristo Yesu (Rum 8:35-39).

Kristo Yesu ni chemchemi ya imani na nuru ya Mataifa
Kristo Yesu ni chemchemi ya imani na nuru ya Mataifa   (Vatican Media)

Somo la pili: Ni Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo 1 Kor 15:12, 16-20. Katika somo la pili, Mtume Paulo anatukumbusha msingi wa Imani yetu ni katika fumbo la mateso kifo na ufufuko wa Kristo yaani fumbo la pasaka. Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi, akazikwa na akafufuka kadiri ya maandiko. Tukitambua kuwa huo ndio msingi wa Imani yetu, tutatambua hakika kuwa furaha ya kweli na ya kudumu inapatikana katika kuungana kabisa na Kristo. Bwana wetu Yesu Kristo kwa ufufuko wake anatuhakikishia njia ya kwenda mbinguni, ambapo tutapata furaha isiyo na mwisho kwa kuungana na Mungu aliyetuumba na kutukomboa. Hitimisho: Katika Dominika ya leo tumshukuru Mungu ambaye alituumba ili tumjue, tumpende, tumtumikie tukiwa hapa duniani ili mwisho turudi kwake mbinguni. Tumshukuru Mungu ambaye ametushirikisha neema zote za kimungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Tuombe neema ya kutambua nafasi ya Mungu katika maisha yetu, tuhangaikapo kutafuta mahitaji yetu ya hapa duniani yanayaopita, tusisahau kumtafuta kwanza Mungu ambaye hatapita kamwe. Tuombe neema pia ya kuwashirikisha wengine neema na baraka tupokeazo bure kutoka kwa Mungu na mwishowe, tupewe thawabu ya kuishi milele na Kristo baada ya maisha yetu ya hapa duniani.

Tafakari D6 Mwaka C wa Kanisa
14 Februari 2025, 15:32