ĐÓMAPµĽş˝

2025.02.07 Dominika ya V ya Kipindi cha kawaida cha Mwaka V.Muujiza wa samaki. 2025.02.07 Dominika ya V ya Kipindi cha kawaida cha Mwaka V.Muujiza wa samaki. 

Ondoka kwangu kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi,Bwana!

Katika Dominika ya 5 ya Mwaka C,masomo yanaunganishwa na wazo la utakatifu wa Mungu dhidi ya dhambi zetu sisi wanadamu.Kwa njia hiyo tuombe Roho Mtakatifu atujalie fadhila ya unyenyekevu ili tuweze kufaidi tunda la kumwona Mungu hapo baadaye na tunda la amani katika jumuiya zetu.

Na Padre Joseph Herman Luwela - Vatican.

Karibu mpendwa msomaji na msikilizaji, leo ni Dominika ya tano ya Mwaka C. Katika Dominika ya leo, masomo yanaunganishwa na wazo la utakatifu wa Mungu dhidi ya dhambi za sisi wanadamu. Kwa maneno mengine, ili tuweze kumsogelea Mungu hatuna budi kwanza kujitakasa wenyewe. Wazo hili lipo wazi katika somo la kwanza na somo la Injili linaligusa kwa maneno ya Mtume Petro,

“Ondoka kwangu kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi, Bwana”

Basi pamoja tuungane na Mtume Petro katika maneno na unyenyekevu huo yawe mwongozo wa tafakari ya neno la Mungu

Ufafanuzi

Tumesikia katika somo la Injili kuwa Yesu alikuwa kando ya ziwa Genezareti, (Ziwa hili pia linajulikana kama ziwa Galilaya au pia ziwa Tiberia) akiwa amezungukwa na umati wa watu walio kuwa wanataka kusikiliza mahubiri yake. Akiwa pale, akaona mitumbwi miwili ipo pembeni ya ziwa na wenye mitumbwi hiyo wapo mbali nayo wakiosha nyavu zao baada ya mzunguko wa usiku mzima wa kuvua bila kupata chochote. Wamiliki wa ile mitumbwi walikuwa Simon Petro, Yakobo na Yohane. Yesu akaingia kwenye mtumbwi wa Petro na kumwomba auingize ndani kidogo ya maji ili ajitenge kidogo na wale watu apate kuwahubiria vizuri. Petro akakubali kuupeleka ule mtumbwi ndani zaidi ili Yesu atumie kama jukwaa la kuhubiria. Injili haisemi kuwa baada ya Petro kumwendesha Yesu hadi ndani  zaidi ya maji yeye alirudi nchi kavu au walibaki wote mle; ila inasema tu kuwa alipomaliza kuhubiri akamwambia Petro upeleke mtumbwi hadi kilindini mkashushe nyavu zenu mkavue. Bila shaka walikuwa wote mle chomboni.

Maneno ya Yesu yalimshangaza sana Petro kadiri ya uzoefu wake wa uvuvi wa tangu ujanani hadi katika uzee ule. Anashangaa kwa sababu anafahamu masherti ya uvuvi kuwa inawezekana wakati wa usiku na si mchana kama ule - ingekuwa kupoteza muda kama usiku wenyewe tu hawakupata kitu. Kule uyahudini kulikuwa na namna mbili za uvuvi:

-Namna ya kwanza ni ile ya kutega nyavu jioni na kisha kuja siku ya pili kuangalia kama samaki wamenasa. Kazi ya kuangalia kama samaki wamenasa iliweza kufanyika hata mchana.

-Namna ya pili ya kuvua ndiyo iliyokuwa ya kuzunguka na nyavu usiku kucha kuwawinda samaki kwa kukokota nyavu. Namna hii ilikuwa na uhakika zaidi kuliko ile ya kutega lakini mara nyingi ukikosa utakuta umekusanya takataka tu katika nyavu yako ndiyo maana hapa, katika Injili inasemwa kuwa hawa mitume walikuwa wakiosha nyavu zao yaani baada ya kukusanya tu takataka badala ya samaki. Na, namna hii ya uvuvi ndiyo pia waliyoitumia hawa akina Petro, Yohane na Yakobo siku ile.

Baada ya kuambiwa kuwa watweke hadi kilindini wakatupe nyavu kuvua samaki, Petro anamwambia Yesu kuwa, walikuwa wameifanya kazi hiyo usiku kucha bila kuambulia chochote. Hata hivyo kwa neno lake, watatupa nyavu. (Petro alimfahamu Yesu kuwa alikuwa mtu wa miujiza kwani alishawahi kutanguzana naye tangu siku ile walipokutana mtoni Yordani na kumpa jina Petro (Yoh 1:42). Lakini tangu hapo walipoonana kwa mara ya kwanza, Petro alikwenda tena nyumbani kufanya kazi zake za uvuvi hadi baada ya mwaka mmoja ndiyo siku ya tukio tulilolisikia katika Injili ya leo). Baada ya kutupa nyavu ziwani, walipozikusanya, zilikuwa zimejaa samaki ambao hata waliwashinda nguvu na nyavu zao kuanza kukatika; wakaomba msaada kwa rafiki zao waliokuwa jirani nao. Mitumbwi yote miwili ilifura samaki na ikataka kuzama. Petro, akiwa ameshikwa na butwaa akasema,

“Ondoka kwangu kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi, Bwana”

Katika maisha: Ndugu zangu katika Kristo, maneno haya ya Petro, yana ujumbe mzito kwetu sisi.  Yanavyoonekana ni kama vile ya kuweweseka, lakini, ni maneno mazito.  Ni maneno mazito kwa sababu yamejaa unyenyekevu unaojionesha katika kukiri ukosefu wake anapoungama kuwa alikuwa mkosefu. Narudia. Maneno haya ni mazito kwa sababu yanaonesha moyo wa unyenyekevu wa hali ya juu aliokuwa nao Petro hata akakiri kuwa ni mkosefu. 

Ndugu zangu katika Kristo, kama sisi tungejenga fadhila hii ya unyenyekevu kwa kukiri; kwa kuungama makosa yetu kwa Mungu na wenzetu, tungekuwa na uhakika wa mambo mawili, yote yakiwa ni matunda ya unyenyekevu wa kukiri makosa yetu: Mosi, kufika mbinguni. Hili ni tunda la kiroho. Baada ya maisha haya ya hapa duniani, mbingu ingekuwa halali yetu. Kwa sababu gani? Tunapoungama/ kukiri makosa yetu kwa Mungu, tunaonesha unyenyekevu wetu mbele yake, na unyenyekevu, Yesu alituambia kuwa ni kigezo cha kufika mbinguni aliposema,

“Msipokuwa kama watoto wadogo, hamwezi kuingia katika ufalme wa mbinguni”       (Mt 18:3; Lk 18:17)

Hii ndiyo sababu, tunapotaka kujisafisha mbele ya Mungu kwa sakramenti ya kitubio, hatuishii tu  na kujuta dhambi bali na kuungama dhambi kabla ya kutimiza malipizi. Wapo watu wanaofundisha kuwa majuto yanatosha kumpatanisha mtu na Mungu, si kweli. Majuto si mapato ya unyenyekevu bali ni mapato ya kutambua kosa ambalo mmoja amelifanya; hata shetani anaweza kujutia pale inapotokea kuwa amefanya uzembe katika kazi yake mbaya ya kumpotosha binadamu; huwa inamuuma sana na anajilaumu. Shetani anapoumia si kwa sababu anaona uchungu kwa tendo baya alilolifanya ila kwa sababu ya kuwa amekosea namna ya kulifanya na kumshindwa binadamu. Sisi tunapotenda dhambi, haitoshi kurudia kwenye kujuta kwani tukiishia  hapo, tutakuwa wenye kiburi na majivuno, hadi hapo tutakapochukua hatua ya kwenda mbele zaidi yaani kumwendea Mungu katika nafsi ya padre na kuungama. Huu ndiyo unyenyekevu  mkubwa. Ndiyo maana, asiyekuwa na fadhila ya unyenyekevu hataonekana kwenye chumba cha kitubio akaungama dhambi zake – kama anavyosema Petro, mzee mzima mbele ya watu wengi, wanawake na wanaume bila hata ya haya,

“Ondoka kwangu kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi, Bwana”

Hoja yenyewe ni hii, kigezo cha kufika mbinguni ni moyo safi lakini sisi binadamu ni dhaifu na na ni vigumu  kukaa bila kutenda dhambi kabisa, ndiyo maana mtume Yohane anasema. Tukisema kuwa hatuna dhambi tunajidanganya wenyewe na wala ukweli haumo ndani yetu (1Yoh 1:8). na Mungu anasogeleka endapo tu tutakuwa safi kiroho na usafi wenyewe unawezekana kwa tendo la kiunyenyekevu la kukiri au kama tunavyozoea kusema,  kuungama. Musa aliambiwa na Mungu vua Makubasi yako hapa ni mahali patakatifu. Makubasi hayo ni dhambi.

Katika hali ya dhambi hatuwezi kumsogelea Mungu. Lazima tuvue makubasi, ndiyo kusema lazima tujitakase dhambi zetu. Tunaweza kuchukua hatua hiyo ya kujitakasa kama kwanza tutakiri kwamba sisi ni wadhambi. Na ili kukiri kwamba sisi ni wadhambi tunahitaji fadhila hii muhimu ya unyenyekevu, kama alivyoonyesha Petro. Tunda la pili la fadhila hii ya unyenyekevu wa kukiri makosa yetu ni amani. Hili ni tunda la kimwili. Amani katika familia, jumuiya, kaya, n.k. kama akina baba wangekuwa wepesi wa kuinama mbele ya akina mama na kusema,

“Mimi ni mkosefu mke wangu”

Badala yake utakuta wanaume wengi husema, â€śKuoa nioe mimi, mahali nitoe mimi halafu nimpigie magoti mke wangu. Mkosi. Toka lini kuku jike anawika?” Wanandoa wasipoishi kwa unyofu na kuombana radhi, ndoa hiyo au itakuwa uwanja wa masumbwi na mwisho ni kuvunjika.(kuvunjana viungo)

“Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi, Bwana”

Basi ndugu zangu katika Kristo, sisi wote tunaitwa kuwa watakatifu kama baba yetu wa mbinguni alivyo mtakatifu. Lakini, sisi tu wadhaifu kufikia lengo hilo, lazima tuwe tunajisafisha kiroho. Kujisafisha huko kunawezekana endapo tutadumu katika fadhila ya unyenyekevu inayotupelekea kumpigia magoti mwenyezi Mungu na kuomba msamaha jambo ambalo tunapaswa pia kufanyiana sisi wenyewe. Tuombe Roho Mtakatifu atujalie fadhila ya unyenyekevu ili tuweze kufaidi tunda la kumwona Mungu hapo baadaye na tunda la amani katika jumuiya zetu.

Tafakari ya Dominika 9 Februari 2025
08 Februari 2025, 11:09