ĐÓMAPµĽş˝

Upendo wa Yesu kwa wote- Upendo wa Yesu kwa wote-  (Copyright 2021. All rights reserved.)

Dominika ya 7,Mwaka C:Ukuu na nguvu ya Upendo

Somo la I la kitabu cha kwanza cha Samweli linasimulia harakati za mfalme Sauli kutafuta kumuua Daudi sababu ya wivu kwa sifa alizopewa Daudi kwa uhodari wake wa kuliongoza jeshi katika vita dhidi ya wafilisti na kushinda.Somo la II ni Waraka wa kwanza wa Paulo kwa wakorinto,anatoa tofauti iliyopo kati ya mwili tulio nao sasa na ule utakaofufuliwa.Injili ya Luka (Lk 6:27-38)inahusu fundisho la amri kuu ya mapendo yasiyo na kikomo.

Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.


Tafakari la Neno la Mungu Dominika ya 7 ya mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya Domenika hii yanatuhimiza kuishi kwa upendo – kupendana sisi kwa sisi, kuwapenda na kuwaombea adui zetu ili nao waweze kubadilika na kuwa watu wema na zaidi sana tuepuke kulipiza kisasi kwa wale waliotukosea. Tukifanya hivi tunaweza kuimba na mzaburi wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya Dominika tukisema; “Nami nimezitumaini fadhili zako; moyo wangu na uufurahie wokovu wako. Naam, nimwimbie Bwana, kwa kuwa amenitendea kwa ukarimu” (Zab. 13:5-6). Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anaomba akisali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi, tunakuomba utujalie kuwaza daima mambo yanayofaa, na kutimiza kwa maneno na matendo yanayokupendeza”.

Somo la kwanza ni la kitabu cha kwanza cha Samweli (1Sam 26:2, 7-9, 12-13, 22-23). Somo hili linasimulia harakati za mfalme Sauli kutafuta kumuua Daudi sababu ya wivu kwa sifa alizopewa Daudi kwa uhodari wake wa kuliongoza jeshi katika vita dhidi ya wafilisti na kushinda. Mfalme Sauli alihofia kuwa watu wanaweza kumfanya Daudi kuwa mfalme badala yake. Wivu huu wa Sauli ulizaa chuki na hivyo kutaka kumuua Daudi. Daudi alipofahamu jambo hili, alikimbia na kwenda kujificha. Hivyo Sauli alichukua jeshi lake kwenda kumtafuta Daudi mchana kutwa bila mafanikio. Ilipofika usiku Sauli na jeshi lake walilala usingizi mzito. Daudi alipowakuta wamelala fofofo, Abishai rafiki yake alimwambia; Mungu amemtia adui yako Sauli mikononi mwako, haya harakisha umuue. Daudi alikataa akisema; “Ni nani awezaye kuunyoosha mkono wake juu ya masihi wa Bwana, naye akawa hana hatia”? Daudi akaweka matumaini yake kwa Mungu akisema; “Naye Bwana atamlipa kila mtu haki yake, na uaminifu wake”. Daudi akamsamehe adui yake Sauli aliyemtafuta kumuua, akimuombea mema kwa Mungu ili ajirudi na kubadilika. Moyo huu wa Daudi, Papa, Mtakatifu Yohane Paulo II katika barua yake ya huruma ya Mungu anasema hivi; Pale upendo ulipo, huruma ipo; na huruma hii inajidhihirisha katika kujitahidi kurudisha uzuri na thamani ya maisha, yaani kutoka hali mbaya aliyonayo mtu na kumrudishia matumaini na furaha katika maisha.

Ni katika muktadha huu, Mzaburi katika wimbo wa katikati anasema hivi; “Bwana amejaa huruma na neema. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, naam, vyote vilivyo ndani yangu, vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote, aukomboa uhai wako na kaburi, akutia taji ya fadhili na rehema. Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhila, hakututendea sawa sawa na hatia zetu, wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao” (Zab. 102:1-4, 8, 10, 12-13). Basi nasi tujifunze kwa Daudi, tusiwe watu wa kulipiza kisasi, tuwasamehe na kuwaombea adui zetu wanaotuchikia na kututakia mabaya katika maisha yetu, ili waweze kuongoka na kuwa watu wema.

 

Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa wakorinto (1Kor 15:45-49). Katika somo hili Mtume Paulo anatoa tofauti iliyopo kati ya mwili tulio nao sasa na ule utakaofufuliwa. Mwili wa sasa ni udongo, yaani dhaifu, lakini mwili utakaofufuliwa utakuwa na hali ya utukufu huko mbinguni. Mtume Paulo anatuasa tujitahidi kupambana na madhaifu yetu kwani hakuna aliye mkamilifu. Zaidi sana tusaidian sisi kwa sisi kwa upendo wa kidugu ili tuweze kuufikia utakatifu, wito wetu sote tunaoitiwa na Mungu Baba yetu aliyemtakatifu.

Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk 6:27-38). Sehemu hii ya Injili inahusu fundisho la amri kuu ya mapendo – upendo usio na kipimo, upendo wa kimungu, fadhila ya kimungu, kuwapenda watu wote bila upendeleo hata adui zetu na kuwatendea mema wanaotuchukia, kuwabariki wanaotulaani, kuwaombea wanaotuonea, kumgeuzia shavu la pili anayekupiga moja, kumuachilia joho lako anayekunyang’anya, na kutokumzuilia kanzu, kumpa anayekuomba, na anayekunyang’anya vitu vyako, usitake akurudishie, na kuwatendea watu tunayotaka tutendewe. Na zaidi sana tuwe na huruma, kama Mungu Baba yetu, tusiwahukumu wengine ili nasi tusijehukumiwa, tusilaumu, ili nasi tusilaumiwe, tuachilie ili nasi tuachiliwe. Tuwape watu vitu, nasi tutapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwa-sukwa hata kumwagika, tutakachowapimia wengine, ndicho tutakachopimiwa na sisi.

Fundisho hili kwa macho ya kibinadamu ni gumu mno, kwani liko kinyume na mtazamo wetu mbele ya adui zetu ambapo tunadai kuwalipa kadiri ya matendo yao maovu. Lakini kwa neema ya Mungu tunaweza kama tukifungua mioyo yetu na kumruhusu Roho Mtakatifu afanye kazi ndani yetu tutaweza kuyaishi haya maagizo ya amri kuu ya mapendo. Upendo huu si kingine isipokuwa kuiweka nafsi ndani ya nafsi nyingine na kuweza kuhisi anachohisi mwingine; iwe ni uchungu, furaha, au maumivu. Ni kukaa ndani ya mwingne: “Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu” (Yh, 15:4). Ni kulishika na kuliishi neno la Mungu: “Mtu akinipenda atalishika neno langu, na Baba yangu atampenda nasi tutakuja kwake na kukaa naye” (Yh, 14:23).

Upendo huu unatudai kutotafuta faida binafsi bali ya wengine: “pasiwe na mtu anayetafuta faida yake mwenyewe tu bali faida ya mwenzake” (Fil. 2:4). Baba mtakatifu Benedicto XVI katika barua yake ya Mungu ni Upendo “Deus caritas est” anasema; Upendo una hulka au tabia ya kuwafikiria wengine, hautafuti faida yake binafsi, bali faida ya mpendwa. Unapopenda unakuwa na majikatalio na uko tayari hata kujitoa sadaka kwa ajili ya umpendaye. Huu ndio uzoefu wa wapendanao: kila mmoja anakandamiza matashi yake na kutekeleza ya mwenzake kwanza. Upendo wa aina hii ni zawadi, ni fadhila kutoka kwa Mungu aliye asili ya upendo. Upendo huu haununuliwi bali unajitoa wenyewe. Ndiyo maana “mtu akijaribu kununua pendo, akajitolea mali yake yote, atakachopata ni dharau tupu” (Wim. 8:7).

Mungu aliye upendo ametufunulia maana halisi ya upendo. Upendo ni kumwambia siri zako umpendaye – Mungu ametufunulia siri za umungu wake kwa njia ya mwanae Yesu Kristo. Upendo ni kuteseka kwa ajili ya umpendaye – Mungu ameteseka kwa ajili yetu hata kufa Msalabani. Ndiyo maana Yesu anasema hivi; “Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko huu wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yh.15:13). Upendo ni kuwa mmoja na umpendaye, umoja wa kimwili na umoja wa kiroho – Mungu ameweka Ekaristi Takatifu ili akae nasi katika maumbo ya mkate wa uzima. Upendo hutamani kuungana na umpendaye milele – Mungu ametuahidi heri ya milele mbinguni ambapo tutamwona kama alivyo. Mtume Paulo anasisitiza hivi; “Nasema ukweli mtupu; nimeungana na Kristo nami sisemi uongo” (Rum. 9:1).

Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika “Caritas in veritate” “Ukweli katika upendo”, anasema; “upendo ni msukumo usio wa kawaida, unaopelekea watu kuchagua kwa ushujaa, kujishughulisha kwa ukarimu katika nyanja za haki na amani. Anayependa kikamilifu anajishikamanisha na matashi ya mpendwa wake. Mtakatifu Yohane Chrisostom anasema; “Ni tabia ya mpenzi kutokuchoka kutenda kile kinachompendeza mpendwa wake.” Hakuna chenye kuamrisha zaidi kama upendo kwa kuwa “pendo lina nguvu kama kifo”. Tena pendo lilivyo na nguvu, “maji mengi hayawezi kamwe kulizima, mafuriko hayawezi kulizamisha” (Wim, 8:6). Pendo lenyewe kwenye shida liko imara, kadhalika kwenye furaha liko imara; kwake shida na raha ni mamoja. Mtume Paulo anauliza; “Nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo...Je ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo?” (Rum. 8:35). “Hakuna kiwezacho kututenga na upendo wa Kristo – anajibu Paulo – wala kifo, wala uhai, wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni, wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka; wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kiwezacho kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana wetu” (Rum. 8:38-39).

Mtume Paulo anapowaandikia Wakorinto waraka wake wa kwanza anataja sifa za upendo; Upendo daima huvumilia, ni mpole, hauna wivu, haujidai, haujivuni, una adabu, tena hautafuti faida yake binafsi, haufurahii maovu, bali ukweli. (1Kor, 4-6). Hii ndiyo picha halisi ya upendo. Ni katika upendo Daudi hakunyanyua mkono wake kumuua Sauli aliyetaka adui yake. Nasi tuuishi upendo ambao kimsingi ni amri, ili tuingie mbinguni lazima tumpende Mungu na jirani hata kama ni adui, vinginevyo hatuwezi kuiona mbingu. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, sisi tunaoadhimisha mafumbo yako ipasavyo, tunakuomba sana, hayo tunayokutolea kwa heshima ya utukufu wako yatufae kwa wokovu”. Na katika sala baada ya komunyo anahitimisha maadhimisho ya Dominika hii akisali hivi: “Ee Mungu Mwenyezi, tunakuomba utujalie kupata wokovu ambao amana yake tumeipata kwa mafumbo haya”. Na hili ndilo tumaini letu, kuupata wokovu wa milele mbinguni.

Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari ya Dominika ya 7 Mwaka C
21 Februari 2025, 08:46