MAP

2025.02.14  Donika ya 6 ya Mwaka C Yesu anatangaza  Heri za Mlimani. 2025.02.14 Donika ya 6 ya Mwaka C Yesu anatangaza Heri za Mlimani. 

Domenika ya 6,Mwaka C:Hakuna yeyote duniani aliyewahi kutangaza aliyotangaza Yesu katika“HERI”

Kama tungewauliza watu waorodheshe vitu ambavyo kwa mtazamo wao vinaleta au kuongeza raha au furaha,hakika wangetaja:fedha,afya njema,kazi,amani katika familia,nyumba nzuri,gari marafiki waaminifu.Yeyote anayesikia maneno ya Yesu kwa mara ya kwanza:“Heri walio maskini,njaa,wanaolia…atashangaa na kusema kuwa anayetoa maneno haya ni lazima awe amerukwa na akili. Ni tafakari ya Padre Ighondo kuhusu Dominika ya 6 ya Mwaka C.

Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.


Katika Dominika ya 6 ya Kipindi cha Mwaka C, wa Kanisa masomo yanatoka: Yer 17:5-8; Zab 1: 1-4, 6; 1 Kor 15: 12, 16-20; na Injili ya Lk 6: 17, 20-26. Katika sehemu ya Injili hii ni mwanzo wa mafundisho makuu ya Yesu ambayo huitwa Hotuba ya mlimani.” Sehemu ya kwanza ya mafundisho haya ya Yesu huitwa “Heri” yaani “Baraka.” Heri hizi zinasimuliwa na Mwinjili Mathayo na Luka tu. Luka anataja heri nne zikifuatiwa na “Ole. Heri ninyi mlio maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu. Heri ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashiba. Heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka. Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu kwa ajili ya Mwana wa Adamu, furahini siku ile na kurukaruka, kwa kuwa tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni. Ole wenu ninyi mlio na mali, kwa kuwa faraja yenu mmekwisha kuipata. Ole wenu ninyi ambao mmeshiba sasa, kwa kuwa mtaona njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka sasa, kwa kuwa mtaomboleza na kulia. Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo.


Mathayo anatupa Heri nne za kwanza kama zile za Luka ila inaongeza nyingine nne: Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi, maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa sababu ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni wao. Mathayo pia anaongeza neno juu ya zile “Heri” alizotaja Luka. Kwenye neno “Maskini” Mathayo anaongeza “wa roho.” Maadui wa heri ni ubinafsi: kujilimbikizia kupita mahitaji yetu, wivu ambao ni hali ya kutoridhika na wengine kupata mafanikio kana kwamba kufanikiwa kwao kunatokana na wao kutuibia sisi. Tamaa potovu ya kupata mali: uroho ni jambazi asiyeridhika wala kushiba. Husuda au jicho baya: mtu yule apataye huzuni au chuki dhidi ya wale waliofanikiwa

Hakuna yeyote duniani aliyewahi kutangaza aliyotangaza Yesu katika “heri”. Kama tungewauliza mamia ya watu: Unapenda kuwa na furaha? Wote wangejibu wakisema: Swali gani hilo. Unapigia mstari majibu! Hakuna asiyependa kuwa na furaha. Kila mmoja anapenda na kutamani kuishi maisha ya furaha na raha. Na kama tungewauliza watu waorodheshe vitu ambavyo kwa mtazamo wao vinaleta au kuongeza raha au furaha, hakika wangetaja: fedha, afya njema, kazi, amani katika familia, nyumba nzuri, gari, marafiki waaminifu na kadhalika. Tuna hakika kwamba katika orodha ile hakuna atakayesahau kutaja pesa tena kuipa nafasi ya kwanza.

Yeyote anayesikia maneno ya Yesu kwa mara ya kwanza: “Heri walio maskini, heri wenye njaa, heri wanaolia…atashangaa na kusema kuwa anayetoa maneno haya ni lazima awe amerukwa na akili. Hakuna anayeweza kuwafikiria maskini, wenye njaa na waliao kama watu wenye bahati na heri. Kinyume chake wanaonekana kama watu walioadhibiwa au kulaaniwa. Njaa, umaskini na kilio kwa mtazamo wa kidunia ni “uovu” ambao kila mmoja anapaswa kuuepuka. Watu wanaalikwa kuwaonea huruma watu waliopatwa na jangwa la umaskini na njaa. Ni kweli kwamba hatupaswi kuushangaa sana mtazamo huo wa kidunia. Ni katika mwanga wa imani tunaweza kuelewa maana ya Heri hizi.

Ni kitu gani ambacho hakumaanisha Kristo katika tangazo lake la “Heri.”? Kristo hakumaanisha kwamba kuwa maskini, kulia, kuwa na njaa na kuteswa ni mambo mazuri. Mungu hakusababisha mambo haya kwa ajili ya mwanadamu. Mwanadamu ndiye aliyejisababishia mambo haya. Ni matokeo ya dhambi. Kristo anataka tutumie kila juhudi tuwezayo ili kuondokana na umaskini, kuboresha hali ya maisha. Wakati wa maisha yake hapa duniani, Yesu alihisi njaa (Lk 4:3), aliwalisha umati uliomfuata na kumsikiliza walipokuwa na njaa (Lk 9:10-17), aliwaonea huruma na kuwafariji waliokuwa na huzuni, hata akatoa machozi - mjane wa Naimu aliyefiwa na mwane (Lk 7:14-15), urafiki na familia ya Lazaro (Lk 8:1-3). Kwa maneno machache, kukosa mahitaji msingi na muhimu ya maisha hususani chakula, mavazi, makazi, kuteswa na kuathiriwa kwa namna yeyote ile ilikuwa hata kwa Yesu “mambo mabaya – ‘uovu” kama ilivyo kwetu sisi.

Kumbe tunaona kuwa yale ambayo kwa macho ya kawaida ni maovu, kwa macho ya imani yanaweza kuwa ngazi ya kuelekea katika ufalme wa Mungu. Aliye maskini wa kweli ni yule anayemtegemea Mungu katika ukamilifu wake, ni yule asiyejiamini kipumbavu katika nguvu na uwezo wake. Umaskini hautokani na wingi au uchache wa vitu vya kidunia, bali katika maambatano yetu na mambo hayo. Daima tutambue madhaifu na mapungufu yetu na kwamba hatuwezi chochote pasipo Mungu. Kadiri tunavyojiachia kwa Mungu tukimtegemea, ndivyo tunavyokuwa salama zaidi na tayari kuingia katika Ufalme wa Mungu. Bwana Yesu alimtegemea Mungu wakati wote na hivyo Mungu alimjalia nguvu ya kupambana na uovu wa kila aina na mwisho akavikwa taji la utukufu na utawala katika Ufalme wa Mungu huko mbinguni.

Basi nasi katika Dominika hii ya 6 ya mwaka C wa Kanisa tutafakari "Heri" hizi za Mlimamani ambazo Yesu anatupatia kama njia nzuri au dira ya kufuata ili kuweza kumfia huko Mbinguni.

Tafakari ya Dominika ya 6 mwaka C

 

 

 

14 Februari 2025, 17:33