ĐÓMAPµĽş˝

Mungu anapomchagua na kumwita mtu ili amtumikie,haangalii ukamilifu wake bali moyo wake wa unyenyekevu na utayari wake wa kutambua hali yake ya dhambi,kutubu na kuwa tayari kufuata maongozi yake. Mungu anapomchagua na kumwita mtu ili amtumikie,haangalii ukamilifu wake bali moyo wake wa unyenyekevu na utayari wake wa kutambua hali yake ya dhambi,kutubu na kuwa tayari kufuata maongozi yake.   (ANSA)

Domenika ya 5,Mwaka C:Wito Dhambi na maisha ya utakatifu

Katika masomo ya Dominika tunaona historia ya watu walioitwa na Mungu kuwa wajumbe wake ina mambo yanayofanana na jinsi Mungu alivyowaita na walivyoitika licha ya kuwa waliitwa katika nyakati tofauti, hawakufahamiana kwa kuwa walitenganishwa na muda mrefu,mahali,elimu na hata mila na tamaduni zao zilitofautiana.Kwanza Mungu aliwaita pasipo wao kutarajia.Na kila aliyeitwa hisia za kutostahili zilimjia kwa kujiona mdhambi hivyo kuweka vipingamizi ili Mungu asimtumie.

Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 5 ya Mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa masomo ya Dominika hii umekitika katika wito kama zawadi kutoka kwa Mungu ambapo anapomchagua na kumwita mtu ili amtumikie, haangalii ukamilifu wake bali moyo wake wa unyenyekevu na utayari wake wa kutambua hali yake ya dhambi, kutubu na kuwa tayari kufuata maongozi yake. Ili haya yatendeke anayeitwa anapaswa kuwa mkweli kwa nafsi yake, kuisikiliza sauti ya Mungu, kutambua udhaifu wake, kuukiri. Ili kuyaweza haya mzaburi katika wimbo wa mwanzo anatoa ushauri akisema hivi; “Njoni, tuabudu, tusujudu, tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba; kwa maana ndiye Mungu wetu (Zab. 95:6-7). Mama Kanisa akiwa na tumaini hili, katika sala ya mwanzo anatuombea akisali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba utulinde sisi watoto wako kwa pendo lisilo na mwisho. Na kwa kuwa twategemea tu neema yako ya mbinguni utuhifadhi daima kwa ulinzi wako”.

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Is 6:1-2a, 3-8). Somo hili linahusu kuchaguliwa na kuitwa kwa Isaya kuwa nabii. Kuitwa kwake kunatokea katika maono ambapo Isaya aliona utukufu wa Mungu katika Hekalu la Yerusalemu katika sehemu ya ndani kabisa iliyoitwa “Patakatifu pa Patakatifu” – palipokuwa na jiko lenye makaa ya moto ambapo Kuhani mkuu pekee aliruhusiwa kuingia, mara moja tu kwa mwaka katika sikukuu ya maondoleo ya dhambi kwa ajili ya kutolea dhabihu za kuteketeza na kuchoma ubani mpaka chumba kile kijae moshi, ishara ya sala za waamini kupaa mbele za Mungu na kupokelewa. Katika hali hii Isaya aliwasikia Malaika wakimsifu Mungu kwa maneno ambayo ni kiunganishi kati ya Prefasio na Sala ya mageuzo(sala ya Ekaristi katika Misa): “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa Majeshi, Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.”

Mbele ya macho ya Mungu Mtukufu na Mtakatifu, Nabii Isaya alitambua hali yake ya udogo na ya kuwa ni mdhambi, asiyestahili kufanya kazi ya Mungu, hivyo akaogopa, akatetemeka na kusema; Ole wangu! “Mimi niliye na midomo michafu na ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu” na macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wamajeshi. Ndipo alipomwona malaika akichukua kaa la moto kutoka katika tanuru iliyoko altareni, na kugusa midomo yake kwa ule mkaa uwakao, akamtakasa dhambi zake na kumweka wakfu kuwa mjumbe wa Mungu. Ndipo sasa Isaya akaitika wito wa Mungu na kusema; “Mimi hapa Bwana, nitume mimi” (Isa 6:9).

Kama Nabii Isaya, sisi tunapaswa kutambua kuwa tu wakosefu hatustahili kumkaribia Mungu aliye mtakatifu mno. Yatupasa kwanza kutakaswa naye katika sakramenti ya kitubio ili tuweze kuitikia mwito wake na kusema; “Mimi hapa Bwana, nitume mimi” (Isa 6:9). Ni katika tumaini hili mzaburi katika wimbo wa katikati anasema hivi; “Ee Bwana, nitakushukuru kwa moyo wangu wote. Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi, nitakusujudu nikilikabili hekalu lako takatifu. Nitalishukuru jina lako, kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako, kwa maana uzima umeikuza ahadi yako, kuliko jina lako lote. Siku ile niliyokuita uliniitikia, ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. Ee Bwana, wafalme wote wa dunia watakushukuru, watakapoyasikia maneno ya kinywa chako. Naam, wataziimba njia za Bwana, kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu. Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu, na mkono wako wa kuume utaniokoa. Ee Bwana, fadhili zako ni za milele; usiziache kazi za mikono yako (Zab. 137: 1-5, 7-8).

Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 15:1-11). Katika somo hili Mtume Paulo anatufundisha kuwa imani yetu juu ya ufufuko wa Kristo ina msingi thabiti kabisa - Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu. Lakini pia mtume Paulo anatambua makosa yake aliyoyafanya ya kuliudhi Kanisa la Mungu kabla ya kuongoka kwake na kuwa mtume wa mataifa. Ni kwa neema ya Mungu amekuwa mtume na neema hiyo si bure, bali ni ya kufanya kazi ya utume na wala si yeye aliyeweza kuhubiri kwa juhudi zaidi ya wengine, bali ni neema ya Mungu iliyo pamoja naye.

Itakumbukwa kuwa kabla ya kuongoka kwake akiitwa Sauli, alipotumwa na Makuhani wa Yerusalemu kwenda Damaski kuwakamata, kuwatesa na kuwatenda jeuri wafuasi wa Kristo, aliona kuwa anatenda kazi ya Mungu. Njiani Yesu alipojifunua kwake alimuuliza: “Wewe ni nani Bwana.” Yesu alimjibu; Mimi ni Yesu, unayenitesa” (Mdo 9:5). Sauli alitambua dhambi zake, akawa kipofu wa kimwili, ili aangaziwe utukufu wa kiroho na kuona vitu katika uangavu wake. Mbele ya Anania, alielezwa anachopaswa kufanya, akakubali kubatizwa na kupata kuona tena. Akiongozwa na Roho Mtakatifu alienda jangwani, na huko kwa njia ya sala, alijifunza mpango wa Mungu katika maisha yake. Baadae alianza kuhubiri habari za ufalme wa Mungu, akimtangaza Kristo huko Damaski, Yerusalemu, na mwisho katika himaya ya Kirumi. Kutokana na ari yake, ulimwengu wa wakati ule ulionekana mdogo sana. Alifanya safari za kimisionari ili kumtangaza Kristo na ufalme wa Mungu. Daima alijiona hana mastahili ya kuwa mjumbe wa Injili ya Kristo na kusema: “Maana mimi ni mdogo kati ya mitume, nisiyestahili kuitwa mtume” (1Kor 15:9). Lakini aliyaweka matumaini yake yote kwa Mungu kama anavyosema; “Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa kama nilivyo na Neema yake kwangu haikuwa bure, bali ni neema ya Mungu pamoja nami” (1Kor 15:10).

Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk 5:1–1). Sehemu hii ya Injili inahusu kuitwa kwa Simoni Petro, Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo kuwa wafuasi wa Kristo wakiwa wanavua samaki katika ziwa Genezareti, (lijulikanalo pia kama ziwa Galilaya au ziwa Tiberia). Kabla ya kuwaita, Yesu aliwahubiria makutano akiwa ndani ya mtumbwi wa Petro. Alipomaliza aliwaagiza watupe nyavu zao ili wavue samaki, kazi waliyoifanya usiku kucha bila mafanikio. Lakini kwa neno la Yesu, walitii, wakatupa nyavu, wakapata samaki wengi kiasi cha nyavu zao kuanza kukatika na hivyo kuomba msaada kwa rafiki zao. Kitendo hiki kilimfanya Petro kujaa hofu na mashaka na kusema; “Ondoka kwangu Ee Bwana, kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi.” Lakini Yesu alimwambia, usiogope, tangu sasa utakuwa mvuvi wa watu. Katika masomo haya tunaona kuwa historia ya watu walioitwa na Mungu kuwa wajumbe wake ina mambo kadhaa yanayofanana jinsi Mungu alivyowaita na walivyoitika licha ya kuwa waliitwa katika nyakati tofauti, hawakufahamiana kwa kuwa walitenganishwa na muda mrefu, mahali, elimu, na hata mila na tamaduni zao zilitofautiana.

Kwanza kabisa Mungu aliwaita pasipo wao kutarajia. Na kila aliyeitwa hisia za kutostahili zilimjia kwa kujiona mdhambi na hivyo kuweka vipingamizi ili Mungu asimtumie. Lakini Mungu aliwaimarisha na kuwastahilisha kwa kuwaambia msiogope maana kazi wanayoipewa si yao bali ni yake Mungu. Baada ya kuhakikishia msaada wa Mungu, kwa unyofu na ushupavu waliukabili mpango wa Mungu, hata wakati ule wa majaribu na mateso waliamini kwamba Mungu yuko pamoja nao. Lakini kukubali kwao kuliongozwa na fadhila ya unyenyekevu. Ni mwaliko kwetu kujivika fadhila ya unyenyekevu ili ituwezeshe kukiri na kuungama makosa yetu mbele za Mungu na wenzetu. Fadhila hii inatupa nafasi ya kufika mbinguni kwani inatustahilisha kuwa kama watoto wadogo. Na Yesu alisema hivi; “Msipokuwa kama watoto wadogo, hamwezi kuingia katika ufalme wa mbinguni”(Mt 18:3; Lk 18:17). Mtu akikosa fadhili ya unyenyekevu, hawezi kamwe kukiri makosa yake na kujuta na kuomba msamaha, na hivyo anajifungia njia ya kwenda mbinguni kwa kujifanya hana dhambi. Na tukisema kuwa hatuna dhambi tunajidanganya wenyewe na wala ukweli haumo ndani yetu (1 Yh 1:8).

Lakini ili tuweze kujitambua na kujikubali kuwa sisi ni wenye dhambi, lazima tuyalinganishe maisha yetu na maisha ya Kristo. Yeye awe mizani ya uadilifu wetu. Kamwe usijilinganishe na watu wengine; jilinganishe na Kristo maana “mtu yeyote anayesema kwamba ameungana na Mungu, anapaswa kuishi kama alivyoishi Kristo” (1 Yh 2:6). Tukijilinganisha na watu wengine, tutajiona tu wakamilifu, hatuna dhambi, wema na wenye haki.  Isaya hakutambua uovu wake wala wa watu wake mpaka alipouona utukufu wa Mungu. Paulo hakutambua uovu wake mpaka alipokutana na Krsito. Na Petro aliutambua udhambi wake alipoyaweka maisha yake mbele ya Kristo. Wakati mwingine tunawatumia watu wengine kuwa vipimo vya uadilifu wetu na kuhalalisha matendo maovu kwa kusema “hata wengine wanafanya hivyo. Maneno haya si suluhisho” maana “hata wao wana midomo michafu”. Sera za kiulimwengu haziwezi kuwa mizani ya maadili yetu kwa maana zima “midomo michafu.” Tujifunze kutoka kwa mitume kuacha yote yanayotutenga na Kristo – hasira, ubaguzi, wivu, urafiki mbaya, uongo, usengenyaji, dharau na mengine kama hayo.

Lakini kuacha dhambi unayoipenda si kazi rahisi. Ili kuitakasa midomo ya Isaya lilitakiwa kaa la moto ambalo hata Malaika aliogopa kulishika kwa mikono na hivyo alitumia koleo lipitishwe katika midomo yake. Lakini hili ndilo kaa lililohitajika ili kumtakasa Isaya. Kwetu sisi tunahitaji kukisogelea kiti cha maungamo kwa moyo wa unyenyekevu na majuto. Usiseme dhambi yangu ni ngumu siwezi kuachana nayo au siwezi kusamehewa. “Mtumaini Mungu kwa moyo wako wote wala usizitegemee nguvu zako mwenyewe” (Meth.3:5). Kumbuka daima kuwa ni walio wagonjwa ndio wanaomhitaji daktari na Yesu hakuja kwa watu walio wema bali kwa wadhambi ili wapate kutubu (Mk 2:17). Nenda katika Sakramenti ya Kitubio “bila fedha na bila thamani” (Isa.55:2). Yesu anatualika; Njooni nyote wenye kusumbuka na kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha (Mt 11:28). Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana Mungu wetu, umeumba vitu hivi ili vitusaidie hasa katika unyonge wetu. Tunakuomba utujalie viwe pia sakramenti ya kutuletea uzima wa milele”. Na katika sala baada ya Komunio anahitimisha maadhimisho haya akisali hivi; “Ee Mungu, umependa tushiriki mkate mmoja na kikombe kimoja. Tunakuomba utujalie kuishi tumeungana na Kristo, tupate kuzaa matunda kwa furaha kwa manufaa ya wokovu wa ulimwengu”. Na hili ndilo tunamaini letu.

Tafakari ya Dominika ya V Mwaka C
06 Februari 2025, 11:11