MAP

Wafanyikazi wakitengeneza  maboya kwenye mpaka wa Marekani na Mexico huko Eagle Pass, Texas kuzuia wahamiaji. Wafanyikazi wakitengeneza maboya kwenye mpaka wa Marekani na Mexico huko Eagle Pass, Texas kuzuia wahamiaji.  (CHENEY ORR)

Rais wa Maaskofu Marekani ajibu utendaji wa Trump:mafundisho ya Kanisa hayajabadilika!

Askofu Mkuu Broglio,Rais wa Baraza la Maaskofu Marekani,alijibu kuhusu maagizo ya utendaji yaliyotiwa saini na Rais Trump.“Ombi letu ni la matumaini kuwa,kama Taifa lililobarikiwa kwa karama nyingi,matendo yetu yanaonesha utunzaji wa kweli kwa dada na kaka zetu walio katika mazingira magumu zaidi,wakiwemo ambao bado hawajazaliwa,maskini,wazee,wahamiaji na wakimbizi.Jaji mwadilifu hatarajii chochote kidogo.”

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kwa kujibu Maagizo ya Utendaji ya Juma hili yaliyotiwa saini na Rais Donald Trump mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa 47 wa Marekani, Askofu Mkuu Timothy P. Broglio, rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani (USCCB) alitoa taarifa ifuatayo kwamba: “Masuala mengi ambayo Rais Trump anayashughulikia katika Maagizo yake ya hivi karibuni ya  Utendaji, pamoja na yale ambayo yanaweza kutolewa katika siku zijazo, ni mambo ambayo Kanisa lina mengi ya kutoa. Baadhi ya masharti yaliyomo katika Maagizo ya Utendaji, kama vile yale yanayolenga kushughulikia wahamiaji na wakimbizi, misaada ya kigeni, upanuzi wa adhabu ya kifo, na mazingira, yanasumbua sana na yatakuwa na matokeo mabaya, ambayo mengi yatawadhuru walio hatarini zaidi kati yetu. Masharti mengine katika Maagizo ya Utendaji yanaweza kuonekana katika mtazamo chanya zaidi, kama vile kutambua ukweli kuhusu kila binadamu kama mwanamume au mwanamke.”

Kanisa Katoliki halifungamani na chama chochote cha kisiasa 

Askofu Mkuu aidha anabinisha kuwa: "Ningependa kusisitiza kwamba Kanisa Katoliki halifungamani na chama chochote cha kisiasa, na pia Baraza la Maaskofu. Haijalishi ni nani anayekalia Ikulu ya White House au anayeshikilia wengi kwenye Capitol Hill, mafundisho ya Kanisa bado hayajabadilika. Ni matumaini yetu kwamba uongozi wa Nchi yetu utaangalia upya matendo yale ambayo yanadharau sio tu hadhi ya watu wachache, bali na sisi sote. Kufuatia mapokeo ya kale, Papa Francisko alitangaza mwaka 2025 kuwa Mwaka wa Jubilei ya Matumaini. Kama Wakristo, tumaini letu daima liko kwa Yesu Kristo, ambaye hutuongoza kupitia dhoruba na hali ya hewa tulivu. Yeye ndiye chanzo cha ukweli wote. Ombi letu ni la matumaini kwamba, kama Taifa lililobarikiwa kwa karama nyingi, matendo yetu yanaonesha utunzaji wa kweli kwa dada na kaka zetu walio hatarini zaidi, wakiwemo wale ambao hawajazaliwa, maskini, wazee na wasiojiweza, na wahamiaji na wakimbizi. Jaji mwadilifu hatarajii chochote kidogo.” Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Marekani(USCCB) hata hivyo itachapisha maelezo ya ziada yanayohusu Maagizo maalum ya Mtendaji kupitia tovuti yake . 

Mahojiano

Katika mahojiano ya mwandishi Domenico Agasso katika Gazeti “LA STAMPA”na Rais wa maaskofu Katoliki nchini Marekani Timothy Broglio na Msimamizi wa Jimbo la Kijeshi,anabainisha kuwa "hii ni hatua za enzi nyingine. Ni upuuzi kukiuka shule na makanisa, hatuwezi kukaa kimya." Kwa njia hiyo Kanisa nchini Marekani linapinga njia wazi ya Donald Trump kwa uvamizi wa polisi "katika makanisa, hospitali na shule ili kutazama uraia" na ikiwezekana kuwazuia na kuwafukuza wahamiaji haramu. “Mateso yanamwakilisha Kristo, tutahukumiwa jinsi tulivyowatendea. Na kisha, kuwafukuza pia haina tija kwa nchi.

Yafuatayo ni mahojiano hayo

Mwashamu, Tycoon ametangaza na anatekeleza sera kali za uhamiaji. Unafikiri nini?

“Msimamo wa Maaskofu wa Marekani juu ya uhamiaji uko wazi. Tunataka kuheshimu sheria, lakini tunatambua kwamba inahitaji marekebisho. Mfumo wa sasa haushughulikii ipasavyo hali nyingi tata, kama vile wazazi ambao wanakiuka sheria lakini wana watoto wadogo ambao ni raia wa U.S. Kama nchi, hatujafanya vya kutosha kushughulikia vyanzo vya umaskini ambavyo vinasukuma watu wengi kutafuta maisha bora hapa. Tunapokabiliwa na wale walio na njaa, kiu, au katika shida au magonjwa, tunaitwa kujibu kulingana na Injili (Mt 25), kwa sababu watu hawa wanamwakilisha Kristo, na siku moja tutahukumiwa jinsi tulivyoitikia. Tunakusudia kufanya mazungumzo na Serikali mpya ili kushughulikia hali hizi madhubuti kwa njia inayowezekana. Pia tunatambua kwamba kuna tatizo la ajira nchini Marekani: hakuna watu wa kutosha kujaza nafasi zilizopo. Kuwafukuza wafanyikazi ambao ni muhimu kwa uchumi hakutakuwa na tija."

Rais aliidhinisha kukamatwa kwa wahamiaji hata makanisani na shuleni. Maoni yako ni yapi?


"Nimetoa taarifa rasmi ambayo, pamoja na kukiri baadhi ya mambo chanya katika hatua za kwanza za Serikali mpya, inakosoa vikali uamuzi wa kuruhusu vyombo vya sheria kuingia makanisani, hospitali na shuleni kukagua raia. Inaonekana kama kipimo kutoka wakati mwingine. Ni muhimu kuheshimu utakatifu wa shule na mahali pa ibada. Kuhusu wagonjwa, hatuwezi kukaa kimya. Maandamano ya kila mwaka ya kuunga mkono maisha na hadhi ya binadamu yatafanyika mjini Washington siku ya Ijumaa. Hakika hatutakosa kuwakumbuka wale wanaotishwa leo."

Uhusiano wa Trump na Papa Francisko umekuwa mgumu kila wakati. Je, inawezekana kuwa bora?

"Kwa kuzingatia uzoefu wangu wa miaka 25 kama mwanadiplomasia wa Vatican nina hakika kwamba itawezekana kufafanua, na kwamba uhusiano kati ya Vatican na Marekani utaimarika. Rais ana majukumu yake ya kusimamia na kuhutubia, wakati Askofu wa Roma lazima aseme wazi kuwatetea maskini, waliotengwa na wasio na uwezo. Haipaswi kuwa na kutokubaliana, lakini wakati huo huo ni kawaida kwamba tofauti zinaweza kuibuka katika baadhi ya masuala."

Marekani inatoa ushawishi mkubwa katika matukio mengi ya vita. Je, utawala mpya unapaswa kuwa na mtazamo gani katika kuimarisha amani?


"Kwa kuzingatia uwezo wa Marekani, tuna kazi ya kuwezesha mazungumzo, kupunguza mauzo ya silaha na katika baadhi ya matukio, kusisitiza kwamba wapiganaji waje kwenye meza ya mazungumzo."

Papa alishutumu "vita vya dunia vya tatu viilivyogawanyika vipande vipande". Je, Marekani ina wajibu gani maalum wa kushughulikia mizozo inayoendelea?

"Ndiyo, ninaamini wana fursa na wajibu wa kufanya zaidi ili kuendeleza upatanisho. Nikiwa mchungaji wa wale wanaotumikia taifa katika jeshi, ninajua vizuri gharama ya ushiriki huo. Tuna wajibu wa kuwa nguvu ya amani."

Je, urais mpya utaweza kuleta matokeo katika mazingira ya moto Mashariki ya Kati?


"Ndio, lakini ni muhimu kwamba kuwe na nia ya kisiasa ya kuhakikisha usalama wa Taifa la Israeli na wakati huo huo, kuhakikisha taifa huru kwa Wapalestina. Kutofanya chochote kunaweza kumaanishakuacha wajibu na kuruhusu hali ilivyo kuendelea kwa muda usiojulikana."

Ripoti ya Maaskofu wa Marekani kuhusu Trump
23 Januari 2025, 09:28