Mtakatifu na Angela Merici:Kila neema muombayo kwa Mungu mtapewa bila ya kukosa!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kila tarehe 27 ya kila mwaka, mama Kanisa anamkumbuka Mtakatifu Angela Merici, Bikira aliyezaliwa tarehe 21 Machi 1474 huko , Lombardia, Kaskazini mwa Italia. Akiwa na umri wa miaka 10, wazazi wake walifariki dunia na akabaki na dada yake tu. Na baada ya muda mfupi, dada yake nae akafariki dunia. Mtakatifu Angela Merici alijiunga na Utawa wa tatu wa Mtakatifu Francisko wa Assisi, ambako aliweka nadhiri ya ubikira. Akiwa na miaka 20, mjomba wake, ambaye ndiye aliyekuwa mlezi wake, alikufa. Mtakatifu Angela aliamua kurudi kijijini kwao ambako aliona wasichana wengi wakiishi maisha yasiyo mpendeza Mungu. Hawakuwa na elimu wala matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Na wazazi wao hawakujali. Mtakatifu Angela Merici aliamua kufungua kituo nyumbani kwao, akiwafundisha wasichana hao kuhusu: Katekesi, na Sala hususan juu ya imani ya Kanisa Katoliki. Mwaka 1524 alifanya hija katika Nchi Takatifu, lakini alipata maradhi ya upofu katika kisiwa cha Crete. Aliendelea na hija hiyo akiwa kipofu akipita sehemu zote. Akiwa njiani kurudi nyumbani, aliweza tena kuona. Kunako Mwaka 1525 alienda mjini Roma ili kuhiji na Papa alisikia habari zake na alimfurahia mno.
Ilikuwa mnamo tarehe 25 Novemba 1535, Mtakatifu Angela akiwa na mabikira 12, walianzisha rasmi Shirika la Watawa wa Ursoline. Shirika lilikuwa na kupanuka kiasi hata cha kuweza kufungua vituo vya kulelea watoto yatima na shule. Mwaka 1537 Mtakatifu Angela alichaguliwa kuwa mkuu wa Shirika. Sheria, Kanuni na Taratibu za shirika zilipitishwa mwaka 1544 na Papa Paulo III. Mtakatifu Angela Merici aliitwa na mwenyezi Mungu hapo, tarehe 27 Januari 1540 kwa kutimiza kile ambacho Mtakatifu Francisko wa Assisi kifo alikiita Dada. Na alizikwa katika Kanisa la Mtakatifu Afra Brescia. Alitangazwa kuwa Mwenyeheri mnamo tarehe 30 Aprili 1768 na Papa Clement XIII. Akatangazwa kuwa Mtakatifu tarehe 24 Mei 1807 na Papa Pio VII. Ni katika muktadha wa maisha yake na tasaufi yake, kuna mashirika mengi ya Waorsoline yaliyoibuka na kuenea sehemu mbalimbali dunia kote. Mtakatifu Angela Merici akiwa anaongozwa na Neno la Mungu katika maisha na utume wake, aliwahimiza watawa wake, kuhakikisha kwamba, wanajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa Mungu na jirani zao. Mtakatifu Angela Merci aliwataka kujizatiti kwa ujasiri katika sekta ya elimu kwa ajili ya watoto na vijana wa kizazi kipya, huku akiwataka kuendelea kuhifadhi mila na desturi njema, tayari kuanza mchakato wa ujenzi wa maisha mapya. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Angela Merici ni mfano bora wa kuigwa katika kusoma, kulitafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika maisha, ili kulitangaza na kulishuhudia kwa furaha kama kielelezo cha imani tendaji!
Wosia wake kwa mabinti wake
“Nanaomba muwakumbuke na kuwaweka katika akili na moyo mabinti zenu wote, mmoja baada ya mwingine. Na si tu majina yao, lakini pia hali zao, asili na hali na kila kitu kinachowahusu wao. Jambo ambalo halitakuwa gumu kwenu ikiwa mtawakumbatia kwa sadaka ya uchangamfu. Jiwekeni dhamana kwa upendo na kwa mkono wa upole na mtamu, sio kwa ukali, lakini katika kila kitu mnachotaka kupendekeza. Zaidi ya yote, jihadharini, msitake kupata chochote kwa kulazimisha, kwa sababu Mungu anampatia kila mtu uhuru wa kuchagua na hataki kulazimisha mtu yeyote, bali hupendekeza tu na kushauri. Nami ninawaambieni, mkisimama pamoja hivi nyote, mkiwa na umoja wa moyo, mtakuwa kama mwamba wenye nguvu sana na mnara usioweza kushindwa, juu ya dhiki zote na adha na madanganyo ya kishetani. Na pia ninawapatia uhakika kuwa kila neema mtakayomuomba Mungu mtapewa bila ya kukosa.”
Maono ya “ngazi ya mbinguni ikiunganisha dunia”
Na ni hasa wakati alikuwa akiomba Mtakatifu wa baadaye kwamba aliona maono ya maandamano ya Malaika na mabikira wakicheza na kuimba nyimbo. Miongoni mwao, Mtakatifu Angela pia alimwona hata dada yake aliyekufa na ambaye alitabiri hivi: “Utapata kundi la mabikira.” Katika karne zilizofuata maono hayo yalijionesha katika picha za wachoraji kwa mchoro wa Angela akitazama "ngazi ya mbinguni" inayounganisha “Mbingu na Dunia.”