Maaskofu Katoliki Uganda wahimiza kuimarishwa kwa familia
Na Christopher Kisekka – Kampala
Katika ujumbe wao Siku Kuu ya Kuzaliwa kwa Bwana wa 2024 uliotolewa na Askofu Anthony Joseph Zziwa, Askofu wa Jimbo la Kiyinda-Mityana na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Uganda (UEC), Maaskofu walizitaka familia kutafakari wajibu wao katika kukuza upendo, amani na utulivu, sambamba na kielelezo kilichotolewa na Familia Takatifu ya Nazareti.
Jenga na urekebishe vifungo vya familia wakati wa Noeli
Askofu Zziwa alisisitiza kwamba Noeli inatoa fursa ya kuishi tena fumbo la umwilisho wa Mungu, linalofananishwa na jina Emmanueli, linalomaanisha: “Mungu pamoja nasi” na kuimarisha vifungo vya familia vinavyoonesha uwepo huu wa kimungu. “Noeli ni wakati wa familia kutafakari juu ya mafundisho ya Kristo na kufanya upya kujitolea kwao kuunda nyumba zenye upendo na kusaidia," alibainisha.
Madhara ya teknolojia kwa familia
Hata hivyo, Maaskofu walikubali changamoto zinazoongezeka ambazo familia hukabiliana nazo katika jamii ya leo, ikiwa ni pamoja na gharama kubwa za maisha, shinikizo la elimu ya kisasa, na huduma duni za afya. Walionesha wasiwasi wao juu ya madhara ya teknolojia kwenye mienendo ya familia na kuongezeka kwa jeuri, kutelekezwa na wazazi, na kuvunjika kwa miundo ya familia. “Tunasikitishwa na kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaotelekezwa au kunyanyaswa, mara nyingi na wazazi waliokatishwa tamaa,” Askofu Zziwa alisema, akitaka hatua za pamoja zichukuliwe kurejesha utu wa familia, ikiwa ni pamoja na kaya za mzazi mmoja, na kuhakikisha kuwa haki za watoto zinalindwa. Maaskofu pia walisisitiza umuhimu wa msaada wa kiserikali kwa familia, wakihimiza utekelezwaji wa sheria zinazosimamia uadilifu wa ndoa na maisha ya familia. “Sheria lazima zipitishwe kulinda familia na kamwe zisipunguze maadili yake ya msingi,” walisisitiza, wakiakisi jukumu muhimu la sheria katika kudumisha utulivu wa kijamii.
Ombea nchi uponyaji
Pamoja na kujikita katika masuala ya kifamilia, Maaskofu walitoa wito wa kutafakari kwa kina kitaifa kuhusu changamoto za Uganda, kijamii na kiuchumi na kisiasa. Kutokana na ongezeko la ukosefu wa ajira, migawanyiko ya kisiasa na umaskini unaozidi kuongezeka, Maaskofu waliwataka Waganda wote kuiombea nchi hiyo uponyaji, wakihimiza kwamba “Noeli ni wakati mwafaka wa kukabidhi mahangaiko hayo kwa Mungu, kuomba mwongozo wa kuelekea kwenye amani, mafanikio na demokrasia zaidi.”
Kubali Mwaka wa Jubilei kwa upyaji wa kiroho
Maaskofu pia wamewakumbusha waamini kuhusu tamko la Baba Mtakatifu Francisko la mwaka 2025 kuwa ni Mwaka wa Jubilei, akiwataka Wakatoliki kukumbatia upyaisho wa kiroho na kuimarisha mahusiano kati yao na Mungu, wao kwa wao na dunia nzima. Mwishoni, Maaskofu walisisitiza ujumbe wao juu ya umuhimu wa familia kama msingi wa jamii, wakihimiza serikali na wananchi kulinda taasisi hii muhimu kwa manufaa ya taifa. Waliwatakia Waganda wote heri ya Noeli na Mwaka Mpya wa 2025, wenye mafanikio, wakitaka kuendelea kutafakari juu ya umuhimu wa familia katika mwaka ujao.