Hija ya Papa Francisko nchini Msumbiji:Sr.Olga amani bado ni dhaifu!
Na Sr. Angela Rwezaula- Vatican News
Mwanashirika la Mtakatifu Paulo Nchini Msumbiji, Sr Olga Massango, ambaye wakati wa Ziara ya Kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Msumbiji kati ya tarehe 16 na 19 Septemba 1988, alikuwa kijana mtawa na ambaye alihusishwa katika Tume ya maandalizi na kuandaa mahali pa kufikia, kutokana na uwezo wake wa lugha, kwa sababu ya kuzungumza lugha ya kireno, kifaransa, kisipanyola na kingereza. Na kwa mara nyingine tena hata katika ziara ya Baba Mtakatifu Francisko, Yeye amechaguliwa katika Tume ya maandalizi. Haya ni kwa mujibu wa maelezo ya Padre Paulo Samasumo, mwakilishi wa Vatican News, aliyeko nchini Msumbiji katika ziara hii ya Kitume ya Baba Mtakatifu akiambatana na wengine ambapo amehojiana naye ili kushirikishana uzoefu wake hasa wa kuwa na fursa ya kushiriki katika tume mbili ya kwanza na ya pili katika matukio ya ujio wa Papa.
Ziara ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini msumbiji 1988
Akifafanua juu ya mtazamo wake kuhusu ushiriki huo wa kamati mbili za maandalizi Sr. Olga Massango, anasema, kuna utofauti sana, kwani kunako mwaka 1988 Mtakatifu Yohane Paulo II alipokuwa nchini Msumbiji alikuta nchi yote ikiwa imejaa vita ya wenyewe kwa wenye. Serikali ilikuwa ya Kimarx au kikomunisti. Na wakati ule, Vatican ililazimika kuwa na uangalizi wa karibu kuhusu maandalizi hayo yaliyo kuwa yanaandaliwa na watu mahalia. Lakini kinyume na hiyo mandalizi ya mwaka huu, Sr Olga anathibitisha kwamba, tume ya maandalizi mahalia, imetambua nini inapaswa kufanya na kwa maana hiyo hapakuwapo na ulazima wa uangalizi wa karibu kwa upande wa Vatican. Na kama ilivyokuwa hija ya mtangulizi wake Mtakatifu Yohane Paulo II, hata Baba Mtakatifu Francisko sasa yupo nchini Msumbiji kwa ajili ya kuwatia moyo wa kuwa na matumaini, amani na kuishi kwa mapatano nchini Msumbiji.
Ziara ya Papa isaidie kuleta ushuhuda mzuri na mfano wa kuigwa nchini Msumbiji
Sr. Olga akiendelea kutazama kwa karibu ziara hii amesema kwamba, hata ziara ya Baba Mtakatifu Francisko ni ya lazima, kwa sababu amani nchini Msumbiji bado ni dhaifu. Iwapo nchini Msubiji watu wataweza kushinda kwa ajili ya amani, nchi itakuwa na ushuhuda mzuri kwa ajili ya nchi nyingie za Afrika kama vile Sudan ya Kusini, amethibitisha Sr. Olga. Aidha Sr, Olga ameshirikisha hata juu ya matarajio yake kabla ya mchana wa siku Alhamisi ya tarehe 5 Septemba 2019, mahali ambapo ratiba ya Baba Mtakatifu Francisko ilikuwa ni kukutana na watawa, waseminari na mapadre wa Msumbiji. Kutokana na hili amesema ni matarajio ya kwamba Baba Mtakatifu Francisko anaweza kuwatia moyo hasa watawa ili wasiache utume wa uinjilishaji hata kama wanapata na taaluma za juu kama za ualimu au udaktari. Kwa upande wa mkutano na vijana na Baba Mtakatifu ni matarajio ya Sr Olga juu ya umuhimu wa vijana kwa ajili ya Ekolojia.
Padre Bernardo Suate:ni furaha na chereko kubwa zinazoonekana nchini Msumbiji
Naye Padre Bernardo Suate, mwakilishi wa Vatican News nchini Msumbiji, katika ziara ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa kuzungumza moja kwa moja na waandishi wa habari Vatican akiwa Msumbiji asubuhi tarehe 5 Septemba 2019, ameelezea kile kinachojiri nchini Msumbiji katika fursa ya ujio wa Baba Mtakatifu tangu alipowasiri katika uwanja wa Maputo tarehe 4 Septemba 2019. Kwa hakika amethibitisha kuwa, ni furaha kwa watu wote, bila kujali dini yoyote. Na zaidi hata katika Luninga ya kitaifa inalezea habari za Baba Mtakatifu katika kipindi hiki cha kihistoria. Kadhalika akifafanua hata juu ya magazeti ndani ya nchi Padre Suate anasema kuwa , karibu ni mahgazeti yote yametoa kipaumbele cha hija ya Baba Mtakatifu Francisko. Hata hivyo amefurahishwa na habari moja ndani ya gazeti kuhusu bibi mmoja mzee ambaye siyo mkatoliki na wala mkristo kuthibitisha kwamba, hataki hakose tukio lolote linaloendelea kuhusu Baba Mtakatifu Francisko nchini humo.