Utapiamlo:kijana wa Gaza wa miaka 20 afariki baada ya kuwasili Italiwa kwa matibabu
Vatican News
Mwathiriwa wa njaa na utapiamlo, Marah Abu Zuhri, mwanamke wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 20 ambaye aliwasili Italia kutoka Ukanda wa Gaza kupata huduma ya matibabu kama sehemu ya operesheni ya kibinadamu, alifariki dunia katika kitengo cha damu cha Hospitali ya Pisa nchini Italia. Alishuka kwa ndege ya serikali ya Italia wakati wa usiku kati ya Agosti 13 na 14 na mara moja alilazwa hospitalini, lakini hali yake mara moja ilionekana kuwa mbaya kwa sababu ya utapiamlo.
Mwanamke huyo kijana alikuwa amewasili Italia, akifuatana na mama yake, kama sehemu ya operesheni ya kibinadamu, na matokeo ya vipimo kuonesha kuathirika sana na kuzorota kwa kiasi kikubwa, kwa mujibu wa maelezo ya Hospitali ya Chuo Kikuu cha Pisa. Siku ya tarehe 15 Agosti 2025, baada ya vipimo muhimu vya awali kufanywa na tiba ya kuunga mkono ilianzishwa, alipata shida ya kupumua kwa ghafla na mshtuko wa moyo uliofuata, ambao, kwa bahati mbaya, ulisababisha kifo cha mwanamke huyo kijana.
Wapalestina 1,760 waliuawa wakitafuta msaada tangu Mei
Wakati huo huo, takriban Wapalestina tisa wameuawa na wengine kujeruhiwa, wakati wa mashambulizi ya Israel kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, katika eneo la kusambaza misaada. Shirika la habari la Palestina "Wafa" liliripoti hili, likinukuu vyanzo vya ndani. Zaidi ya Wapalestina 1,760 wameuawa katika Ukanda huo tangu mwishoni mwa Mei, wengi wao chini ya moto wa jeshi la Israel, walipokuwa wakitafuta msaada wa kibinadamu."
Hayo yameripotiwa na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa katika maeneo ya Palestina. Kati ya Mei 27 na Agosti 13, Kamishna Mkuu alirekodi angalau "Wapalestina 994 waliuawa walipokuwa wakitafuta msaada karibu na maeneo yanayosimamiwa na Msaada wa Kibinadamu wa Gaza (GHF) na 766 kwenye njia za msafara wa usambazaji," ilisema katika taarifa. "Mauaji mengi haya yalifanywa na jeshi la Israel," shirika la Umoja wa Mataifa linadai.