Vita kati ya Israeli na Iran: Mauaji Yanatisha!
Na Sarah Pelaji, - Vatican.
Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari (CPJ) imesema kuwa "imeshtushwa" na shambulio la Israel dhidi ya studio ya Kituo cha Televisheni ya Serikali ya Iran mjini Tehran mnamo tarehe 16 Juni 2025. CPJ imeshtushwa na bomu la Israel dhidi ya Kituo cha Televisheni ya Serikali ya Iran wakati waandishi wa habari wakiwa wakirusha matangazo mubashara. Pia Shirika hilo limesema Israeli mpaka sasa imeua waandishi wa habari takribani 185 huko Gaza bila kuwajibishwa jambo ambalo limeipatia Israeli ujasiri wa kushambulia vyombo vya habari katika maeneo mengine ya Iran. Hivyo imesema umwagaji huo wa damu lazima ukome sasa,” aliongeza.
Shambulio la Israel dhidi ya Studio ya Kituo cha Televisheni cha IRINN lilikatiza matangazo ya moja kwa moja yaliyokuwa yakitolewa na mtangazaji Sahar Imani, ambaye alikuwa anaripoti kuhusu mashambulizi yanayoendelea dhidi ya Iran. “Sikilizeni, sauti ya mshindo mnayoisikia ni sauti ya shambilizi,” alisema Imani hewani kabla ya shambulio kutokea kwa mujibu wa taarifa ya CPJ. Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali ya Iran, IRNA, inakadiriwa kuwa, watu wawili waliuawa katika shambulio hilo. Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, alisema kuwa “mamlaka ya utangazaji ya propaganda na uchochezi ya utawala wa Iran” ilishambuliwa na jeshi la Israel baada ya kutoa agizo la kuwaondoa wakazi katika eneo linalozunguka studio hiyo. Effie Defrin, Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF), alisema kuwa studio hiyo “ilijificha kama Shirika la utangazaji” lakini ilikuwa inatawaliwa na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) cha jeshi la Iran. Kituo hicho kinatumiwa na jeshi la Iran kusambaza propaganda dhidi ya Israel huku kikitoa wito wa mauaji ya halaiki,” alidai Defrin.