Trump atia saini ya marufuku kuwazuia raia wa nchi 12 kuingia Marekani!
Na Sarah Pelaji – Vatican.
Tarehe 4 Juni 2025, Rais Donald Trump wa Marekani alitia saini ya kuwazuia raia kutoka nchi 12 duniani kuingia Marekani huku akisema ni kwa sababu za usalama wa raia wake wa taifa la Marekani, dhidi ya vitisho. Katika taarifa iliytolewa na Ikulu ya (White House) Bwana Trump alisema utekelezaji wa marufuku hiyo utaanza tarehe 9 Juni 2025. Nchi zilizoorodeshwa ni Afghanistan, Myanmar, Chad, Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Guinea ya Ikweta, Eritrea, Haiti, Iran, Libya, Somalia, Sudan na Yemen. Mataifa mengine saba ambayo raia wake wamewekewa vikwazo vya usafitri ni pamoja na Burundi, Cuba, Laos, Sierra Leone, Togo, Turkmenistan na Venezuela.
Sababu za marufuku na masharti
Agizo hilo ni sehemu ya msako mkali wa wahamiaji uliozinduliwa na Bwana Trump mwaka huu mwanzoni mwa muhula wake wa pili, ambao pia umehusisha kuwarejesha El Salvador mamia ya raia wa Venezuela wanaoshukiwa kuwa wanachama wa magenge ya uhalifu pamoja na juhudi za kukataa usajili wa baadhi ya wanafunzi wa kigeni na huku wengine wakirudishwa makwao.
Bwana Trump alisema kwamba nchi zilizowekewa masharti makali zaidi zilichaguliwa kwa sababu zinadaiwa kuwa na uwepo mkubwa wa magaidi, kushindwa kushirikiana katika usalama wa visa na kutokuwa na uwezo wa kuthibitisha utambulisho wa wasafiri, kuwa na rekodi duni za kihalifu na viwango vya juu vya watu wanaokaa Marekani zaidi ya muda wa visa zao. "Hatuwezi kuwa na mipaka iliyo wazi inayoruhusu wahamiani kutoka kwa nchi yoyote kuingia Marekani. Lazima kuwakagua tujiridhishe ili kuwa na usalama wa uhakika wa wale wanaotaka kuingia Marekani," alisema Trump.
Marufuku hiyo yakosolewa
Hata hivyo hatua hiyo ya Trump imepingwa na mataifa yaliyoathiriwa ikiwemo Venezuela ambayo ni mojawapo ya nchi saba zilizoathiriwa na vikwazo vya marekani katika maeneo kadhaa. Waziri wa Mambo ya Ndani Diosdado Cabello ameonya kuwa "kuwa nchini Marekani ni hatari kwa raia wa mataifa mbalimbali na si kwa raia wa Venezuela pekee. Ameshutumu utawala wa Marekani wa sasa akisema watawala wake ni ni watu wabaya wenye itikadi kali ambao wanadhani wanamiliki dunia na kuwatesa watu bila sababu. Wakati huo huo, Somalia ambayo raia wake wapigwa marufuku kuingia Marekani imeahidi kufanya kazi na Marekani kushughulikia masuala ya usalama.Balozi wa Somalia nchini Marekani, Dahir Hassan Abdi, anasema nchi yake inathamini uhusiano wake wa muda mrefu na Marekani.
Hata hivyo Bwana Trump amesema orodha hiyo inaweza kutathminiwa upya endapo maboresho ya msingi yatafanywa basi nchi zaidi zinaweza kuongezwa huku uamuzi huo ukiibua wasiwasi kwa mataifa mengi ulimwenguni. Hii ni mara ya pili kwa rais huyo kuamuru marufuku dhidi ya raia wa nchi tofauti. Alitia saini agizo kama hilo mnamo 2017, wakati wa muhula wake wa kwanza ofisini. Marufuku hiyo itaanza kutekelezwa Jumatatu ijayo ili kuzuia msongamano wa wasafiri katika viwanja vya ndege vya Marekani kama ilivyoshuhudiwa miaka minane iliyopita hatua sawa na hiyo ilipochukuliwa na utawala wa Trump.
Kwa nini marufuku imetangazwa?
Ikulu ya ya Marekani (White House) ilisema kuwa hivyo ni vikwazo vya kawaida ambavyo vinalenga kuwalinda raia wa Marekani dhidi ya vitisho kutoka nje. Bwana Trump alitangaza marufuku ya awali wakati wa muhula wake wa kwanza alipoingia madarakani mwaka 2017. Yapo mataifa ambayo ambayo raia wake walipigwa marufuku kuingia marekani mwaka 2017 na sasa yamejumuishwa tena katika marufuku ya sasa. Mataifa hayo ni pamoja na Iran, Libya na Somalia.
Wakosoaji wanaitaja marufuku hiyo ya Marekani kuwa inalenga nchi zenye waumini wengi wa dini ya kiislamu . Wakati hayo yakiendelea mwaka 2017 White House ilifanyia marekebisho sera hiyo, na kuongeza nchi ya Korea Kaskazini na Venezuela. Amri hiyo ilipitishwa na mahakama ya juu zaidi mwaka 2018. Rais Joe Biden, ambaye alimrithi Trump, alifuta marufuku hiyo mnamo 2021, na kuiita doa kwenye dhamiri ya kitaifa la Marekani. Na Sasa Trump amesimamia msimamo wake akisema analilinda taifa la Marekani dhidi ya vitisho vya nje.