杏MAP导航

Tafuta

Wapalestina wanasheherekea tangazo la kusitisha mapigano wakati ukanda mzima umejaa magofu, majeruhi na vifo. Wapalestina wanasheherekea tangazo la kusitisha mapigano wakati ukanda mzima umejaa magofu, majeruhi na vifo.  (AFP or licensors)

Makubaliano yatangazwa ya kusitisha mapigano Gaza,baada ya karibu siku 470 za vita

Tangu vita kuanza huko Gaza,inasadikika watu 46,700,walikufa katika Ukanda huo ambapo imetangaza kuwepo kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.Trump,Umoja wa Ulaya(UE),Katibu wa Umoja wa Mataifa,Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina(UNRWA),Mratibu mkuu wa misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura wa Umoja wa Mataifa(OCHA)na UNICEF wamekaribisha tangazo hilo.

Na Angella Rwezaula -Vatican.

Makubaliano ya kusitisha uhasama na kuachiliwa kwa mateka huko ukanda wa Gaza, utaanza Dominika tarehe 19 Januari 2025, huku Hamas ikitarajiwa kuanza kuwaachilia mateka 33 wa moja kwa moja. Makubaliano haya yalitangazwa kusitisha mapigano Gaza, baada ya karibu siku 470 za vita na vifo vya watu 46,700. Makubaliano hayo yatathibitishwa 16 Januari 2025 na Serikali ya Israel, lakini waziri wa siasa kali za mrengo wa kulia Smotrich tayari ametangaza kura yake dhidi yake. Mara baada ya Tangazo hilo viongozi wa ulimwengu walikaribisha tangazo hilo. Waziri Mkuu wa Qatar Mohammed Al Thani alithibitisha kuachiliwa kwa mateka 33 wa Israel katika awamu ya kwanza ya usitishaji vita huko Gaza. Waliotekwa nyara mnamo Oktoba 7, wanaweza kurejea wakiwa hai kwa familia zao. Vita vya Israel dhidi ya Hamas huko Gaza vilianza tangu tarehe 7 Oktoba 2023, wakati wanamgambo hao walivamia kusini mwa Israel na kuua takriban watu 1,200 na kuwateka nyara takriban 250.

Maoni ya Trump

Hata hivyo tangazo la Donald  Trump kwamba makubaliano yamefikiwa yaliweka kila mtu kuwa na furaha. Na  anajisifu kwa kukamilisha kile anachokiita "mpango wa kipekee. Hakuna magaidi tena huko Gaza," rais mteule alitangaza, kwamba "tutapanua Makubaliano ya Abraham." Utawala wa Biden hauna budi ila kuthibitisha makubaliano yaliyofikiwa, wakati maelfu ya watu tayari wanasherehekea usitishaji vita kote Gaza.

Makubaliano hayo yawe msingi wa utulivu wa kudumu, UE

Miongoni mwa maoni ya kwanza ya kitaasisi, ni yale ya Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen, ambaye anakumbuka kwamba misaada yakibinadamu sasa itaweza kuwafikia raia wa Gaza. Alisisitiza kuwa sasa “pande zote mbili lazima zitekeleze kikamilifu makubaliano haya, kama hatua ya kuelekea utulivu wa kudumu katika kanda na utatuzi wa kidiplomasia wa mzozo.”

Sherehe huko Gaza

Zinasikika honi kila pembe, kucheza na bendera za Palestina zilisalimia tangazo lililokuwa likisubiriwa kwa muda mrefu la makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza. Familia zinazungumza juu ya ukosefu wa chakula, milipuko ya mabomu, vifo, vifusi, woga, na kutokuwa na hakika kila wakati, mazungumzo yakishindwa tena na tena. Sasa hamu kubwa zaidi ni kutozungumza tena juu ya wahasiriwa kila siku, kujisikia salama. Kila mtu anazungumza juu ya kurudi nyumbani, wengi wanaripoti kwa kukurupuka, ingawa imeharibiwa. Lakini kwa sasa unafuu unazidi wasiwasi.

Katibu Mkuu wa UN alikaribisha makubaliano

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alikaribisha tangazo la makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka Gaza, akiyataja makubaliano hayo kuwa ni hatua muhimu kuelekea kupunguza janga la kibinadamu katika eneo hilo. Katika taarifa aliyoitoa tarehe 15 Januari 2025  mjini New York Marekani,Bwana  Guterres amezipongeza nchi za Misri, Qatar, na Marekani kwa jukumu lao muhimu kama wapatanishi katika kufanikisha makubaliano hayo. Bwana Guterres alisema:“Juhudi zao za dhati za kutafuta suluhu ya kidiplomasia zimekuwa muhimu katika kufanikisha mafanikio haya.” Katibu Mkuu alisisitiza wito wake wa muda mrefu wa kusitisha mapigano mara moja na kuachiliwa kwa mateka bila masharti yoyote, huku akisisitiza umuhimu wa kutekelezwa kikamilifu kwa makubaliano hayo. Aliongeza kuwa: “Kipaumbele chetu ni kupunguza mateso makubwa yanayosababishwa na mgogoro huu.” Katibu Mkuu aliahidi kwamba Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia utekelezaji wa makubaliano hayo na kuongeza juhudi za kibinadamu ili kukabiliana na mahitaji makubwa ya watu walioathirika.

Janga la kibinadamu Gaza limefikia pabaya hatua za haraka zahitajika

Hali ya kibinadamu Gaza imefikia viwango vya janga, huku vikwazo vikubwa vya kiusalama na kisiasa vikizuia juhudi za kufikisha misaada. Katibu Mkuu Guterres alisisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo hivi ili kuwezesha ongezeko kubwa la msaada wa kuokoa maisha kuingia Gaza. “Ninatoa wito kwa pande zote kuwezesha misaada ya kibinadamu kwa haraka, bila vizuizi, na kwa usalama kwa raia wote wanaohitaji,” aliongeza. Ingawa kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka kunachukuliwa kama hatua muhimu ya awali, Bwana Guterres alisisitiza umuhimu wa kushughulikia malengo makubwa zaidi ya kisiasa. Amebainisha hitaji la umoja wa Wapalestina na harakati za kufanikisha suluhu ya mataifa mawili kupitia mazungumzo, suluhisho ambayo itahakikisha amani na usalama kwa Waisraeli na Wapalestina. Bwana Guterres alisema: “Kumaliza uvamizi na kufanikisha suluhisho lenye uhai la mataifa mawili, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, maazimio husika ya Umoja wa Mataifa, na makubaliano ya awali, bado ni kipaumbele cha dharura.”

Daima tutawaenzi waliopoteza maisha Gaza

Alihitimisha taarifa yake kwa kuwaenzi kwa heshima raia, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, na wahudumu wa kibinadamu waliopoteza maisha yao katika mzozo huo. Guterres alithibitisha tena ahadi ya Umoja wa Mataifa ya kuendeleza juhudi za kukuza amani, utulivu, na mustakabali mzuri kwa eneo hilo. Tangazo la makubaliano haya ya amani linakuja wakati kukiwa na miito ya kimataifa inayozidi kuongezeka ya kupunguza mzozo na kutoa misaada ya kibinadamu Gaza. Jumuiya ya kimataifa sasa inatarajia pande zinazohusika kuheshimu ahadi zao na kufanya kazi kuelekea suluhisho la kudumu la mzozo huu wa muda mrefu.

Kauli za mashirika ya UN baada ya tangazo la usitishaji mapigano Gaza

Ma baada ya tangazo hilo la usitishwaji uhasama kutolewa mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa yametoa kauli.

Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA

Kwa upande wa Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema: “Tangazo la kusitisha mapigano linakuja wakati sheria mbili za Israeli zinazolenga kusitisha shughuli za UNRWA katika eneo la Palestina linalokaliwa zinatarajiwa kuanza kutekelezwa katika kipindi cha wiki chache zijazo.” Shirika hilo limesema Gaza ina idadi ya watu zaidi ya milioni mbili, ambapo milioni 1.9 tayari wamepoteza makazi yao, na mamia kwa maelfu wanapata katika shule zetu zilizogeuzwa kuwa makazi ya muda. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amerejelea kusema mara kadhaa kwamba UNRWA ni “Uti wa mgongo wa juhudi za misaada katika eneo hilo. Shirika hilo limekumbwa na hasara kubwa, huku wafanyakazi wake 265 wakiuawa na miundombinu yake kushambuliwa.” Kamishna Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini leo wakati wa mkutano mjini Oslo uliolenga suluhy ya mataifa mawili amesema “Kuanguka kwa shirika hili  iwe ni mara moja au polepole kutazidisha tu mateso makubwa katika Ukanda wa Gaza.”

Sitisho la mapigano Gaza ni tumaini lakini kuna changamoto: OCHA

Taarifa kutoka kwa mratibu mkuu wa Misaada ya Kibinadamu na Masuala ya Dharura wa Umoja wa Mataifa,  Tom Fletcher, inasema kuwa "Sitisho la mapigano lililokubaliwa leo kati ya Israel na Hamas linatoa tumaini linalohitajika sana kwa mamilioni ya watu ambao maisha yao yameharibiwa na mzozo huu. Ninalipongeza makubaliano haya na kusihi pande zote kuyaheshimu." Katika taarifa hiyo aliongeza kusema kuwa "mashirika ya kibinadamu yameanza kuandaa vifaa vya msaada ili kuongeza utoaji wa misaada huko Gaza, ambako Wapalestina wamepitia zaidi ya miezi 15 ya mateso, uharibifu, na kwa zaidi ya watu 46,000 vifo. Pia, makumi ya mateka wa Kiyahudi bado wanashikiliwa. Tutafanya kila tuwezalo kukabilina na hali kwa juhudi, ubunifu, na haraka inayohitajika katika wakati huu, licha ya changamoto kubwa za kiusalama na kisiasa zinazotukabili.  Fletcher amesisitiza kuwa “Ili tuokoe maisha, tunasisitiza pande zote kuheshimu kikamilifu sheria za kimataifa za kibinadamu. Hii inamaanisha kulinda raia na miundombinu ya kiraia, kuruhusu wafanyakazi wa misaada kufika salama na bila vizuizi kwa watu wenye mahitaji, popote walipo, na kuondoa vizuizi vyote kwa upatikanaji wa misaada muhimu.” Pia ni muhimu kuwezesha kuingia kwa bidhaa za kibiashara amesema akiongeza kwamba  Tunatoa wito kwa Baraza la Usalama kutumia sauti na ushawishi wake kuhakikisha sitisho la mapigano linadumishwa, sheria za kimataifa zinaheshimiwa, na vizuizi vya kuokoa maisha vinaondolewa. Ameendelea kusema: “Tunasihi nchi wanachama kuhakikisha kuwa operesheni zetu za kibinadamu zinafadhiliwa ipasavyo ili kukidhi mahitaji makubwa yaliyo mbele yetu.Tunatoa wito pia wa uwajibikaji kwa ukatili uliofanywa. Huu ni wakati wa tumaini na fursa, lakini tusidanganyike na ugumu wa kazi ya kuwafikia manusura. Hali ni tete, na umuhimu wake hauwezi kupuuzwa.”

Sitisho la mapigano ni tumaini kwa watoto na familia: UNICEF

Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF, inakaribisha sitisho la mapigano katika Ukanda wa Gaza, likisema linaleta matumaini kwa watoto na familia ambao wamepitia zaidi ya mwaka mmoja wa maangamizi. Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF, Bi Catheine Russell alisema "Mzozo huu umesababisha vifo vya watoto wasiopungua 14,500, majeruhi kwa maelfu, karibu watu milioni moja kukosa makazi, na watoto 17,000 kuachwa bila mzazi au kutenganishwa na wazazi wao. Ameongeza kuwa huduma muhimu zimeporomoka, huku chini ya nusu ya hospitali za Gaza zikiwa zinafanya kazi kwa kiasi, uzalishaji wa maji ukiwa katika asilimia 25 pekee, na uhaba mkubwa wa chakula ukiathiri karibu watu wote milioni 2.1."

Mkuu huyo alisisitiza kuwa “UNICEF iko tayari kuongeza juhudi zake, ikizingatia umuhimu wa kuhakikisha upatikanaji wa chakula, huduma za afya, maji safi, elimu, na msaada wa kisaikolojia bila vizuizi. Sitisho hili la mapigano linapaswa kuwezesha operesheni za kibinadamu kuwa salama na juhudi za haraka za kurejesha hali ya kawaida, ikijumuisha matibabu ya utapiamlo, chanjo kwa watoto 420,000 walio chini ya miaka mitano, na kuzuia mlipuko wa magonjwa.” UNICEF imesisitiza umuhimu wa kuheshimu sitisho hilo la mapigano na imetoa wito wa suluhisho la kisiasa la kudumu ili kuhakikisha maisha bora ya baadaye kwa watoto wa Gaza, ambao tayari wameumia sana.

Kusitisha mapigano Gaza
16 Januari 2025, 10:07