Rais Samia Suluhu Hassan Ameiwakilisha Vyema Tanzania UN
Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Mwanga, Kilimanjaro, Tanzania.
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameiwakilisha vyema Tanzania alipohutubia Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Jijini New York, Marekani. Amesema kuwa Rais Mheshimiwa Samia ametoa ujumbe maalum ambao Tanzania ulitaka Mataifa mengine yasikie na kuiunga mkono kwenye mipango yake ya maendeleo. Mheshimiwa Majaliwa ametoa kauli hiyo Ijumaa Septemba 24, 2021 baada ya kukagua maendeleo ya mradi mkubwa wa maji wa Mwanga-Same, Wilayani Mwanga, Kilimanjaro. Waziri Mkuu ameongeza kuwa hotuba hiyo pia imeyaonesha Mataifa mengine duniani kile Tanzania inakifanya kina lengo la kuwapelekea wananchi wake maendeleo. “Mheshimiwa Rais ametumia mkutano huo kukaribisha Mataifa rafiki yenye nia njema ya kuja Tanzania kuwekeza waje. Wito wake huo una manufaa makubwa kwetu”. Akizungumza kuhusu mradi wa Maji wa Mwanga-Same ambao utahudumia wananchi wapatao 438,931, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Nishati kuhakikisha inatengeneza mfumo kwa haraka ili kusukukuma maji kutoka kwenye mashine na maji yaanze kusafirishwa”.
Pia Waziri Mkuu amemtaka mkandarasi anayejenga mradi huo kumaliza majadiliano na Wizara ya Maji na kukubaliana jambo la kufanya ili kuhakikisha wanaukamilisha mradi huo kwa muda uliopangwa na wananchi waanze kupata huduma ya maji. Aliongeza kuwa, Rais Mheshimiwa Samia amedhamiria kuhakikisha kampeni yake ya kumtua mama ndoo kichwani inatekelezwa kwa vitendo. “Kampeni hii itawawezesha wananchi kupata maji kwa ukaribu.” Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi katika eneo la Ngangamfumuni, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro. Amesema mradi huo ni wa kimkakati kwani mkoa wa Kilimanjaro upo mpakani hivyo uwepo wa kituo cha mabasi cha kisasa utatoa fursa kwa wakazi wa mkoa huo kufanya biashara kwa kuwa utapokea mabasi kutoka nchi za jirani ikiwemo Kenya. Ameyasema hayo Alhamisi, Septemba 23, 2021 wakati akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Manispaa Moshi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa kituo hicho akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa serikali katika mkoa huo.
“Hiki ni kituo cha mabasi chenye hadhi ya kimataifa, mkoa huu unapokea watalii wengi kutoka katika maeneo mbalimbali, hivyo ujenzi wa hoteli katika kituo hiki utasaidia kuongeza fursa za biashara kwa wakazi wa hapa.” Naye, Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Rashidi Gembe amesema mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 28.86 unatekelezwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa jengo la abiria lenye ukubwa wa mita 13,979 ikijumuisha sakafu ya chini ya ardhi na ghorofa mbili kwa gharama ya shilingi bilioni 17.9. “Awamu ya pili itahusisha ujenzi wa jengo la hoteli lenye ghorofa nne kwa gharama ya shilingi bilioni 11.40. Mradi huu utakapokamilika unatarajiwa kuiongezea Halmashauri wastani wa mapato ya shilingi bilioni 2.72 kwa mwaka kutokana na makusanyo ya ushuru na kodi zitakazokusanywa.” Baada ya kuweka jiwe la msingi katika kituo hicho, Mheshimiwa Majaliwa alikagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Tella Mande uliopo Moshi vijijini ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wa kufikisha huduma ya maji vijijini.
Akizungumza na wananchi hao, Waziri Mkuu aliwataka wakazi hao wahakikishe wanaulinda mradi huo ili uendelee kuwapa uhakika wa upatikanaji wa maji wakati wote pamoja na kuendelea kuvitunza vyanzo vyote vya maji. Akiongea na wakazi wa Himo, Waziri Mkuu amesema kuwa Rais Mheshimiwa Samia amedhamiria kuwekeza katika elimu ya mtoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao “vijana nawapa tahadhari ukijulikana umempa mtoto wa kike mimba, sheria kali zitachukuliwa dhidi yako.” Pia aliwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ipo makini na itaendelea kuwatumikia hivyo kila mwananchi katika nafasi yake afanye kazi kwa bidii ili waweze kujiletea maendeleo.