Vatican:Kozi za malezi ya Maaskofu wapya zinaanza,Roma Septemba 3-11
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Hata kwa mwaka 2025, toleo la Mafunzo ya Malezi kwa Maaskofu ambao kwa mujibu wa Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari Fides, limebainisha kuwa watakuwa 192 linafunguliwa tarehe 3 Septemba hadi tarehe 11 Septemba 2025. Miongoni mwa Maaskofu hao kama kawaida ni kutoka mabara yote matano na ambao waliteuliwa hivi karibuni (karibu wote waliowekwa wakfu katika mwaka uliopita) na watashiriki katika masomo ya malezi yaliyoandaliwa kwa ajili yao na Mabaraza mbalimbali ya Vatican. Kozi za Malezi kwa Maaskofu walioteuliwa hivi karibuni ni "tukio la Septemba" ambalo sasa limekuwa sehemu ya kawaida ya shughuli za Curia Romana. Mwaka huu, kwa kuthibitisha muundo mpya wa Kozi zilizoanzishwa mwaka 2024, vikao vya kazi siku ya Jumatatu, tarehe 8 Septemba na Jumanne, Septemba 9 vitaandaliwa katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana na vitahusisha ushiriki wa pamoja wa Maaskofu wote wa sehemu mbili walioandikishwa katika Kozi iliyoandaliwa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji (Sehemu ya Uinjilishaji wa Kwanza na Ushiriki wa Maaskofu wapya) na Kozi iliyoandaliwa na Baraza la Kipapa la Maaskofu(kwa hiyo ni sehemu mbili za kozi hiyo).
Maaskofu 78 wamejiandikisha katika Kozi ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji, wakati huku maaskofu 114 wakishiriki katika Kozi iliyoandaliwa na Baraza la Kipapa Maaskofu. Miongoni mwa hao wa mwisho ni maaskofu watano kutoka Makanisa Katoliki ya Mashariki (ambao wana Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki kama marejeo yao) na maaskofu watano waliowekwa wakfu hivi karibuni ambao wana Nyadhifa katika Curia Romana. Mfumo mpya wa Kozi, unaojumuisha vikao vya kazi vilivyoshirikishwa na maaskofu wote walioteuliwa hivi karibuni kutoka duniani kote, ulizinduliwa na kujaribiwa mwaka 2024 kama ishara na tafakari ya ushirika unaokumbatia na kuunganisha Kanisa la kiulimwengu na kama wakati wa ushirikiano, kuelewana, na uwezekano wa kujenga uhusiano kati ya Makanisa mbalimbali mahalia
Ili kuwa wachungaji wenye mizizi ndani ya Kristo, uhusiano wa kiroho wenye nguvu na Bwana ni muhimu: kila Askofu lazima kwanza azungumze na Mungu, kisha kusema juu ya Mungu kwa wengine; ili kuliongoza kundi kwenye malisho ya uzima, mchungaji anapaswa kwanza kujilisha mwenyewe kwa Mkate wa Uzima. Haya yamesemwa katika utangulizi wa Kitabu cha "Pastori di Cristo per una Chiesa Sinodale" yaani Mchungaji kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi”(LEV, 2024), ambacho kinakusanya mawasilisho na mahubiri yaliyotolewa wakati wa kozi za kila mwaka za malezi kwa Maaskofu wapya zilizofanyika mwaka 2024. Dibaji hiyo imetiwa saini na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwezi wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji na Kardinali Robert Francis Prevost, ambaye wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maaskofu ambaye sasa ni Papa Leo XIV.
Katika siku nyingine za kozi, makundi mawili ya maaskofu watasikiliza mawasilisho na kushiriki katika mijadala, vikundi vya kazi, na nyakati za kushirikishana zinazolenga masuala mahususi katika maeneo mawili tofauti: kozi iliyoandaliwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Uinjilishaji, yenye kichwa: "Kufungua Njia ya Matumaini; Kuitwa kwa Uaskofu katika Muktadha wa Jubilei," itakayofanyika katika Chuo cha Kipapa cha Mtakatifu Petro, wakati kozi iliyoandaliwa na Baraza la Maaskofu itfanyika katika Chuo cha Kipapa cha Mtakatifu Paulo.
Kozi ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji
Kozi ya mafunzo kwa Maaskofu wapya, iliyoandaliwa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji (Sehemu ya Uinjilishaji wa Kwanza na Makanisa Mahalia ), itaanza asubuhi ya Alhamisi, tarehe 4 Septemba 2025 kwa hotuba ya Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle Mwenyekiti na Askofu Mkuu Fortunatus Nwachukwu, Katibu Mkuu wa Baraza hilo. Siku ya Alhamisi mchana, Maaskofu watasikiliza wasilisho la Askofu Mkuu Rino Fisichella, Msimamizi Mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa (Sehemu ya Masuala ya Msingi na Uinjilishaji Ulimwenguni). Kipindi cha Ijumaa, Septemba 5, kitazingatia mahitaji ya haraka ya utamaduni, kitawasilishwa na Askofu Mkuu Nwachukwu (“Ushiriki wa Kikabila katika Huduma kwa Kanisa”),Askofu Aurelio Garcia Macias, Katibu Msaidizi wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Ibada na Nidhamu ya Kisakramenti ahafafanua kuhusu “Utamadunisho wa Liturujia Leo hii” na kwa upande wa Askofu Mkuu Flavio Pace na Askofu Usma Gomez Juan Fernando, Katibu na Mkuu wa Ofisi, kwa mtiririko huo, wa Baraza la Kuhamasisha Umoja wa Kikristo, ambaye atashughulikia "Changamoto ya Upentekoste."
Jumamosi tarehe 6 Septemba siku itaanza kwa Maaskofu kwa njia ya Msalaba kuelekea Mlango Mtakatifu, Misa ya Jubilei, na kuheshimu masalia ya Mtume katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Vikao vya kazi vifuatavyo vitazingatia mawasilisho ya Askofu Mkuu Juan Ignacio Arrieta, Katibu wa Baraza la kipapa kwa ajili ya Maandiko ya Sheria ("Askofu kama Jaji"), na Askofu Mkuu John Joseph Kennedy, Katibu wa Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa wa Baraza la Kipapa Mafundisho Tanzu ya Kanisa atajikita na:Kushughulikia Kesi Kuhusu 'Delicta Graviora'" yaana masuala mazito/nyeti). Alasiri, Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la kipapa la Walei, Familia, na Maisha, pamoja na Dk Linda Ghisoni na Dk Gabriella Gambino, Makatibu Wadogo wa Baraza hilohilo, watatoa mawasilisho kuhusu mada "Walei, Familia, na Maisha: Usindikizaji na Malezi katika Huduma ya Kichungaji ya Watu wa Mungu."
Maaskofu watashiriki Misa ya Kutangazwa wenyeheri Carlo Acutis na Pier Giorgio Frassati kuwa watakatifu
Dominika tarehe 7 Septemba 2025 Maaskofu wote waliokusanyika mjini Roma kwa ajili ya kozi za mafunzo watashiriki Ibada ya Misa Takatifu ya Kutangazwa Watakatifu kwa Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati na Carlo Acutis katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Kushirikishana vipindi
Siku zitakazotumiwa pamoja na Maaskofu wote wapya zitaanza Jumatatu, tarehe 8 Septemba, kwa maadhimisho ya Ekaristi yataongozwa na Kardinali Christoph Schönborn katika Kanisa kuu la Mtakatifu Maria Mkuu (Santa Maria Maggiore. Kisha, Askofu Mkuu Mstaafu wa Vienna atatoa mada kuhusu: “Huduma ya Maaskofu kama shuhuda na utangazaji wa matumaini yaliyosimikwa katika Kristo” ili kufungua vikao vya kazi vinavyoandaliwa katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbanana.
Jumatatu alasiri, mdahalo wa Maaskofu katika Ukumbu Mkuu wa Urbaniana utaanza kwa kuwasilishwa na Kardinali Fabio Baggio, Katibu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu, yenye mada: "Matumaini na Mateso - Jambo la Uhamiaji."
Jumanne, Septemba 9: athari za safari ya sinodi kwenye miundo, maisha, na uongozi wa jumuiya za kijimbo zitaainishwa katika mawasilisho na Kardinali Sérgio da Rocha, Askofu Mkuu wa Sao Salvador de Bahia, na Kardinali Fridolin Ambongo Besungu, Askofu Mkuu wa Kinshasa, Congo DR. Mawasilisho yatafuatiwa na majadiliano ya kina katika vikundi vya kazi vilivyopangwa kulingana na lugha tofauti.
Alasiri ya Jumanne ile ile, tarehe 9 Septemba 2025, kikao kazi kitajikita zaidi katika uhusiano wa kimisionari na Baraza la Kipapa kwa kuzingatia zaidi mifumo ya kuinua rasilimali za utume wa kimisionari, ambayo inaungwa mkono na Sadaka ya Petro na Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa (PMS).
Taarifa na mawazo kwa ajili ya majadiliano na utafiti zaidi yatatolewa kwa mawasilisho na Kardinali Tagle, Padre Tadeusz Nowak, Katibu Mkuu wa Shirika la Kipapa la Kueneza Imani (POPF), na Dakta Giuseppe De Summa, wa Ofisi ya Uhasibu na Fedha Baraza la Kipapa la Kimisionari. Haya yatafuatiwa na majadiliano kuhusu utume na wasifu wa utendaji kazi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa mbele ya Makatibu Wakuu wa PMS. Siku ya Jumatano, tarehe 10 Septemba 2025, Vikao vya mwisho vya Kozi iliyoandaliwa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji vitaandaliwa tena katika Chuo cha Kipapa cha Mtakatifu Petro. Mada ya “Askofu na Usimamizi wa Migogoro, Hasa Wakleri,” itatolewa na Monsinyo Peter Beer, Profesa katika Taasisi ya Anthropolojia katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, wakati Padre Hans Zollner, Mkuu wa Taasisi hiyo, atazungumzia “Wajibu wa Makanisa Mahususi kwa ajili ya Ulinzi wa Watoto wadogo na watu wazima walio katika mazingira magumu.
Alasiri, warsha za vikundi vya lugha zitaongozwa na washiriki wa Taasisi ya Gregorian ya Anthropolojia. Makundi mawili ya "maaskofu wapya" yatapokelewa pamoja katika Mkutano na Papa Leo XIV siku ya Alhamisi, tarehe 11 Septemba 2025.
Zoezi la kutoa semina za masomo zilizotengwa kwa ajili ya maaskofu waliowekwa wakfu hivi karibuni katika mamlaka ya kikanisa waliokabidhiwa uangalizi wa Barazala la Kipapa la Uinjilishaji lilianza mwaka 1994. Lengo lilikuwa ni kuwapa maaskofu wote wapya muda fulani. Mwanzoni mwa muhula wao, ili kutafakari juu ya athari nyingi za zoezi la huduma ya kiaskofu, kusikiliza mawasilisho, kupata habari, na uzoefu wa siku katika Roma zilizoadhimishwa kwa mazungumzo na sala, ili kushirikiwa na maaskofu wenzao kutoka sehemu zote za dunia.