Hamasa ya Papa kwa Kikundi Kazi cha Pamoja:kuungana katika ulimwengu uliogawanyika
Vatican News
Kikao cha Kikundi Kazi cha Pamoja kati ya Kanisa Katoliki na Baraza la Makanisa Ulimwenguni (WCC) kimehitimishwa tarehe 3 Septemba 2025. Ulikuwa ni Mkutano wa kubadilishana uzoefu, kuimarisha mahusiano, na kuchunguza vipaumbele vipya. Kwa vyombo vya habari vya Vatican, Monsinyo Flavio Pace, Katibu wa Baraza la Kipapa la Kuhamaisha Umoja wa Wakristo alijikita kufafanua juu ya kazi ya Kikundi Kazi cha Pamoja na Mkutano ambao walikutana asubuhi Septemba 3 na Baba Mtakatifu Leo XIV. Kikao cha pili cha awamu hii ya Kikundi Kazi cha Pamoja, kama ilivyo kwa kila tukio, kimsingi kimejitolea kuwafahamisha washiriki wa Kikundi na washiriki wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni na ukweli wa Curia Romana. Na kikao cha tarehe 2 Septemba kilikuwa kizuri sana, uzoefu wa mambo mengi.
Badala ya kutembelea Mabaraza mbalimbali ya Kipapa, tuliwaita pamoja wawakilishi wa Mabaraza hayo ya Kipapa au taasisi za kipapa katika vikundi vya watu wanne. Walipata fursa ya kutoa mada fupi ya kazi zao, lakini pia kushiriki katika harambee na mazungumzo, kwa mtindo mzuri wa sinodi.“Kwa hiyo, tulikuwa na Sekretarieti ya Vatican, Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Maendeleo Fungamani ya Kibinadamu, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji, Baraza la kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti, Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Majadiliano ya Dini Mbalimbali na Sekretarieti ya Sinodi. Hii iliwapa hisia ya ukweli hai wa Curia Romana, ambayo inaingiliana, kusikiliza, na inabadilika, kulingana na maeneo yake mbalimbali ya ujuzi. Kwa hiyo, awamu ya pili, inapofanyika Roma, kama ilivyo desturi, daima ni fursa ya kukutana na kusikiliza ukweli huu. Pia kulikuwa na hotuba ya Kardinali Kurt Koch, Mwenyekit wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Kikristo kuhusu changamoto za sasa za Kanisa la Kukuza Umoja wa Wakristo. Kisha kuna kazi ya ndani ya Kikundi Kazi cha Pamoja, ambacho kinajumuisha tume tatu ndogo za washiriki, Wakatoliki na washiriki wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, wakifanyia kazi mada fulani ambayo itawezekana kuwa mada ya hati, kama ilivyo mapokeo, mwishoni mwa mamlaka yao.”
Ikumbukwe kwamba mamlaka ya Kikundi hiki cha Pamoja cha Kazi itakamilika mwaka 2030 na itawasilisha matokeo yake kwa Kanisa Katoliki na Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Kwa hiyo, ni jitihada za miaka mingi, na moja ambayo itaendelezwa kwa muda. Mwisho, ningependa pia kutaja mkutano, tena kwa mtindo wa pamoja, wa mashirika ya kiekumene yaliyopo na yanayofanya kazi huko Roma: Centro Uno (Focolare), Centro Pro Unione, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, na Taasisi ya Uekumene katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Thomas wa Aquinas-Angelicum.
Ulikuwa ni mkutano mzuri sana. Kwanza, kwa sababu Baba Mtakatifu alikubali kuweka nafasi katika ajenda yake na kutupatia fursa ya kukutana kabla ya Katekesi yake. Hapo awali, ilipaswa kuwa salamu tu, fursa ya kujitambulisha na kupiga picha ya pamoja. Kiukweli, Baba Mtakatifu alitaka kutumia wakati huo na kila mmoja wa washiriki, kusikiliza asili na uhusiano wao, na kisha kutoa neno la kutia moyo kabla ya kusali sala ya Baba Yetu, baraka, na picha ya pamoja. Alisisitiza zaidi kwamba, "Kazi hii ya pamoja kati ya Kanisa Katoliki na Baraza la Makanisa Ulimwenguni haina budi kuendelea, hasa kwa sababu wito wa umoja, katika wakati huu ambapo dunia imegawanyika na kujeruhiwa, ni jambo la dharura. Kwa sababu mashahidi wa Kikristo na wa Kanisa hawawezi kujizuia kuwa wito wa umoja na ushirika."Na Sala ya Bwana, ambayo alisali pamoja, alisema kwamba "tunapata nguvu hii, chanzo hiki cha umoja, kwanza katika uhusiano wetu na Kristo, kwa kumwita Mungu "Baba." Kisha akatupatia baraka zake. Kwa hiyo ulikuwa ni mkutano mzuri zaidi kuliko ilivyotarajiwa, kwa maana ya kwamba alijitolea wakati mwingi zaidi kwetu, na maneno haya rahisi yalitupatia furaha ya kusonga mbele tukiwa na matumaini na pia jukumu la agizo hili la ushirika.