Carlo Acutis Mtakatifu wa vijana,Sayansi na Teknolojia
Na Padre Philemon Anthony Chacha, SDB, - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) anakazia zaidi: Udumifu, uvumilivu na unyenyekevu wa moyo kama alama za utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo dhidi ya tabia matumizi ya nguvu, ubinafsi na uchoyo pamoja na hali ya mtu kujiridhisha binafsi katika ufahari wake. Wakristo wawe wanyenyekevu kwa kujikita katika ukweli na uwazi; utu wema pamoja na kuwa na matumizi sahihi ya ulimi! Waamini wafurahie pia mafanikio ya jirani zao, wawasahihishe kwa upole na udugu pale wanapolegea katika dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu. Hakuna unyenyekevu pasi na kunyenyekeshwa na huu ni ushuhuda wa utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo. Kuna waamini wanaoendelea kusimamia haki, amani na maridhiano katika jamii kiasi hata cha kuyamimina maisha yao! Hawa wanahesabika kuwa ni vyombo vya amani! Maisha ya Kikristo ni chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu na kwamba, furaha ya kweli inafumbatwa katika upendo!
Wakristo wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha na utulivu wa ndani, kwa kujenga na kudumisha umoja na upendo wa kidugu. Waamini waoneshe uhuru na upendo wa ndani kabisa kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya upya wa maisha yao! Familia ya Mungu ioneshe ujasiri wa kutoka kifua mbele kama ilivyokuwa kwa watakatifu wa nyakati mbali mbali ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Baba Mtakatifu anaendelea kusema, utakatifu unafumbatwa katika maisha ya sala kama sehemu ya mchakato wa kutaka kujenga uhusiano wa karibu na Mwenyezi Mungu, kumbe, sala endelevu ni chachu ya utakatifu wa maisha! Ukimya na tafakuri ni nyenzo zinazojenga uhusiano mwema na Kristo Yesu! Lakini, sala ya kweli inamwilishwa katika uhalisia wa maisha yanayofumbatwa katika upendo. Waamini wajenge utamaduni na sanaa ya kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika medani mbalimbali za maisha kwani hiki ni kiini na utambulisho wa Kanisa. Waamini wajitahidi kukutana na Kristo Yesu katika Neno na Sakramenti za Kanisa, ili waweze kuwa ni chachu ya utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo!
Baba Mtakatifu anasema mapambano ya maisha ya kiroho yanakita mizizi yake katika; kukesha na kufanya mang’amuzi! Baba Mtakatifu Francisko anasema, maisha ya kikristo ni mapambano endelevu yanayohitaji nguvu na ujasiri, ili kumpatia nafasi Kristo aweze kushinda na hatimaye, waamini kufurahia maisha. Waamini watambue kwamba, shetani, Ibilisi yupo na wala si dhana ya kufikirika tu! Waamini wawe macho na waendelee kukesha na kusali kwa kutambua kwamba, ushindi wao unafumbatwa katika Msalaba wa Kristo. Utakatifu ni chemchemi ya furaha na amani ya ndani. Huu ni mwaliko wa kupambana na “giza la maisha ya kiroho” kwa kujikita katika mang’amuzi ya maisha ya kiroho kwa kutafakari kwa kina na mapana matamanio halali ya maisha, uchungu na fadhaa katika maisha yao; hofu na mashaka ili kutambua njia zinazowaelekeza katika uhuru wa kweli, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati kadiri ya mwanga wa Kristo Mfufuka. Mang’amuzi ya maisha ya kiroho, yawasaidie waamini kutambua Fumbo la Utatu Mtakatifu. Waamini wampatie nafasi Kristo Yesu ili aweze kuzungumza kutoka katika undani wa maisha yao! Furaha ya kweli anasema Mtakatifu Bonaventura, imetundikwa kwenye mti wa Msalaba. Waamini wamwombe Roho Mtakatifu ili aweze kuwaondolea woga na hofu zisizokuwa na mashiko ili kuanza mchakato wa kutoka katika ubinafsi, tayari kuliendea Fumbo la maisha ya Mungu, anayewasaidia waja wake kutekeleza utume wao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya ndugu zao katika Kristo!
Ndugu Msikilizaji na Msomaji wa Radio Vatican. Tunapoendela na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu: Mahujaji wa matumaini, Mama Kanisa anaendelea kutuhimiza kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa maisha na uzima wa milele hasa katika kufanya hija ya maisha ya kiroho. Hii ni nafasi nzuri kabisa ya toba, wongofu na utakatifu wa maisha. Kumbe ni katika muktadha huu ambapo Kanisa linaendelea kutupatia matukio mbalimbali ndani ya mwaka wa Jubilei katika kuishi vyema tunu za ukristo wetu. Tarehe 7 Septemba 2025, tutashuhudia maadhimisho kumtangaza Mwenyeheri Carlo Acutis kuwa Mtakatifu, akiwa na mwenzake kijana Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati. Hivyo ni fursa kwa vijana wote kuelewa na kujifunza juu ya maisha ya Mtakatifu huyu, ambaye anasifika kuwa Mtakatifu wa kizazi kipya, Mtakatifu wa T-shirt na Jeans. Carlo Acutis ni kijana aliyeishi hapa duniani kwa takribani miaka 15 tu, na kufariki kwa ugonjwa wa leukaemia. Carlo ameibuka kama kielelezo cha maisha ya imani kwa vijana duniani kote. Maisha yake yalijaa furaha na tamanio la ndani la kuishi utakatifu na matendo yake yanaendelea kuwa chanzo cha mwongozo kwa vijana wengi, na kumfanya kuwa mtakatifu wa kisasa anayezungumza moja kwa moja kwa vijana wa kizazi kipya. Alikuwa kijana mwenye shauku ya kompyuta na teknolojia kama vijana wengine. Lakini tofauti yake ilikuwa ni upendo wake mkubwa kwa Yesu Kristo. Tangu alipopokea Komunyo ya Kwanza akiwa na umri wa miaka saba, Carlo hakuwahi kukosa Ibada ya Misa Takatifu kila siku na alipenda kukaa na kuabudu mbele ya Ekaristi Takatifu kwa muda mrefu.
Carlo alizaliwa London nchini Uingereza mnamo mwaka 1991 na wazazi kutoka Italia. Baada ya takriban miezi sita walihamia mji wa Milano, nchini Italia. Tangu utotoni alionesha hamu kubwa ya kumjua na kumpenda Mwenyezi Mungu. Maisha yake yalijengwa kwa msingi wa imani, akihudhuria Misa kila siku na kujishughulisha na maisha ya sala. Alifariki Monza, nchini Italia tarehe 12 Oktoba 2006 akiwa na umri wa miaka 15, lakini ingawa alikuwa na umri mdogo, aliacha mchango mkubwa kwa jamii na marafiki zake. Carlo alimwamini Mama Bikira Maria kwa dhati, alikuwa akisali Rosari kila siku na kumtumikia kwa moyo wote. Itakumbukwa kwamba, Rozari Takatifu ni muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu sanjari na Upendo na huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Ni njia muafaka ya kutafakari maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kumfahamu, kumpenda, kumfuasa na kumtumikia kwa njia ya upendo kwa Mungu na jirani wenye shida. Waamini wanahamasishwa kuendelea kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu!
Ingawa Carlo alikuwa mtaalamu wa teknolojia na kompyuta, alijua kuwa lengo la maisha ni kumfurahia Mungu milele. "Sote tunazaliwa kama wa kipekee," alisema, "lakini wengi hufa kama nakala au fotokopi." Kwa Carlo, njia ya kwenda mbinguni ilikuwa ni kwa kufuata Neno la Mungu, kushiriki Sakramenti na kusali kwa uaminifu. Aliiona Ekaristi Takatifu kuwa kiini na hatima ya maisha yake, akiita "barabara yangu ya kwenda mbinguni." Uhusiano huu wa kina na Ekaristi Takatifu, pamoja na shauku yake ya teknolojia, umemfanya kuwa mfano wa pekee wa jinsi teknolojia inavyoweza kutumika kwa imani. Hata alipoanza kuugua, alitoa mateso yake kwa ajili ya Baba Mtakatifu na Kanisa. Maisha yake mafupi yameacha mwanga wa mfano kwa vijana wote. Carlo anatuonesha kwamba: unaweza kuwa mtaalam wa teknolojia na kuwa mtakatifu kwa wakati mmoja. Hakukataa raha za ujana, bali aliziishi kwa undani zaidi kwa kumfuata Kristo Yesu. Hapa tunakumbuka maneno ya Mtakatifu Don Bosco aliyowaambia vijana wake “cheza, imba, ruka lakini usitende dhambi” ni maneno ambayo tunaona katika maisha ya Carlo, maana aliweza kuyaishi katika maisha yake. Leo, Carlo anatuachia changamoto: kuishi maisha yetu kwa ukweli na upendo kwa Mungu na jirani tukijua kwamba kila dakika ina thamani kubwa. Kama alivyosema mwishoni: "Nimefurahi kufa kwa maana nimeishi bila kupoteza hata dakika moja kwa mambo yasiyompendeza Mungu." Ewe kijana wa kizazi kipya, unatumiaje mtandao na mitandao ya kijamii katika kulisha roho yako?
Itakumbukwa kwamba, Carlo Cutis alifariki dunia tarehe 12, Oktoba 2006 na kifo chake kilitokana na ugonjwa wa Saratani ya damu, Leukemia, katika Hospitali ya Mtakatifu Gerardo, mji wa Monza, Italia. Mchakato wake wa kutangazwa Mtakatifu ulipata kibali kuanzia tarehe 13 Mei 2013. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 5 Julai 2018 alimtangaza kuwa Mtumishi wa Mungu. Februari 21, 2020 Papa Francisko aliridhia mchakato wa kutangazwa kuwa Mwenyeheri. Muuujiza uliomwinua kuwa Mwenye heri ulitokea kutokana na uponyaji wa mtoto Nchini Brazil aliyekuwa na shida ya kongosho hapo mwaka 2013. Jumamosi Oktoba 10, 2020 katika mji wa Assisi, Mtumishi wa Mungu Carlo Acutis akatangazwa kuwa Mwenyeheri, tangu wakati huo, watu wa Mungu na hasa vijana wa kizazi kipya wanaenzi wito wake wa kusali Rozari, Kuabudu Ekaristi Takatifu, Kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu na kutoa sadaka ili kuwasaidia maskini na wahitaji zaidi.