Dk.Ruffini kwa UCAP:katika AI epuka mfumo wa utawala ambao unaharibu kila kitu,ukipuuza ukweli!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baraza la Kipapa la Mawasiliano liliwataka waandishi wa habari wa Kiafrika kushikilia sana maadili ya binadamu katika zama za Akili Unde(AI) na kuonya dhidi ya hatari ya kuruhusu teknolojia kudhalilisha hadhi ya binadamu. Hayo yalisikika katika hotuba iliyoandaliwa na Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, Dk. Paolo Rufini iliyosomwa na Mwakilishi wa Baraza katika tukio hilo, Monsinyo Janvier Yameogo, kwa waandishi wa habari katika ufunguzi wa Kongamano la III la Umoja wa Vyombo vya Habari Katoliki Afrika(UCAP) huko mjini Accra nchini Ghana. Katika Kongamano hilo la Juma moja, lililoanza tarehe 10 Agosti na litahitimishwa tarehe 17 Agosti 2025, katika Taasisi ya Usimamizi na Mafunzo ya Kitaalamu ya Ghana, linafanyika chini ya kauli mbiu: "Kusawazisha Maendeleo ya Kiteknolojia na Uhifadhi wa Maadili ya Kibinadamu katika Enzi ya Akili Unde(AI).”
‘Kusoma na kusimilia historia kwa ajili ya moyo’
Kwa njia hiyo katika hotuba alisema: "Tunapaswa kusoma na kusimulia historia kwa akili ya moyo, kwa hekima ya upendo, bila kuchanganya njia na mwisho wake, ukweli na uongo, uelewa na hesabu. Tunachotakiwa kufanya ni kubaki wanadamu. Na kuwa zaidi na zaidi.” Monsinyo Yameogo aliwakumbusha washiriki hao kuhusu hali halisi ya mawasiliano kwamba: “Asili ya Kilatini ya neno ‘mawasiliano’ inachanganya maneno mawili: ‘cum’ (pamoja) na ‘munus’ (zawadi), ambayo hutuambia kwamba mawasiliano kwanza kabisa ni zawadi ya sisi wenyewe, zawadi inayotokana na uhusiano tunaoanzisha sisi kwa sisi.” Kwa njia hiyo, jumuiya ya Wakristo wa kale, inayofafanuliwa katika Kitabu cha Matendo ya Mitume ilikuwa inaonesha kuwa wao “walikuwa na moyo mmoja na nafsi moja”, na ilipata nguvu zake kutokana na ushirika, ambao unasalia kuwa “siri ya mawasiliano ya Kanisa.”
Changamoto zinatoloewa na AI
Tukigeukia changamoto zinazoletwa na Akili Unde(AI) ujumbe wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ulionya juu ya hatari ya "mfumo wa utawala ambao unaharibu kila kitu, ukipuuza ukweli, haki na uzuri, ambapo upekee wa mtu binafsi hutolewa pamoja na hadhi ya mtu binafsi.” Kadhalika wito huo ulitahadharisha “kile kisemacho kwamba Akili nunde haiwezi kukosea na kwamba kuwa mawazo kama hayo yanapingana na kanuni za kisayansi zinazoiunga mkono.” Kadhalika aliongeza kusema: "Kwa upande mmoja, kuna udikteta wa mashine, unaoelekezwa na mawazo ya kiimla; kwa upande mwingine, kuna uhuru wa binadamu, ambao bila hiyo hakuna ukweli.
Kuwajibika kwa ajili ya watu wengine
Hatimaye katika ujumbe huo wa Vatican kulikuwa na swali: “ikiwa matokeo ya muda mfupi ya akili unde inategemea, ni nani anayeidhibiti, matokeo muda mrefu yanategemea ikiwa yanaweza kudhibitiwa au la? Monsinyo Yameogo alihimiza Kongamano hilo “ kutimiza lengo lake la kuandaa wataalamu wa vyombo vya habari kuelimisha hadhira juu ya umuhimu wa kuhifadhi maadili ya binadamu katika ulimwengu unaoendeshwa na teknolojia, na kuendeleza michango ya Umoja wa Vyombo vya habari Katoliki Afrika (UCAP) kwa utume wa Kanisa, ikiwa ni pamoja na jukumu lake katika Sinodi inayoendelea kuhusu Sinodi.” Akikumbuka wito wa Papa Francisko wa mshikamano wa kimataifa katika Waraka wa Fratelli tutti yaani Wote ni Ndugu na mwangwi wake katika dhana ya Kiafrika ya Ubuntu, ilisisitiza kwamba “kustawi kwa binadamu kunapatikana katika mahusiano, na “kwamba sote tumeunganishwa na kuwajibika kwa ajili ya mtu mwingine.” Kwa kifupi, wito kama huo ni “kwa ajili ya urafiki wa kimataifa, mshikamano na kutegemeana kwa jamii endelevu zaidi.”