杏MAP导航

Tafuta

WUCWO inasema: Huu ni wakati wa kuhakikisha kwamba, utume wao unamwilishwa katika huduma, njia ya kuwapeleka mbinguni kwa Baba. WUCWO inasema: Huu ni wakati wa kuhakikisha kwamba, utume wao unamwilishwa katika huduma, njia ya kuwapeleka mbinguni kwa Baba.  

Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika: Utu, Heshima Na Haki Msingi za Binadamu

Hii ni changamoto ya kuachana na tabia ya uchoyo na ubinafsi na hivyo kuanza kuambatana na Mama Kanisa katika safari ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari. Ni wakati wa kujifunza kusamehe na kusahau; wanawake Barani Afrika wawe ni mashuhuda na wajenzi wa haki, amani na maridhiano kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaomgusa mtu mzima!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika, WUCWO-Afrika kuanzia tarehe 28 Julai hadi tarehe 1 Agosti 2025 unaadhimisha Mkutano wake mkuu, Jijini Entebbe, Uganda kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Wekeza katika Malezi ya familia kama Daraja la Maisha ya Furaha na Utakatifu.” Mkutano ulifunguliwa na Askofu mkuu Paul Ssemogerere, wa Jimbo kuu la Kampala, Uganda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Walei Baraza la Maaskofu Uganda tarehe 29 Julai 2025 kwa Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Madhabahu ya Namgongo, Uganda. WUCWO, kwa niaba ya wanawake wapatao milioni 36, iliwasilisha ombi lao la kwanza mwaka 1960, likisisitiza umuhimu wa kupyaisha: Utu, haki na heshima ya mwanamke, pamoja na nafasi yake katika familia, jamii na Kanisa katika ujumla wake.  Tafakari hii ya kihistoria inawakumbusha Wanawake Wakatoliki kuwa kile kilichoanzishwa, kilichopangwa na kutekelezwa na waliotutangulia, leo hii wanakienzi na kukiendeleza kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina ulioshuhudiwa kwa macho ya imani na maisha safi ya watoto wa Mungu.

WUCWO: Wanawake simameni kidete kulinda: utu, heshima na haki msingi
WUCWO: Wanawake simameni kidete kulinda: utu, heshima na haki msingi

Katika Ulimwengu mamboleo ambapo vijana wanaogopa kuingia katika maisha ya Sakramenti ya ndoa, ni lazima kupyaisha tena wito wa ndoa na familia. Kumbe, Kanisa linapaswa: Kutoa msaada kwa kila hatua ya maisha—kuanzia ujana hadi uzee; Kukuza utakatifu wa upendo wa kibinadamu na usafi wa moyo; Kuhimiza sera zinazowezesha familia kukua na kustawi; Kutoa mafunzo kwa viongozi wa kidini na waamini walei ili waelewe maana ya maisha halisi ya familia; Kukuza jumuiya jumuishi kati ya vizazi mbalimbali. Familia si wapokeaji tu wa imani, bali ni wahusika wakuu wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kila tendo la kifamilia kuanzia sala za pamoja hadi kushiriki changamoto na mateso kwa pamoja ni kielelezo cha Injili hai. Kanisa linapaswa kuwa karibu zaidi na familia, hasa zile zinazolelewa na mzazi mmoja, kwa njia ya kuzisikiliza na kuandamana nazo.

Wanawake wanao mchango mkubwa katika maendeleo na ustawi wa Kanisa
Wanawake wanao mchango mkubwa katika maendeleo na ustawi wa Kanisa

Vitendo vya ukatili wa kijinsia majumbani vimeendelea kutikisa wanawake sehemu nyingi Barani Afrika, huku wenza wakifanyiana visa vinavyosababisha wakati mwingine vifo, ulemavu na uharibifu wa mali. Ukatili na Ubaguzi Dhidi ya Wanawake: Utafiti wa WUCWO kupitia mradi wa Uangalizi wa Wanawake wanaopitia nyanyaso chini ya mradi wa (World Women Observatory - WWO), umeonesha kuwa takriban 67% ya wanawake 10,680 walioshiriki utafiti kutoka nchi 36 Afrika wameshuhudia ukatili wa kijinsia. Maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni ukatili wa majumbani, wa kiuchumi, na ubaguzi wa kielimu. Mfumo dume, nyanyaso, mifumbo mbalimbali ya utumwa mamboleo na ukatili wa majumbani, ukeketaji; ukosefu wa haki na fursa sawa ni mambo ambayo yanasigina kwa kiasi kikubwa utu na heshima ya wanawake sehemu mbali mbali za dunia! Hili ni tatizo nyeti ambalo linaendelea kuzipekenyua familia nyingi, kiasi kwamba, madhara yake ni makubwa katika malezi, makuzi na ustawi wa familia zenyewe. Kanisa linasema, hili ni tatizo linalopaswa kuvaliwa njuga ili kulinda na kudumisha tunu msingi za Injili ya familia, utu, heshima na haki msingi za wanawake! Watu wanapaswa kutambua na kushirikishana Habari Njema kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu na ni mazuri sana! Huu ni wakati wa kujenga na kudumisha utamaduni wa kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Ukatili wa majumbani, kiuchumi na ubaguzi wa elimu umekithiri Afrika
Ukatili wa majumbani, kiuchumi na ubaguzi wa elimu umekithiri Afrika

Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika, WUCWO-Afrika, katika hotuba yake ya kufunga mkutano wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika, uliokuwa unaadhimishwa huko Entebbe, nchini Uganda, amewasihi Wanawake Wakatoliki Barani Afrika kumwilisha sala zao katika matendo adili na matakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia zao. Huu ni wakati wa kuhakikisha kwamba, utume wao unamwilishwa katika huduma, njia ya kuwapeleka mbinguni kwa Baba. Amewashukuru wajumbe na wadau wote waliowezesha maadhimisho ya mkutano huu, changamoto kubwa mbele yao ni wanawake kuondokana na chuki, kwa kujikita katika upendo thabiti, kwa kuendelea kuiga mfano wa Bikira Maria, Mlinzi na Mwombezi wao wa daima. Hii ni changamoto ya kuachana na tabia ya uchoyo na ubinafsi na hivyo kuanza kuambatana na Mama Kanisa katika safari ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari. Ni wakati wa kujifunza kusamehe na kusahau; wanawake Barani Afrika wawe ni mashuhuda na wajenzi wa haki, amani na maridhiano. Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika ameomba msamaha kwa mapungufu yaliyojitokeza katika Mkutano huu. Kumbe, Wanawake Wakatoliki waanze kujifunza kujinyenyekesha, kusamahe, kusikiliza na hatimaye, kujisadaka kwa ajili ya upendo na mafungamano ya kijamii.

Wanawake Afrika
01 Agosti 2025, 16:51