杏MAP导航

Tafuta

Kwa miongo mitatu, amekuwa daraja la mawasiliano kati ya Vatican na ulimwengu wa Kiswahili, akieneza Habari Njema, akiimarisha imani ya waamini, na kuwa sauti ya matumaini kwa mamilioni ya wasikilizaji. Kwa miongo mitatu, amekuwa daraja la mawasiliano kati ya Vatican na ulimwengu wa Kiswahili, akieneza Habari Njema, akiimarisha imani ya waamini, na kuwa sauti ya matumaini kwa mamilioni ya wasikilizaji. 

Kilele cha Jubilei ya Miaka 25 ya Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Padri Mjigwa alizaliwa tarehe 28 Novemba 1964. Daraja Takatifu ya Upadri tarehe 17 Aprili 1999 mikononi mwa Askofu mkuu Cesare Nosiglia, kwenye Parokia ya “SS. Corpo e Sangue di Cristo” Jimbo kuu la Roma. Kabla ya kujiunga na utume wa Vatican, alihudumu kama Paroko Msaidizi; Mhariri mkuu wa Radio Mwangaza FM, Dodoma, Mtangazaji Radio Tumaini, Jimbo kuu la Dar es Salaam na pia Mkuu wa Chuo cha Ufundi cha Mtakatifu Gaspari, Kunduchi, Dar es Salaam! Yaani!

Na Sarah Pelaji – Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei ni muda muafaka wa kufanya toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia tayari kukimbilia huruma na kuambata msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake. Ni kipindi cha kushukuru na kuomba tena neema ya kuweza kujizatiti zaidi katika maisha na wito, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani, kama shuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu. Jubilei ni muda muafaka wa kuchuchumilia na kuambata udumifu katika imani, matumaini na mapendo tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia: mapendo imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa.

Papa Francisko akimbariki Padre Mjigwa kwa Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre
Papa Francisko akimbariki Padre Mjigwa kwa Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre   (Vatican Media)

Katika tukio la kihistoria na la kipekee lililojawa na moyo wa shukrani na tafakari, Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., ameadhimisha Jubilei ya miaka 25 ya Daraja Takatifu la Upadri sanjari na kutimiza miaka 60 ya kuzaliwa. Sherehe hii imefanyika hivi karibuni katika Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji, Nyamiongo, Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania mahali alikozaliwa na kulelewa. Padre Mjigwa, C.PP.S. kwa zaidi ya miongo mitatu amekuwa akihudumu kama mwandishi na mtangazaji wa Radio Vatican. Akifahamika na wengi kwa jina maarufu ‘Mtoto wa Mkulima, na falsafa ya ufagio ni unyenyekevu.’ Ni mmoja wa wanahabari wachache wa Kanisa Katoliki wa Kiafrika waliotumikia kwa uaminifu katika vyombo vya habari vya Vatican tangu mwaka 1994 wakati wa maadhimisho ya kwanza ya Sinodi ya Maaskofu wa Kanisa Barani Afrika.

Kilele cha Jubilei, Parokia ya Mt. Yohane Mbatizaji, Nyamiongo, Musoma
Kilele cha Jubilei, Parokia ya Mt. Yohane Mbatizaji, Nyamiongo, Musoma

Katika Misa Takatifu ya shukrani iliyoongozwa na Padre Mjigwa C.PP.S. mwenyewe, mahubiri yenye tafakari ya kina yalitolewa na Padre Vedasto Ngowi,C.PP.S., Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Kanda ya Tanzania. Padri Ngowi C.PP.S.   alimtaja Padre Mjigwa kuwa ni mfano bora wa Ukuhani anayejituma kwa moyo wote katika utume wa Kristo, akisema: “Padre Mjigwa ametumia vyema zawadi ya maisha na wito wa upadri aliopokea kutoka kwa Mungu. Si heshima tu kwake binafsi, bali pia kwa Familia yake, Shirika lake, na Kanisa kwa ujumla.” Akifafanua maana ya ukuhani katika Kanisa Katoliki, Padre Ngowi C.PP.S. alieleza kuwa Kuhani ni hazina ya kipekee yenye thamani, inayoweza kufananishwa na chombo cha udongo kinachobeba vitu vya thamani kubwa. Aliunganisha mafundisho ya Biblia kwa kumrejea Kuhani Mkuu Melkisedeki, Kuhani na Mfalme wa Amani aliyekutana na Abrahamu na kutoa sadaka ya mkate na divai kwa Mungu, akisema ukuhani wa Kristo unaongozwa katika mfano huo wa Melkisedeki, ambao hauna mipaka ya kikabila wala ya kijiografia.

Ibada ya Misa Takatifu, "Procura Tegeta" Jimbo kuu la Dar es Salaam
Ibada ya Misa Takatifu, "Procura Tegeta" Jimbo kuu la Dar es Salaam

“Mwenyezi Mungu alipokuwa akijichagulia makuhani, alitazama kijiji kidogo cha Makoko na akamwona kijana Richard Mjigwa. Alimwita, akamwandaa na akampeleka mbali na nyumbani kwao Makoko, Musoma hadi Roma ili aitangaze Injili kupitia Radio Vatican. Kwa kweli tunakushukuru sana kwa kuitikia wito wa Kristo,” alisisitiza Padre Ngowi C.PP.S. Akimwelezea zaidi, Padre Ngowi alisema Padre Mjigwa ni Kuhani mchapakazi asiyependa uzembe, anayejitoa kwa dhati katika utumishi wake. Aliongeza kuwa ingawa hahudumu katika Parokia moja kwa moja, utume wake katika vyombo vya habari vya Vatican ni mkubwa sana katika kuwafikia waamini wengi sehemu mbalimbali za duniani kwa njia ya: Habari, Mafundisho Jamii ya Kanisa, Elimu ya imani na Katekesi ya kina.

Padre Richard A. Mjigwa akipewa nishani ya huduma bora kutoka kwa Papa.
Padre Richard A. Mjigwa akipewa nishani ya huduma bora kutoka kwa Papa.

“Padre Mjigwa si mwandishi wa kawaida wa habari, yeye huandika na kutangaza kwa mtindo wa katekesi akifundisha juu ya: Imani, Sakramenti, Maisha adili, Sala, Utume na maisha ya Kanisa. Kwa njia hii, anaelimisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu,” alisema Padre Ngowi C.PP.S. Alitoa shukrani kwa Mungu kwa maisha na utume wa Padre Mjigwa C.PP.S.  akimwombea afya njema na baraka zaidi katika safari yake ya kuhudumu kwa Kristo kupitia mawasiliano ya Kanisa. Alisisitiza kuwa dhabihu anayoitoa kila siku kwenye Altare ya maisha yake ya kila siku iwe kwa ajili ya utakatifu na wokovu wa watu, na kwamba aendelee kuhuisha sadaka ya Kristo Msalabani hadi siku ya mwisho. “Padre Mjigwa C.PP.S.   wewe ni Kuhani milele kwa mujibu wa utaratibu wa Ukuhani wa Melkisedeki. Hongera sana kwa miaka 25 ya huduma ya Upadri na miaka 60 ya maisha yako ya kuzaliwa. Tazama ulipotoka, na utazame ulipo sasa ni ushuhuda wa baraka na neema ya Mungu katika maisha ya mhudumu wake mwaminifu,” alihitimisha.

Padre Mjigwa akikata keki!
Padre Mjigwa akikata keki!

Kwa upande wake, Padre Mjigwa C.PP.S.  aliushukuru uongozi wa Kanisa, Shirika la Damu Azizi ya Yesu, familia yake, na wale wote waliomsaidia katika safari yake ya wito tangu utotoni hadi kufikia Daraja Takatifu ya Upadre. Alitambua mchango mkubwa wa walezi wake wa kiroho, wazazi, ndugu, marafiki, wakufunzi wa seminari, mapadri, na maaskofu waliomjenga katika: Utu, imani, malezi na majiundo ya kipadre. Aliwashukuru hata wale ambao alisahau kuwashukuru na kuwapongeza katika safari ya maisha na wito wake kama Padre.

Litungu kwenda mbele ili kunogesha Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre
Litungu kwenda mbele ili kunogesha Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre

Wasifu Mfupi wa Padri Richard A. Mjigwa, C.PP.S.: Padri Mjigwa alizaliwa tarehe 28 Novemba 1964, katika kijiji cha Makoko, Jimbo Katoliki Musoma. Alipata Daraja Takatifu ya Upadri tarehe 17 Aprili 1999 mikononi mwa Askofu mkuu Cesare Nosiglia, kwenye Parokia ya “SS. Corpo e Sangue di Cristo” Jimbo kuu la Roma. Kabla ya kujiunga na utume wa Vatican, alihudumu kama Paroko Msaidizi katika Parokia ya Mtongani, Kunduchi –Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam kwa miaka mitatu. Pia amewahi kuhudumu kama Mhariri mkuu wa Radio Mwangaza FM, Dodoma, Mtangazaji Radio Tumaini, Jimbo kuu la Dar es Salaam na aliwahi pia kuwa Mkuu wa Chuo cha Ufundi cha Mtakatifu Gaspari, Kunduchi, Dar es Salaam. Tangu mwaka 1994 hadi sasa, Padre Richard Mjigwa, C.PP.S., amekuwa mwandishi na mtangazaji wa Radio Vatican akihudumu kwa bidii, uaminifu na mapendo kwa ajili ya Injili ya Kristo. Kwa miongo mitatu, amekuwa daraja la mawasiliano kati ya Vatican na ulimwengu wa Kiswahili, akieneza Habari Njema, akiimarisha imani ya waamini, na kuwa sauti ya matumaini kwa mamilioni ya wasikilizaji.

Jubilei Padri Mjigwa
13 Agosti 2025, 11:19