Kardinali Parolin,atakuwa nchini Burundi kufunga Jubilei ya miaka 60 ya uhusiano na Vatican
Vatican News
Kwa kuitikia mwaliko wa Kanisa mahalia na mamlaka ya Burundi, Katibu Mkuu wa Vatican Kardinali Pietro Parolin atasafiri hadi nchi ya Afrika kuanzia tarehe Agosti 12, hadi Jumatatu, tarehe 18 Agosti 2025. Safari hii ni katika fursa ya kuadhimisha kufunga Mwaka wa Jubilei ya Miaka 60 ya Mahusiano ya Kidiplomasia kati ya Burundi na Vatican, pamoja na uzinduzi wa mnara na uwekaji wa jiwe la msingi wa kituo cha afya kwa ajili ya heshima ya aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Burundi, Askofu Mkuu Michael Aidan Courtney, ambaye miaka ishirini na tatu iliyopita aliuawa kwa kuviziwa.
Kumbuka Balozi wa Vatican Courtney
Alipoteuliwa mnamo mwaka wa 2000 na Mtakatifu Yohane Paulo II kama mwakilishi wa Papa katika nchi iliyoharibiwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, Askofu Mkuu Courtney alichukua nafasi kubwa katika kufikia makubaliano ya mwezi Novemba 2003 kati ya serikali ya Burundi na waasi wa Kihutu. Akiwa ametumwa katika Ubalozi wa Kitume nchini Cuba, Kuhani huyo mzaliwa wa Ireland aliomba kubaki jijini Bujumbura, mji Mkuu kwa muda wa ziada, huku akiamini kwamba kungewapo uwezekano wa amani ya uhakika. Akiwa safarini ambayo haikuwa si mbali na mji mkuu wa Burundi, gari lake lilipigwa na milio kadhaa ya risasi. Mhudumu pekee wa gari hilo aligongwa, Askofu mkuu alikufa akiwa hospitalini mnamo tarehe 29 Desemba 2003, akiwa na umri wa miaka 58 tu.
Mnamo mwaka 2023, miaka ishirini baada ya kifo chake, Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Vatican wa Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa aliadhimisha Misa ya kumbukumbu ya Balozi huyo katika Kikanisa cha Ireland kilichopo kwenye Groto za Vatican. Na kwa sasa nchi nzima, mbele ya Kardinali Parolin, itamkumbuka Askofu Mkuu kwa kuanzishwa kwa kituo hicho ambacho kitajengwa mahali pale alipouawa. Mpango huo ulitangazwa mwaka 2024 na Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye, na tarehe ya uwekaji wa jiwe la msingi ilipangwa kuwa tarehe 14 Agosti 2025. Siku hiyo, Kardinali Parolin ataongoza sherehe za kuzindua mnara huo na kuashiria kuanza kwa ujenzi wa kituo hicho cha afya.
Mpango mzima wa safari
Mpango wa kina wa safari ya Kardinali Parolin umetolewa na Sekretarieti ya Vatican kwenye akaunti ya Facebook, @TerzaLoggia. Habari zinasema kuwa, Kardinali huyo ataadhimisha Misa tarehe 13 Agosti 2025 na Baraza la Maaskofu wa Burundi, ambapo watakutana naye kwa faragha.
Mkutano na Rais Ndayshimiye na utiaji saini wa mikataba maalum kati ya Baraza la Maaskofu na serikali umepangwa kufanyika siku hiyo hiyo. Ijumaa, tarehe 15 Agosti 2025 Kardinali Parolin ataadhimisha Misa katika Madhabahu ya Maria ya Mugera, kabla ya kutembelea mji mkuu wa kisiasa na kiutawala, huko Gitega.
Misa nyingine itaadhimishwa Jumamosi, tarehe 16 Agosti 2025, na mara baada ya hapo, Kardinali Parolin atakutana na waseminari na wasimamizi wakuu wa mashirika ya kiume na ya kike. Siku hiyo hiyo, uzinduzi wa kumbukumbu ya Askofu Mkuu Michael Aidan Courtney utafanyika katika Ofisi ya Balozi wa Kitume nchini Burundi, pamoja na mapokezi na kikundi cha Wanadiplomasia.
Hatimaye, Dominika tarehe 17 Agosti 2025, Kardinali Parolin ataongoza Misa ya kufunga Jubilei ya miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Burundi na Vatican katika Madhabahu ya Mama Yetu wa (Notre-Dame Trois Fois admirable de Schoenstatt,) iliyojengwa kwenye ardhi ileile ambayo Mtakatifu Yohane Paulo II aliadhimisha Ibada yaMisa Takatifu kunako tarehe 7 Septemba 1990.