Kard.Parolin:Liturujia&maisha,kutafakari&kutenda,kunatufanya kuwa mafundi wa umoja
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Tarehe 25 Agosti 2025, Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican akiwa katika Kanisa Kuu la Napoli, nchini Italia, alihutubia washiriki katika ufunguzi wa Juma la 75 ya Liturujia Kitaifa. Tafakari yake, ikiongozwa na mada: “Liturujia inalisha na kudumisha tumaini,” na kushirikishwa kwa wasomi na wanaliturujia wapatao 500 ambao kwa siku hizi, hadi tarehe 28 Agosti watachunguza mada iliyopangwa: “Ninyi ni tumaini letu. Liturujia: kutoka kutafakari hadi kutenda.” Kwa njia hiyo, tumaini, tafakari, hatua, na amani yalikuwa ni manne yaliyoongoza tafakari kamili ya Kardinali Parolin. Akianza hotuba yake aliwakumbusha wasikilizaji kwamba imani katika Kristo, “tumaini letu,” kama inavyotangazwa katika Te Deum (Shukrani kwa Mungu) na Jubilei yenyewe 2025 ni “hali halisi tunayoadhimisha na kuishi katika liturujia.” Kwa wale waliolemewa na uchovu, udhaifu, na dhambi, alisema, liturujia inakuwa mahali ambapo mtu anaweza kujiachia mwenyewe kwa upendo na huruma ya Mungu.
Kusali kwa imani na tumiani na kumuona Mungu katika adhimisho
Kardinali alisema "Ili liturujia iweze kulisha imani na tumaini la kweli ni lazima kumwona Mungu katika adhimisho hilo, tukizoeza mioyo yetu mbele zake kwa njia ya kutafakari. Tafakari, si tu kulisha macho, bali ni kukutana kwa ndani kabisa na Mungu ambayo inaongoza nje kwa Mwingine. Ni mtazamo wa kutambua karama ya Mungu katika liturujia, ambalo ni Fumbo la Pasaka la Kristo, iliyopo katika sakramenti, zaidi ya yote katika Ekaristi, katika Neno, katika mhudumu, na katika kusanyiko.” Mwaliko huo ni wa kugundua uzuri wa liturujia, uzuri wa upendo wa Mungu unaookoa uliodhihirishwa katika kifo na ufufuko wa Kristo, kama Papa Francisko anavyoakisi katika Waraka wake wa Kitume wa Evangelii gaudium. Kutafakari kunazua mshangao, Kardinali Parolin alisema, "kujiruhusu kulishwa na tumaini linalotoka katika Fumbo tunaloadhimisha. Hii huchochea maisha ya kiroho, kufungua mikono kupokea zawadi. Lakini ili hili litokee, liturujia lazima ijumuishe: inayoweza kuzua maajabu kwa watoto na vijana, watu wazima na wazee, watu wenye ulemavu, na wahamiaji—katika wale wote wenye njaa ya Mungu na upendo Wake. Kwa njia hiyo, liturujia inakuwa ishara ya tumaini la mwanadamu kwa Mungu na ishara ya tumaini kwa Kanisa, ambalo bado linawahesabu wengi wamtafutao Mungu.
Liturujia na majitolea
Kardinali Parolin alisema kuwa: "Liturujia huinua macho yetu mbinguni, lakini daima ndani ya uthabiti wa maisha. Ni pale tu majitoleo na maisha yanapounganishwa pamoja ndipo sherehe inakuwa chanzo cha matumaini. Kuunganisha liturujia na maisha, kutafakari na kutenda, kunatufanya kuwa “mafundi wa umoja.” Kushikilia pamoja sakramenti na ubinadamu, hutuwezesha kujibu wale wanaouliza sababu ya tumaini ndani yetu.”Kardinali Parolin alisisitiza kwamba liturujia lazima izidi kuwa mahali pa ukaribu, matumaini, uhuru, ukarimu, na kimbilio”. “Wakati mwingine, alisema, ni mahali pekee pa kukaribisha kwa kweli, kuungana badala ya kugawanyika, ambapo watu wanajitambua kama jumuiya. Kwa kutoa mfano alielekeza kwenye Parokia moja ya Familia Takatifu katika Jiji la Gaza, iliyokumbwa na milipuko ya mabomu mnamo tarehe 17 Julai 2025 ambapo watu watatu walikufa, ambapo hali hiyo inasalia kuwa mojawapo ya ishara adimu, kama si pekee za matumaini katika nchi hiyo iliyoharibiwa.” Na Karibu Wakristo 500 wanaomba na kupata hifadhi huko katika nyumba ya Mungu.
Wageni waliopitia kama njia ya Msalaba kufika Italia
“Nyumba ya sala, na kwamba inakuwa makao na kimbilio kwa watu wa Mungu na kwa wote wanaoteswa au kukandamizwa, ishara ya tumaini hakika. Katibu Mkuu wa Vatican pia alitoa wito wa kuwepo kwa liturujia ambayo inajumuisha, tamaduni, na kukaribisha katika Parokia za za Kiitaliano zinazozidi kuwa na tamaduni nyingi, liturujia ambayo ni usemi kamili wa sinodi. Alikumbuka watu wengi ambao wamefikia miji ya Italia kutoka mabara mengine, wakisafiri njia za matumaini lakini mara nyingi wakikabiliana na safari ambazo zilikuja kuwa halisi kupitia njia za Msalaba, na ambapo maombi ya wokovu yalibakia daima.
Kwa njia hiyo Kardinali alitoa wito wa kukazia fikira si mahitaji yao ya kimwili tu bali pia kiu chao cha hali ya kiroho na njaa yao ya tumaini, ambayo inatokana na imani yao kwa Mungu. Kiini cha liturujia ni amani, ni zawadi ya Kristo Mfufuka. Si ishara tu bali amani ya kweli, ushirika wa kweli. Amani hii ni matunda ya sherehe na tayari ina uzoefu ndani yake, ikienea ulimwenguni kote - na sisi ndio wabebaji wake wa kwanza. Iwapo liturujia inaadhimishwa kwa ukweli wa ndani,tunakuwa mashahidi wa matumaini na amani. Kwa kuhitimisha alisema “Ingependeza,” ikiwa kwenye mlango wa kila Kanisa mtu angeweza kusoma: “ Mmwilishwe kwa tumaini, ninyi mnaoingia humu.” Kwa maana tumaini ni Kristo Mwenyewe, aliye hai na mwenye bidii na uhai katika liturujia.