Hospitali ya Kipapa ya Bambino Gesu' yafikisha idadi ya watoto 20 kutoka Gaza!
Vatican News
Watoto watatu miongoni mwa wengine wengi waliofika kutoka huko Gaza, wakiwa na wazazi na ndugu zao, walitua jioni tarehe 13 Agosti 2025 kwenye Uwanja wa Ndege wa Ciampino, nchini Italia. Kwa hiyo wavulana wawili, wenye umri wa miezi 6 na miaka 13, na msichana wa miaka miwili walipelekwa katika Hospitali ya Kipapa la Bambini Gesu, na baada ya kukaguliwa kwenye chumba cha dharura katika Hospitali ya Watoto ya Bambino Gesù jijini Roma, mtoto mchanga alilazwa kwa ajili ya upasuaji wa jumla kufuatia kukatwa mguu hapo awali, mvulana wa umri wa miaka 13 alilazwa katika idara ya magonjwa ya mfumo wa neva kwa majeraha ya ubongo, na msichana wa miaka miwili, ambaye anaugua ugonjwa wa mfumo wa chakula, alilazwa katika wodi ya watoto kwa matibabu ya utapiamlo.
Pamoja na waliofika hawa wapya, idadi ya watoto kutoka Gaza inayotunzwa na Hospitali ya kipapa ya Bambino Gesù tangu mwanzo wa mzozo mnamo Oktoba 2023 imeongezeka hadi kufikia watoto 20. Wagonjwa wadogo wanakabiliwa na magonjwa mbalimbali kama vile: majeraha ya viungo, kuchoma, utapiamlo, magonjwa ya Saratani, ugonjwa wa moyo na kasoro za moyo wa kuzaliwa, magonjwa ya kuambukiza na ya fumo wa vyakula na ya ubongo.
Kwa mujibu wa Rais wa Hospitali ya Kipapa ya Watoto, Dk Tiziano Onesti alisema: "Kila wakati tunapokaribisha watoto kutoka sehemu zilizokumbwa na vita, tunajikuta tunakabiliwa na maisha dhaifu ambayo yanawaletea uchungu na matumaini. Maneno ya Papa Leo XIV juu ya hali mbaya ya watu walioko katika vita yanatukumbusha kwamba huruma haiwezi kuwa na hisia tu, lakini lazima iwe hatua madhubuti. Kwa sababu hii, pamoja na huduma ya matibabu, tumejitolea kuzipa familia mahali salama ambapo zinaweza kupumua kwa amani kidogo. Tunajua kwamba kwa kila mmoja wa watoto hawa, safari itakuwa na changamoto, lakini hawatalazimika kukabiliana nayo peke yao: watakuwa na jumuiya yetu ikiwa kandokando yao, pamoja na utaalamu wake na ubinadamu, kwa kuzingatia utume ambao Kitakatifu kimetukabidhi kila wakati."