杏MAP导航

Tafuta

Kauli mbiu ya mkutano wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika “Wekeza katika Malezi ya familia kama Daraja la maisha ya Furaha na Utakatifu.” Kauli mbiu ya mkutano wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika “Wekeza katika Malezi ya familia kama Daraja la maisha ya Furaha na Utakatifu.”  

Umoja wa Wanawake Wakatoliki Afrika: Mahujaji wa Imani, Matumaini na Amani

Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika kuanzia tarehe 28 Julai hadi tarehe 1 Agosti 2025 unaadhimisha Mkutano wake mkuu, Jijini Entebe, Uganda kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Wekeza katika Malezi ya familia kama Daraja la maisha ya Furaha na Utakatifu.” Mkutano umefunguliwa na Askofu mkuu Paul Ssemogerere, wa Jimbo kuu la Kampala tarehe 29 Julai 2025 kwa Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Madhabahu ya Namgongo, Uganda. Mahujaji wa imani na amani

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, - WUCWO, Entebbe, Uganda.

Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika kuanzia tarehe 28 Julai hadi tarehe 1 Agosti 2025 unaadhimisha Mkutano wake mkuu, Jijini Entebbe, Uganda kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Wekeza katika Malezi ya familia kama Daraja la maisha ya Furaha na Utakatifu.” Mkutano umefunguliwa na Askofu mkuu Paul Ssemogerere, wa Jimbo kuu la Kampala, Uganda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Walei Baraza la Maaskofu Uganda tarehe 29 Julai 2025 kwa Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Madhabahu ya Namgongo, Uganda. Naomba nianze kwa kunukuu maneno ya Kardinali Emmanuel Wamala, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kampala, Uganda yanayosema “In te Domine Speravi” – yaani, “Nimekutumainia Wewe, Bwana.” Kauli hii ya Kilatini, inayopatikana katika Zaburi 31, inaonesha imani na kumtegemea Mungu. Ndiyo maana tupo hapa leo – kwa sababu tuna tumaini katika Yesu Kristo Bwana wetu. Tumaini hili linatupa nguvu ya kuendeleza utume wetu kama wanawake ndani ya Kanisa Katoliki. Historia ya Ushiriki wa Wanawake wa Kikatoliki katika Kanisa: Ni nafasi gani wanawake wa Kikatoliki walichukua? Shirikisho la WUCWO (Umoja wa Mashirika ya Wanawake Wakatoliki Duniani) ndilo lilikuwa la kwanza kuwasilisha ombi rasmi kwa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Ombi hilo likawa mfano kwa mashirika mengine ya wanawake kuwasilisha hoja zao, na kwa njia hiyo sauti na mahitaji ya wanawake yakasikika katika majadiliano ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Wajumbe wakifuatilia mada wakati zinawasilishwa
Wajumbe wakifuatilia mada wakati zinawasilishwa

Miaka ya 1963–1964, wanawake wa Kikatoliki walisafiri hadi Roma – kama mahujaji, walikutana na Maaskofu wao, walishiriki Ibada ya Misa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, na hata baadhi ya Maaskofu waliwashirikisha katika mijadala. Baadhi ya wanawake waliingia kwenye kamati ndogo zilizotayarisha sura mbalimbali za hati ya “Gaudium et Spes” yaani “Kanisa Katika Ulimwengu Mamboleo.” Watawa walikuwa miongoni mwa waangalizi wa walei na walichangia kuandaa katika hati ya “Perfectae caritatis” kuhusu Maisha ya wakfu. Mashirika ya kitawa yaliwakaribisha washiriki katika nyumba zao za wageni – jambo lililoimarisha mazingira ya upendo na mshikamano. Wakuu wa mashirika ya kitawa na kazi za kitume waliwavutia hata maaskofu kwa mafundisho yao.

Wanawake wakatoliki walishirikishwa vyema katika Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican
Wanawake wakatoliki walishirikishwa vyema katika Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican

Nini kilikuwa kilio kikuu cha wanawake wakati wa Mtaguso? WUCWO, kwa niaba ya wanawake wapatao milioni 36, iliwasilisha ombi lao la kwanza mwaka 1960, likisisitiza umuhimu wa kupyaisha: Utu, haki na heshima ya mwanamke, pamoja na nafasi yake katika familia, jamii na Kanisa katika ujumla wake.  Mama zangu, rafiki na dada wapendwa katika Kristo, tafakari hii ya kihistoria inatukumbusha kuwa kile kilichoanzishwa, kilichopangwa na kutekelezwa na waliotutangulia, sisi leo tunakienzi na kukiendeleza. Tunaendeleza uinjilishaji wa kina ulioshuhudiwa kwa macho ya imani na maisha safi ya wana wa Mungu. Nukuu ya Wito wa Papa Paulo VI kwa Wanawake. Mtakatifu Paulo VI alisema: “Na sasa tunawageukia ninyi wanawake wa kila hali – wasichana, wake, mama, wajane; pia bikira walioweka nadhiri na wanawake wanaoishi peke yao – ninyi mnaunda nusu ya familia kubwa ya wanadamu.” Aliendelea kusema: “Kama mjuavyo, Kanisa lina fahari kuwa limeinua na kumkomboa mwanamke, na limeonesha usawa wake wa msingi na mwanamume. Lakini saa imefika – na kwa kweli imefika – ambapo wito wa mwanamke unafikiwa kwa ukamilifu wake, saa ambapo mwanamke anapata ushawishi na nguvu ambazo hazijawahi kuonekana awali.” Wito huo ni wa sasa – Kanisa la kimisionari na kisinodi linatuita sote – walei na maklero – tutembee pamoja kama familia moja ya Mungu. Tumshangilie Mungu kwa furaha na tutumike kwa unyenyekevu.

Wajumbe wa WUCWO kutoka Tanzania
Wajumbe wa WUCWO kutoka Tanzania

Wanawake Tumepewa Upendeleo na Mungu: Sisi wanawake tumependelewa Kushiriki katika kazi ya uumbaji kwa namna ya tofauti, tumekabidhiwa jukumu la kulinda familia, kuumba nafsi, ubongo katika siku za mwanzo kabisa za uumbaji wa mtoto akiwa tumboni na hata anapozaliwa wakati wa kunyonyesha. Tunapobeba mimba, kwa hakika tunashiriki moja kwa moja katika kazi ya uumbaji wa Mungu, zawadi ya ajabu sana! Wapendwa Mama zangu/ dada zangu, kwa kukubali zawadi hii, tunakuwa wake, mama wa familia, na walimu wa kwanza wa jamii ya binadamu ndani ya jukwaa la familia. Tujue kuwa kwa kupitia watoto wetu, sisi mama, tunahusiana moja kwa moja na mustakabali ambao huenda tusiuone. Hivyo basi, na tuijenge dunia hii iwe mahali pazuri zaidi pa kuishi kulingana na kusudi la Mungu.

WUCWO: Utu, heshima na haki msingi za wanawake
WUCWO: Utu, heshima na haki msingi za wanawake

Kwenu watawa na wanawake mnaoishi maisha ya Wakfu: Kwenu watoto wetu mnaoishi maisha ya wakfu na mliojitolea kumfuta Yesu machozi, tunajua kuwa jamii ya leo inawahitaji kwa namna ya kipekee. Familia nyingi haziwezi kuishi bila msaada wa wale wasio na familia. Ninyi mlioweka nadhiri, katika dunia hii inayotawaliwa na ubinafsi na tamaa ya starehe, tunawaombea na tunamwomba Mwenyezi Mungu awalinde katika maisha yenu ya: Utii, Ufukara, Usafi wa moyo, kujitolea na ibada. Hitimisho: Ninapenda kuwaalika kila mmoja wetu kushiriki kikamilifu katika ratiba ya mkutano huu ambayo imetufanya kuwa hapa Uganda. Tusikilize na kusikilizana kwa umakini, tumsikilize Roho Mtakatifu na tushirikishane kwa moyo wa kujali, ili kuimarisha utume wetu ndani ya Kanisa duniani kote. Na Bi, Evaline Malisa Ntenga, Rais WUCWO, Kanda ya Afrika.

Mama Evaline Ntenga Malisa Ntenga, Rais Wanawake kanda ya Afrika.
Mama Evaline Ntenga Malisa Ntenga, Rais Wanawake kanda ya Afrika.

UJUMBE KUTOKA KWA MONICA SANTAMARINA RAIS Wa UMOJA WAKATOLIKI DUNIANI (WUCWO- WORLD UNION OF CATHOLIC WOMEN’S ORGANISATION) Mkutano wa Kanda ya Afrika – Entebbe, Uganda, 28 Julai – 1 Agosti 2025

Wapendwa katika Kristo, kwa furaha kuu na moyo wa matumaini, nawakaribisha kwa upendo wote nyote mliokusanyika hapa Entebbe, Uganda kwa ajili ya Mkutano wa Kanda ya Afrika wa WUCWO wa mwaka 2025. Huu ni wakati wa kutafakari tena juu ya utambulisho na utume wetu kama wanawake Wakatoliki wa Afrika tukiwa wamoja katika imani, tukijitolea kwa ajili ya uinjilishaji, maendeleo ya binadamu na utetezi wa wasio na sauti. Wanawake wa Afrika ni waleta matumaini, wenye ustahimilivu, uhai, na mshikamano wa kina wa kijamii hata wanapokabiliana na changamoto kubwa kama vile umaskini, ukatili na uharibifu wa mazingira. Umuhimu wa Mkutano Huu. Afrika ni bara la matumaini, moja ya mabara machache ambako Kanisa Katoliki linaendelea kukua kwa kasi. Ni bara lenye uhai na lililotunza asili yake, lakini pia linakumbwa na baa la njaa, vita, unyonyaji wa rasilimali na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ni bara lenye wanawake jasiri lakini pia ni bara ambalo wanawake wengi bado ni waathirika wa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

Wanawake ni mahujaji wa imani, matumaini na mapendo
Wanawake ni mahujaji wa imani, matumaini na mapendo

Nimevutiwa na kaulimbiu kuu za mkutano huu: “Wanawake, Walezi wa Mama Dunia. Wekeza katika malezi ya familia kama Daraja la maisha ya furaha na utakatifu.” Ukatili na Ubaguzi Dhidi ya Wanawake Barani Afrika Kauli mbiu hizi zinaendana na vipaumbele vya WUCWO kwa kipindi cha 2023–2027 ambazo ni pamoja na: Kupanua Uangalizi wa Wanawake na wale wote wanaopitia nyanyaso chini ya mradi wa (World Women Observatory - WWO), Kukuza uhuru wa kidini na majadiliano ya kiekumene; Kukabiliana na baa la njaa na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote (Laudato si’); Kuilinda familia na kuimarisha wito wa ndoa na uzazi –(Amoris laetitia) ; Kuwawezesha wanawake kushiriki katika ujenzi wa Kanisa la Sinodi na Kimisionari Wanawake, Walezi wa Mama Dunia: Wanawake wa Afrika wameonesha uongozi wa kuvutia katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa: kupanda miti, kusafisha maeneo yao na kushiriki harakati za “Laudato si.’ Hata hivyo, bado kuna haja ya kuongeza juhudi zaidi. Papa Leo XIV anatukumbusha kuwa sisi ni “mbegu za amani na matumaini,” na kutunza kazi ya uumbaji ni wajibu wa kiimani na wa kimaadili.

Mama Monica Santamarina, Rais wa WUCWO Duniani
Mama Monica Santamarina, Rais wa WUCWO Duniani

Wekeza katika malezi ya familia kama Daraja la maisha ya furaha na utakatifu. Katika Ulimwengu mamboleo ambapo vijana wanaogopa kuingia katika Sakrament ya ndoa, ni lazima kupyaisha tena wito wa ndoa na familia. Kumbe, Kanisa linapaswa: Kutoa msaada kwa kila hatua ya maisha—kuanzia ujana hadi uzee; Kukuza utakatifu wa upendo wa kibinadamu na usafi wa moyo; Kuhimiza sera zinazowezesha familia kukua na kustawi; Kutoa mafunzo kwa viongozi wa kidini na waamini walei ili waelewe maana ya maisha halisi ya familia; Kukuza jumuiya jumuishi kati ya vizazi mbalimbali. Familia si wapokeaji tu wa imani, bali ni wahusika wakuu wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kila tendo la kifamilia—kuanzia sala za pamoja hadi kushiriki changamoto na mateso kwa pamoja ni kielelezo cha Injili hai. Kanisa linapaswa kuwa karibu zaidi na familia, hasa zile zinazolelewa na mzazi mmoja, kwa njia ya kuzisikiliza na kuandana nazo.

Wanawake wa Afrika ni wajumbe na vyombo vya matumaini
Wanawake wa Afrika ni wajumbe na vyombo vya matumaini

Ukatili na Ubaguzi Dhidi ya Wanawake: Utafiti wa WUCWO kupitia mradi wa Uangalizi wa Wanawake wanaopitia manyanyaso chini ya mradi wa (World Women Observatory - WWO), umeonesha kuwa takriban 67% ya wanawake 10,680 walioshiriki utafiti kutoka nchi 36 Afrika wameshuhudia ukatili wa kijinsia. Maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni ukatili wa nyumbani, wa kiuchumi, na ubaguzi wa kielimu. Kwa kushirikiana na Hilton Foundation, WUCWO imeanzisha mtandao wa bara zima wa kupambana na changamoto hizi, ambao unahusisha: Wasimamizi wa jamii katika nchi 22; Mashirika ya kidini na ya kiraia zaidi ya 60; Ujenzi wa uwezo na ufadhili wa miradi; Kampeni ya #InvisibleNoMore yenye mabalozi 750 duniani kote. Lengo ni kuwawezesha wanawake, kueneza uelewa, na kushiriki mbinu bora zaidi zinazotoa matumaini na suluhisho la kweli. Hitimisho: Licha ya changamoto hizi zote, tunamtumaini Bwana Yesu Kristo na mshikamano wetu chini ya ulinzi na tunza ya Mama Bikira Maria, Malkia wa Amani. Katika mwaka huu wa Jubilei, tukutane, tusikilizane, tuombe, na tujenge matumaini pamoja. Toka Entebbe, tuondoke tukiwa na moyo mpya wa kupanda mbegu za amani, haki na matumaini kila mahali tunapoitwa na kutumwa. Sala zetu na juhudi zetu ziendelee kubadilisha maisha na jamii Barani Afrika. Kwa mshikamano na imani, mimi ni Mónica Santamarina Rais wa – WUCWO Duniani.

Wanawake Wakatoliki Afrika
31 Julai 2025, 16:30