杏MAP导航

Tafuta

Ujumbe wa Dominika ya Utume wa Bahari tarehe 13 Julai 2025 unanogeshwa na kauli; “Mahujaji wa matumaini, Madaraja ya Kuwakutanisha Nchi Maadui, Manabii wa Amani.” Ujumbe wa Dominika ya Utume wa Bahari tarehe 13 Julai 2025 unanogeshwa na kauli; “Mahujaji wa matumaini, Madaraja ya Kuwakutanisha Nchi Maadui, Manabii wa Amani.”  

Tarehe 13 Julai 2025 Ni Dominika ya Utume wa Bahari: Mahujaji wa Matumaini na Amani

Ujumbe wa Dominika ya Utume wa Bahari tarehe 13 Julai 2025 unanogeshwa na kauli; “Mahujaji wa matumaini, Madaraja ya Kuwakutanisha Nchi Maadui, Manabii wa Amani.” Kwa hakika bahari ni kiungo muhimu sana kwa Jumuiya ya Kimataifa, changamoto ni kuwa na mwelekeo wa kudumisha amani badala ya kuendekeza vita. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na wahitaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa Dominika tarehe 13 Julai 2025 anaadhimisha Dominika ya Utume wa Bahari, fursa kwa Familia ya Mungu sehemu mbalimbali za dunia, kumshukuru Mungu kwa huduma na mchango mkubwa, unaotolewa na mabaharia pamoja na wavuvi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni siku maalum ya kutambua na kuthamini sadaka ya watu hawa ambao wakati mwingine: haki, utu na heshima yao vinahatarishwa kutokana na changamoto mbalimbali, wanazokumbana nazo wakati wa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa jamii. Hii ni siku maalum ambayo Kanisa linatambua mchango mkubwa unaotolewa na Mabaharia pamoja na wavuvi katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika nyanja mbalimbali za maisha. Maadhimisho haya pia yana mwelekeo wa kiekumene, kwani yanawashirikisha Wakristo kutoka katika Makanisa na madhehebu mbalimbali ya Kikristo, ili kuonesha moyo wa upendo na mshikamano na mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Utume wa Bahari, “Apostolatus Maris” unaojulikana na wengi kama “Stella Maris” ulianzishwa tarehe 4 Oktoba 1920 na waamini walei wanaoshiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu unaopata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo. Ni jukumu na wito wa waamini walei kuutafuta Ufalme wa Mungu wakiyashughulikia mambo ya dunia, na kuyaelekeza kadiri ya mpango wa Mungu. Wanaitwa kuyatimiza majukumu yao wenyewe wakiongozwa na roho ya Kiinjili, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa imani, matumaini na mapendo thabiti! Ili kuonesha na kushuhudia ukaribu wa Kanisa kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao, Papa Pio XI tarehe 17 Aprili 1922 akaridhia kuanzishwa kwa Utume wa Bahari “Apostolatus Maris.” Leo hii kuna jeshi kubwa la watu wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwadumia mabaharia na wavuvi katika bandari 300 kwa kutembelea meli zisizopungua 70,000 kwa mwaka.

Mabaharia ni mahujaji wa matumaini na amani
Mabaharia ni mahujaji wa matumaini na amani   (ANSA)

Mama Kanisa anawashukuru kwa dhati Mitume hawa wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Wadau wa Utume wa Bahari wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji wa kina kwa kuwafunulia watu wa Mungu, ile sura pendelevu ya Mama Kanisa: kwa kuonesha ukaribu wake kwa watu watakatifu wa Mungu, na hivyo kuwahamasisha kujisikia kuwa ni sehemu hai ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Takribani miaka 100 iliyopita, imekuwa ni kipindi muafaka cha ujenzi wa misingi ya majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, kutokana na mwingiliano wa watu kutoka katika dini, tamaduni na Mataifa mbalimbali duniani. Ujumbe wa Dominika ya Utume wa Bahari tarehe 13 Julai 2025 unanogeshwa na kauli; “Mahujaji wa matumaini, Madaraja ya Kuwakutanisha Nchi Maadui, Manabii wa Amani.” Kwa hakika bahari ni kiungo muhimu sana kwa Jumuiya ya Kimataifa, changamoto na mwaliko wa kuwa na mwelekeo mpana zaidi, kwa kudumisha amani badala ya kuendekeza migogoro, mipasuko na vita. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Rej. Gaudium et spes, 1. Huu ni ujumbe mahususi kwa watu wa Mungu, Waraka huu wa Kanisa Katika Ulimwengu Mamboleo, kwa mwaka 2025 unapoadhimisha kumbukizi ya miaka 60 tangu kuchapishwa kwake. Mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao, kamwe wasijisikie pweke, katika mchakato wa kutafuta haki, utu, heshima na furaha ya kweli. Maendeleo fungamani ya binadamu ni mchakato unaowakumbatia na kuwaambata watu wote: kimwili, kiroho na katika mwelekeo wa kijumuiya. Mahali ambapo Injili inatangazwa, inamshuhudia na kumkaribisha Kristo Mfufuka, lazima kunatokea mabadiliko na Ulimwengu hauwezi kubaki kama ulivyo, kwa sababu Yule aliyeshinda dhambi na mauti anasema, “Tazama, nayafanya yote kuwa mapya.” Ufu 21:5.

Wavuvi wanachangia sana kwenye mchakato wa kukuza uchumi
Wavuvi wanachangia sana kwenye mchakato wa kukuza uchumi

Katika maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, Wakristo kutoka sehemu mbalimbali za dunia wanaalikwa kutangaza na kushuhudia uwepo endelevu na angavu wa Ufalme wa Mungu kwa ari na moyo mkuu. Huu pia ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani; muda wa kuvunjilia mbali minyororo inayowafunga watu; ni muda muafaka wa kusamehe madeni; kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na mgawanyo wa haki wa rasilimali za dunia, kwa watu kukutana katika amani kwa ujasiri, kama kitendo cha ubinadamu, tayari kupyaisha tena Injili ya matumaini. “Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona.” 1Yn 4:20. Kanisa linaalikwa kuangalia jinsi ambavyo linatekeleza dhamana na wajibu wake bandarini na kwenye meli; haki msingi za mabaharia, mazingira ya kazi pamoja na huduma zipi za maisha ya kiroho zinaweza kutolewa. Katika ulimwengu uliojeruhiwa, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inaendelea kuongezeka maradufu na kwamba, upendo kwa Mungu kwa njia ya maisha unapaswa kusimikwa katika maisha yenyewe. Maisha ni tunu muhimu sana na kwamba, yanapaswa kumwilishwa katika ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya kibinadamu, ili hatimaye, yaweze kuwa ni kikolezo cha uhuru, vinginevyo maisha yatamfunga mtu; maisha yamwendeleze mtu vingevyo yatamdhalilisha. Mabaharia ni watu wanaojisadaka kila siku ya maisha yao kukuza na kudumisha uchumi, lakini ni watu wanaofaidika kidogo sana.

Utume wa Bahari 2025
Utume wa Bahari 2025   (2025 Getty Images)

Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa ajili ya Mabahari, Wavuvi pamoja na Familia zao, yananogeshwa na kauli mbiu mahujaji wa matumaini, dhana inayowajumuisha watu wote bila ya ubaguzi wa dini au madhehebu ya mtu, hapa jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapewa kipaumbele cha kwanza; hawa ni watu wanaosafiri katika Injili ya maisha na kwamba, matumaini linapaswa kuwa ni lengo kuu, ili utu, heshima na haki msingi za Mabaharia na wavuvi ziheshimiwe na kuthaminiwa na kwamba, haya ndiyo matumaini ya watu hawa. Huu ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu wanajenga na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Tamko la Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 Hii ni changamo ya kujishikamanisha na kuambatana na upendo wa Mungu, kwani hakuna kitu chochote kinachoweza kuwatenga wat una upendo wa Mungu. Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, anahitimisha ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Dominika ya Utume wa Bahari kwa kuwashukuru Mabaharia na wavuvi wote kwani wao ni; “Mahujaji wa matumaini, Madaraja ya Kuwakutanisha Nchi Maadui, Manabii wa Amani.” Ni mahujaji wa matumaini wanapotekeleza dhamana na wajibu wao kwa uangalifu na upendo mkubwa; wanapodumisha mshikamano wa upendo pamoja na familia na jumuiya zao; wakati wote wanapokabiliana na changamoto ya ukosefu wa haki msingi za binadamu. Kwa hakika wawe ni madaraja ya kuwakutanisha nchi maadui na manabii wa amani. Bahari inaziunganisha nchi zote, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupanua wigo wao na hivyo kujisikia kuwa ni wamoja, ili kuzuia kinzani na mipasuko ya kijamii. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kujikita katika wongofu. Bikira Maria Nyota ya Bahari, awaongoze na kung’arisha matumaini yao!

Utume wa Bahari 2025
10 Julai 2025, 16:41