杏MAP导航

Tafuta

Familia ya Damu Azizi ya Yesu, inaadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo: Mahujaji wa matumaini katika Damu Azizi ya Yesu, Uhai na Wokovu wa Ulimwengu. Familia ya Damu Azizi ya Yesu, inaadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo: Mahujaji wa matumaini katika Damu Azizi ya Yesu, Uhai na Wokovu wa Ulimwengu. 

Sherehe ya Damu Azizi ya Yesu, Jubilei ya Mwaka 2025: Agano Jipya na la Milele

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, katika mahubiri yake amejikita katika Agano Jipya na la Milele, kielelezo cha umainifu wa Mungu na ushirika kwa watu wake Israeli; Kristo Yesu anatoa Mwili na Damu yake Azizi, kama kielelezo cha hali ya juu cha uaminifu wa binadamu kwa Mungu na kwamba, Damu Azizi ya Kristo Yesu ni chemchemi ya upatanisho, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa katika upendo na huruma yake kuu, ametenga mwezi Julai kwa ajili ya kukuza na kudumisha Ibada kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu, Mto wa rehema, shule ya utakatifu, haki, upendo na msamaha. Damu Azizi ya Kristo ni chemchemi ya upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu. Hii ni Ibada ambayo inaenezwa kwa namna ya pekee kabisa na: Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., Shirika la Masista Waabuduo Damu Azizi ya Yesu, ASC, Mashirika ya Kitawa pamoja na waamini walei. Fumbo la huruma na upendo wa Kristo Yesu limekuwa ni kivutio kikubwa cha waamini na waanzilishi wa Mashirika ya Kitawa kama vile Mtakatifu Gaspari del Bufalo na Mtakatifu Maria de Mathias, kiasi kwamba, fumbo hili la upendo na huruma ya Mungu limekuwa ni msingi wa maisha na utume wa Mashirika haya. Damu Azizi ya Kristo ni chemchemi ya: Uhai na wokovu wa ulimwengu na kwamba, ni alama ya juu kabisa inayoshuhudia upendo na sadaka ya maisha kwa ajili ya wengine. Sadaka hii inajirudia tena na tena katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, kiasi cha Kristo Yesu kuwakirimia waamini Mwili na Damu yake Azizi; Damu ya Agano Jipya na la milele, iliyomwagika kwa ajili ya maondoleo ya dhambi, maisha na uzima wa milele. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kujitambua kama watu waliotiwa muhuri ili kushiriki katika: maisha na utume wa Kristo Yesu, ili waweze kuwa ni mwanga na baraka inayofufua na kupyaisha; mwanga unaoponya na kumweka mtu huru; tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Waamini wawe tayari kuwashirikisha jirani zao, tunu na ukarimu unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; ni mtakatifu wa Mungu anayestahili kuonjeshwa upendo wa dhati. Rej. Evangelii gaudium 273-274.

Mahujaji wa matumaini kutoka Tanzania
Mahujaji wa matumaini kutoka Tanzania

Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Wamisionari wa Shirika ya Damu Azizi ya Yesu, Vyama vya Kitume pamoja na Familia ya Damu Azizi ya Yesu, wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Mahujaji wa matumaini katika Damu Azizi ya Yesu, uhai na wokovu wa ulimwengu.” Maadhimisho haya yameanza, Jumatatu tarehe 30 Juni 2025 kwa Mkesha wa kimataifa wa sala ukiongozwa na Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo,” Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma na kilele chake ni tarehe Mosi Julai 2025 kwa Ibada ya Misa Takatifu ambayo imeongozwa na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Mahujaji wa matumaini 57 kutoka Tanzania, ambamo wamo Mapadre 7, Watawa 5 pamoja na idadi kubwa ya waamini walei, wanaendelea kushiriki katika maadhimisho haya, kama sehemu ya hija maalum ya Damu Azizi ya Kristo Yesu.

Ibada ya Misa Takatifu Sherehe ya Damu Azizi ya Yesu
Ibada ya Misa Takatifu Sherehe ya Damu Azizi ya Yesu

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, katika mahubiri yake amejikita katika Agano Jipya na la Milele, kielelezo cha umainifu wa Mungu na ushirika kwa watu wake Israeli; Kristo Yesu anatoa Mwili na Damu yake Azizi, kama kielelezo cha hali ya juu cha uaminifu wa binadamu kwa Mungu na kwamba, Damu Azizi ya Kristo Yesu ni chemchemi ya upatanisho wa watu wa Mungu, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, amewashukuru Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, watawa, vyama vya kitume kwa kukuza na kudumisha Ibada kwa Damu Azizi ya Yesu, chemchemi ya Agano Jipya na la milele. Agano ni neno linalotumika katika medani mbalimbali za maisha ya binadamu, lakini jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, vita, kinzani na mipasuko mbalimbali ikijitokeza katika ulimwengu mamboleo, kwa hakika watu washindwa kuishi maagano yao. Maadhimisho ya Sherehe ya Damu Azizi ya Yesu ni mwaliko kwa waamini kuwa ni wamisionari wa kweli wa Agano Jipya na la milelel, lililofungwa kwa damu Azizi ya Kristo Yesu.

Kardinali Tagle akiongoza Ibada ya Misa Takatifu Sherehe ya Damu Azizi
Kardinali Tagle akiongoza Ibada ya Misa Takatifu Sherehe ya Damu Azizi

Agano la Kale lilikuwa ni kati ya Mwenyezi Mungu na Israeli, aliyepaswa kuwa mwaminifu kwa Neno la Mungu, kielelezo maalum cha umuhimu wa Agano, ambalo watu walitumia damu ya wanyama kufunga Agano, kwani damu ni kielelezo cha uhai unaowashirikisha watu wa Mungu hatima yao ya maisha. “nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni Bwana, Mungu wenu, niwatoaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri.” Kut 6:7. Kwa hakika Mungu Mwenyezi amekuwa mwaminifu kwa Neno lake na ushirika wake kwa Israeli, lakini Israeli kwa upande wake, alikengeuka na kuliacha Agano na Mungu, akamtolea Mungu sadaka ya damu ya wanyama. Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na asili ya Agano Jipya na la Milele; kielele cha uaminifu wa mungu kwani Kristo Yesu anayamimina maisha yake kama sadaka safi mbele ya Mungu na kwa kazi ya uumbaji. Damu Azizi ya Kristo Yesu ni kielelezo cha maisha; Damu inayomwagika kwa ajili ya Agano jipya na la milele, hii ni Damu iliyomwagika bila ya kujibakiza hata kidogo.

Familia ya Damu Azizi ya Yesu katika Ibada ya Misa Takatifu
Familia ya Damu Azizi ya Yesu katika Ibada ya Misa Takatifu

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, anakaza kusema, Damu Azizi ya Kristo Yesu ni chimbuko la Jumuiya mpya iliyopatanishwa na Mungu, kwa njia ya Kristo Yesu, wafuasi wake kutoka katika: Mataifa na tamaduni na watu mbalimbali, wanafungamanishwa kwa pamoja kama familia moja. Agano Jipya linatoa mwelekeo wa kuwaangalia wengine kwa huruma na upendo, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu anawapenda na Yesu ni kiungo cha wafuasi wake wanaounda Jumuiya ya Kikristo, changamoto na mwaliko kwa waamini kulilinda, kulitunza na kulilisha Kanisa la Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. Rej. Mdo 20:28. Kwa Damu yake Azizi, Kristo Yesu amevunjilia mbali nguvu za dhambi na mauti na hivyo kuwafanya kuwa ni jirani na ndugu wamoja. Kila mtu ana thamani kubwa mbele ya Mungu na anahitaji kupendwa na wote.

Wamisionari wa C.PP.S na ASC wakisubiri kuhudhuria Masifu ya Jioni
Wamisionari wa C.PP.S na ASC wakisubiri kuhudhuria Masifu ya Jioni

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, amewataka waamini kusimama kidete, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbwa katika tabia ya watu kupoteza maisha kwa kujinyonga, kwa njia ya vita, baa la njaa; ujinga na maradhi. Kuna tabia ya ubaguzi na ukosefu wa haki msingi pamoja na udhalilishaji wa utu, heshima na haki msingi za binadamu; mambo yanayokwenda kinyume kabisa cha Agano Jipya na la Milele lililotekelezwa na Kristo Yesu. Jumuiya za Kikristo zijitahidi kuwa ni kielelezo cha ukarimu wa kidugu na upendo usiokuwa na mipaka. Sherehe ya Damu Azizi ya Yesu inatoa changamoto ya kujenga na kudumisha umoja na usawa, badala ya kuwainua baadhi ya watu katika jamii na kuwatweza wengine. Kwa watu wanaotamani kupata matumaini, basi Damu Azizi ya Kristo Yesu izime kiu na matamanio yao kwa sababu hii ni Damu ya Agano Jipya kati ya Mungu na binadamu.

Sherehe Damu Azizi ya Yesu

 

01 Julai 2025, 16:50