杏MAP导航

Tafuta

Rehema kamili zitatolewa kwa watawa wa Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na Watu wote wa Mungu kuanzia tarehe 16 Julai 2025 hadi 3 Julai 2026 Rehema kamili zitatolewa kwa watawa wa Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na Watu wote wa Mungu kuanzia tarehe 16 Julai 2025 hadi 3 Julai 2026 

Rehema Kamili Kutolewa Wakati wa Jubilei ya Miaka 100 ya Masista Wakarmeli

Papa Leo XIV ametoa ruhusa kwa Wakarmeli na watu wa Mungu kuweza kupata rehema kamili katika mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Miaka 100 tangu Mt. Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu alipotangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Pio XI tarehe 17 Mei 1925 sanjari na Jubilei ya Miaka 100 tangu Shirika la Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mt. Theresa wa Mtoto Yesu walipounganishwa katika familia kubwa ya Karmelitarehe 3 Julai 1925.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mafundisho ya imani na ibada ya rehema katika Kanisa yameunganika kabisa na matunda ya Sakramenti ya Upatanisho. Kanisa linafundisha kwamba, Rehema kamili ni msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu wa adhabu za muda kwa ajili ya dhambi ambazo kosa lao limekwishafutwa. Huu ni msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata baada ya kutimiza mashari yaliyotolewa na Mama Kanisa, kwa tendo la Kanisa ambalo likiwa ni mgawaji wa ukombozi hutumia kwa mamlaka yake hazina ya malipizi ya Kristo Yesu na ya watakatifu wake. Rehema imegawanyika katika sehemu kuu mbili: Rehema Kamili au Rehema ya Muda kutokana kwamba, inaondoa au sehemu au adhabu yote kabisa ya muda inayotakiwa kwa sababu ya dhambi. Kila mwamini anaweza kupata rehema kwa ajili yake mwenyewe au kwa ajili ya marehemu wake kama atatimiza yafuatayo: Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa. Pili, apokee Sakramenti ya Upatanisho. Tatu, apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa rehema kamili. Nne, asali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu Leo XIV. Mwishoni atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa rehema kamili.

Sr. Maria Lilian Kapongo Mama Mkuu wa Shirika
Sr. Maria Lilian Kapongo Mama Mkuu wa Shirika

Ni katika muktadha huu wa rehema kamili, Hakimu mkuu wa Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume: "Penitenzieria Apostolica", kwa niaba ya Kardinali Angelo De Donatis Mhudumu mkuu wa Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume, amemwandikia Sr. Maria Lilian Kapongo, Mama mkuu wa Shirika la Masista Wakarmeli Wamisionari wa Theresa wa Mtoto Yesu kuhusu ruhusa iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV kwa watawa na watu wa Mungu katika ujumla wao kuweza kupata rehema kamili katika mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Miaka 100 tangu Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu alipotangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Pio Pio XI tarehe 17 Mei 1925 sanjari na Jubilei ya Miaka 100 tangu Shirika la Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu walipounganishwa katika familia kubwa ya Karmeli O. Carm, tarehe 3 Julai 1925.

Watu wote wa Mungu watakaotimiza masharti kupewa Rehema Kamili
Watu wote wa Mungu watakaotimiza masharti kupewa Rehema Kamili

Maadhimisho ya Jubilei hii yananogeshwa na kauli mbiu: “Kumpenda Yesu na kumfanya Apendwe kwa Kukarabati Ubinadamu Uliojeruhiwa: Mahujaji wa matumaini kuelekea Utakatifu,” ?Fadhili za Bwana nitaziimba milele, kwa kinywa changu, nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.” (Zab 89:2). Kumbe, rehema hii inatolewa kuanzia tarehe tarehe 16 Julai 2025, Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli hadi tarehe 3 Julai 2026 Sikukuu ya Mtakatifu Thoma, Mtume. Watawa na watu wa Mungu katika ujumla wao, kwa kutekeleza masharti ya kuweza kupata rehema kamili, wanaweza kuwakumbuka na kuwaombea marehemu wao, katika Kikanisa cha Nyumba Mama kichopo San Marinella, Jimbo Katoliki la Porto-Santa Rufina, lililoko nchini Italia, mahali ambapo Masalia ya Mwenyeheri Mama Maria Krochifissa Kurcio yamehifadhiwa au katika Kikanisa chochote kilichoko kwenye nyumba ya Shirika la Masista Wakarmeli Wamisionari wa Theresa wa Mtoto Yesu.

Mahujaji wa Matumaini kuelekea Utakatifu
Mahujaji wa Matumaini kuelekea Utakatifu

Kumbe, Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume: "Penitenzieria Apostolica", kwa niaba ya Baba Mtakatifu Leo XIV linayo furaha kutoa rehema kamili, kwa wakristo waaminifu ambao katika uzee au magonjwa yao, hawawezi kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Jubilei yao, waoneshe moyo wa kuchukia kutenda dhambi, watoe sadaka pale inapowezekana na wajitahidi kuunganishwa kiroho katika maadhimisho ya Jubilei hii, huku wakitolea mateso na mahangaiko yao kwa Mwenyezi Mungu.

Rehema Kamili
17 Julai 2025, 17:14