Jubilei ya Wamisionari wa Kidijitali Kikatoliki na Washawishi washirikishana matumaini
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika sehemu ya Jubilei ya Vijana, tarehe 28-29 Julai 2025 kuna pia Jubilei ya Wamisionari na Washawishi wa Kidijitali inayohamasishwa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Mawasiliano, ambapo wameweza kulta kwa pamoja wale wanaoinjilisha kupitia mtandaoni ili kutafakari, kusali na kusherehekea pamoja kama Kanisa moja lisilo na mipaka. Katika hotuba yake ya ufunguzi wa hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa njia ya Conciliazione, Jijini Roma, Dkt. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, aliwakaribisha washiriki wote huku akiwaalika katika nafasi Takatifu ya kusikiliza na kukutana. "Inapendeza kuwa pamoja ana kwa ana, alisema, huku akibainisha kwamba ingawa majukwaa ya kidijitali yanatuunganisha, kinachotufunga kweli si wavuti, lakini kitu kinachotushinda: Mungu Mwenyewe.
Dk. Ruffini alitafakari juu ya ukweli kwamba "Kanisa daima limekuwa mtandao, kwa muda mrefu kabla ya mtandao wa sasa wa kidijitali kuwepo, na kwamba mtandao huu haujatengenezwa kwa kanuni au maudhui, bali ni watu, wasio wakamilifu, wa aina mbalimbali, lakini wameunganishwa kwa ubatizo mmoja na imani moja. Aliwataka kwa njia huo waliohudhuria kupinga vishawishi vya kujikweza na kujiona walio juu juu, na badala yake watafakari utume wao kwa unyenyekevu. Dk. Ruffini akimnukuu Papa Franciskp aliyeuliza maswali yenye nguvu kwamba: je "Tunapandaje tumaini katikati ya kukata tamaa? Je, tunaponyaje migawanyiko? Je, mawasiliano yetu yanatokana na maombi, au tumejiruhusu kutumia lugha ya biashara ya soko?" Haya yote si maswali rahisi, lakini ni muhimu kwa yeyote anayetaka kutangaza Injili katika utamaduni wa kisasa wa kidijitali, katika nafasi iliyojaa uwezo, lakini pia yenye hatari kubwa: “Acheni tushuhudie kwamba inawezekana tusisombwe na wimbi hili,” na aliwatia moyo kwamba : “Na tutupe wavu upande mwingine.”
Kwa upande wake Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican katika, hotuba yake kwa wasikilizaji alitoa wito wa kuunganishwa na tumaini. "Katika enzi ambapo habari potofu, ubaguzi, na kutengwa kunaweza kutawala mazungumzo ya mtandaoni, wamisionari wa kidijitali, wanaitwa kutoa kitu tofauti yaani nuru ya Kristo. Sio waundaji wa maudhui bali wao ni mashubuda alisema na kwamba “siyo tu kwamba mnajenga majukwaa; bali mnajenga madaraja." Kardinali Parolin alisisitiza kwamba uwepo wa Wakristo mtandaoni lazima udhihirishwe na ukweli, upendo na unyenyekevu, kwa lengo la kukuza utamaduni wa kukutana. "Hata chapisho fupi, linaposhirikishwa katika imani na upendo, linaweza kuwa cheche ya neema. Kwa njia hiyo Kardinali Parolin aliwahimiza washawishi kubaki na mizizi katika sala, Maandiko, na sakramenti, wakipata nguvu kutoka katika jumuiya ya Kanisa.
Kardinali Parolin kadhalika alisema kuwa: “Katika hali kama hiyo, utume wa Kanisa huwezi kusimama au kushtukiza.Huo unakaa katika uwezo wa kutoa, kwa njia ya kukutana na Mungu maana, na mwelekeo. Wakati huo huo, unahitahiji tabia makini, iliyo hai, majadiliano na utume, wenye uwezo wa kujua kusoma alama za nyakati kwa mtazamo wa imani na moyo wa Yesu. Katibu wa Vatican, kadhalika alisema Teknolojia ya kidijitali imaecha kuwa chombo tu kati ya vingine, chenye nguvu zaidi ya vingine na kuwa lugha, mazingira, namna ya kukaa katika dunia. Mbele ya mabadiliko haya, Kanisa halipo kubaki kwenye mfumo uliowekwa lakini kuchanganua kutoka Injili kwa uaminifu na ubunifu, katika muktadha huo.”
Kwa njia hiyo matukio ya Jubilei yameanza Jumatatu 28 Julai 2025 kwa Misa katika Parokia zilizo karibu na Vatican na kuendelea na mfululizo wa mikutano, tafakari, na meza za mduara, ikiwa ni pamoja na michango kutoka kwa Mapadre wajesuit David McCallum na Antonio Spadaro, katika kuchunguza jinsi Kanisa linaweza kuitikia utamaduni wa mfumo na mitandao na hekima ya kudumu ya Injili. Warsha ziliakisi changamoto na fursa za ulimwengu halisi katika uinjilishaji wa kidijitali, wakati huo huo nyakati za maombi na jumuiya zilikuza hali ya ushirika zaidi ya skrini. Vivutio maalum vilijumuisha kuabudu na upatanisho, wakiongozwa na Makardinali Rodríguez Maradiaga na José Cobo Cano, na mkesha wa maombi uliohuishwa na Jumuiya ya Taizé.
Jumanne tarehe 29 Julai, washiriki watatembea pamoja katika hija ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, kupitia Mlango Mtakatifu na kuadhimisha Ekaristi pamoja na Kardinali Luis Antonio Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji. Baadaye alasiri utakuwa ni wakati wa kutembelea Bustani ya Vatican na , wataweka wakfu wa misheni yao ya kidijitali kwa Bikira Maria, ambapo Dk. Ruffini alimwita "mshawishi wa kwanza wa Mungu,” katika hotuba yake. Kujiweka wakfu huku kunaonesha hamu ya kusitawisha ubunifu na mawasiliano ya kidijitali katika unyenyekevu, utambuzi na upendo. Kama vile Dk. Ruffini alivyowakumbusha mahujaji kwamba "Hatupo hapa kuwafukuza wafuasi au kujitangaza wenyewe, lakini kuwa wanafunzi wamisionari katika enzi hii ya kidijitali."
Jubilei ya Wamisionari wa Kidijitali na Washawishi Wakatoliki itahitimisha kwa muziki na ushuhuda katika Uwanja wa Risorgimento Roma, tamasha ambalo linalenga kuwa maadhimisho ya utofauti, umoja, na furaha ya kushiriki matumaini na ulimwengu. Wakati wote wa hafla hiyo, Vatican News inatoa matangazo ya moja kwa moja katika lugha nyingi, pamoja na usaidizi kutoka kwa programu ya Vatican Vox na Radio Vatican, kuhakikisha kwamba roho ya Jubilei inawafikia hata wale ambao hawataweza kuhudhuria ana kwa ana. "Hatuko peke yetu," Dk Ruffini alisema. "Sisi ni watu pekee. Na kwa pamoja, tumeitwa kufanya ulimwengu wa kidijitali sio tu kuunganishwa, lakini binadamu wa kweli, wa Kikristo wa kweli."