Jubilei ya Mwaka 2025 Vijana Mahujaji wa Matumaini
Na Padre Philemon Anthony Chacha, SDB., Na Pd Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.
Maadhimisho ya Jubilei ya Vijana kuanzia tarehe 28 Julai hadi tarehe 3 Agosti 2025 yananogeshwa na kauli mbiu “Jubilei ya Mwaka 2025 Vijana Mahujaji wa Matumaini.” Baba Mtakatifu Leo XIV katika salam zake kwa vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia wanaohudhuria Jubilei hii, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Dominika tarehe 27 Julai 2025 anasema, ni matumaini yake kwamba hii ni fursa ya kila kijana kukutana na Kristo Yesu katika maisha yake, tayari kuimarishwa naye katika imani na katika majitoleo yake binafsi ya kumfuasa Kristo Yesu katika uadilifu wa maisha. Hii ni Jubilei ya matumaini inayopania pamoja na mambo mengine; kupyaisha, kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu, tayari kuwajenga vijana hawa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya matumaini. Maadhimisho haya ni cheche ya mwanga wa imani, matumaini, mapendo na zawadi kubwa ambayo Mtakatifu Yohane Paulo II ameliachia Kanisa na kwamba, matunda ya maadhimisho haya ni juhudi za sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbalimbali za dunia, kabla, wakati na baada ya maadhimisho haya!
Maadhimisho haya ni maabara au karakana za imani, kama alivyopenda kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II, enzi zake! Hapa pamekuwa ni chemchemi na chimbuko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa na kwamba, Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, limejikuta likiwa na sura ya ujana, pasi na makunyanzi. Hili ni Kanisa ambalo limewasukuma vijana kuendelea kujiaminisha kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Vijana wamekuwa kweli ni wadau wa Heri za Mlimani, Manabii wa nyakati hizi; vyombo vya ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Vijana wanapaswa kutambua kwamba, Jubilei hii ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa lake; mahali ambapo vijana wanaweza kuchota tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Maadhimisho haya ni chombo muhimu sana cha unjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; ni mahali ambapo wenye kiu na njaa ya maisha ya uzima wa milele wanaweza kushibishwa kwa kujishikamanisha na upendo wa Kristo Yesu. Hili ni Jukwaa la majadiliano kati ya Kanisa na Vijana, changamoto kwa pande hizi mbili anasema Mtakatifu Yohane Paulo II, ni kusikilizana kwa makini tayari kujenga Kanisa la Kisinodi na Kimisionari kama alivyokazia Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Hii ni Epifania na ufunuo wa imani; ni mahali pa kupanga na kutekeleza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya utume wa vijana.
Tunapoendelea kusherehekea mwaka wetu wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo ni wazi kuwa tunaendelea kupata neema na baraka katika kipindi hiki. Tunaadhimisha Jubilei ya Vijana kuanzia tarehe 28 Julai mpaka tarehe 03 Agosti 2025. Jubilei hii inatarajia kuwa na ratiba iliyojaa utajiri wa maadhimisho, mikutano na nyakati za furaha na shangwe zitakazowakutanisha maelfu ya vijana kutoka pande zote za dunia. Kila mmoja atakuwa na nafasi ya kufanya hija hadi kwenye Milango Mitakatifu, na kupokea rehema kamili ya Jubilei kwa kupitia Sakramenti ya Upatanisho. Katika Wosia wa kitume wa Hayati Baba Francisko “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”, ambao umeandikwa katika mfumo wa barua kwa vijana, Hayati Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Papa Francisko anasema: “Endeleeni kufuata matumaini yenu na ndoto zenu. Lakini jihadharini na jaribu moja linaloweza kuturudisha nyuma. Jaribu hili ni wasiwasi. Wasiwasi unaweza kutufanya tukate tamaa kila tunapokosa kuona matokeo ya haraka. Ndoto zetu bora zaidi hufikiwa kwa tumaini, uvumilivu na kujitolea — si kwa pupa. Wakati huohuo, tusisite, wala kuogopa kuchukua nafasi au kukosea. Epukeni kifo cha hofu, kama wafu walio hai — wasio na maisha kwa sababu wanaogopa kuchukua changamoto, kufanya makosa au kuendelea kushikilia ahadi zao. Hata mkikosea, daima mnaweza kuinuka tena na kuanza upya, kwani hakuna mtu mwenye haki ya kuwanyang’anya tumaini.” (CV 142).
Hayati Baba Mtakatifu Francisko anaonesha huruma na kuelewa hali ya vijana wanaokabiliwa na hali ya upweke, wasiwasi, kujitenga, huzuni, na hofu, hali zinazoweza kuwafanya wapoteze tumaini. Mazingira magumu ya maisha katika jamii na utamaduni yanaweza kuongeza mashaka na hofu waliyonayo vijana. Hata hivyo, Papa Francisko anawaita vijana kuwa "Mahujaji wa Matumaini." Katika ujumbe wake katika siku ya 38 ya Vijana Ulimwenguni alisema: “Kama vijana, ninyi ni tumaini la kweli, tumaini lenye furaha kwa Kanisa na kwa ulimwengu mzima.” Licha ya changamoto wanazokabiliana nazo kila siku, Papa Francisko anaamini kuwa vijana wameitwa kwa jambo kuu zaidi, kuliko hali au mizigo ya maisha inayowakandamiza.Tukio hili la Jubilei ya Mwaka Mtakatifu ni mwaliko kwa vijana wote kuamka, kuishi kwa matumaini, na kutambua kuwa maisha yao yana maana kubwa zaidi mbele ya Mungu na ulimwengu. Ni mwaliko pia wa kujikita katika Tumaini linaloweza kuwa nafasi kwa vijana kuhuisha imani yao kwa Mungu, ambaye hushinda giza na kuvuka maumivu, mashaka na wasiwasi wa dunia hii. Kwa nini vijana waweke tumaini lao hapa? Jibu ni rahisi: Yesu Kristo alishinda katika kutokukata tamaa kwa kiwango cha juu kabisa—katika kifo chake—kupitia Ufufuko. Papa Francisko anatuambia: “Kwa sababu Yeye anaishi, hakuna shaka kwamba wema utashinda katika maisha yako. Tukimshikilia Yeye, tutakuwa na uzima.” (CV 127). Kanisa Katoliki ni jumuiya ya waamini iliyoanzishwa juu ya Fumbo la Pasaka — mfululizo wa matukio muhimu ya maisha, mateso, kifo, ufufuko, na kupaa kwa Bwana, yanayokamilika kwa kutumwa kwa Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste. Safari hii imejaa tumaini kuu, kwa sababu Kristo anatufundisha kwamba hakuna lisilowezekana kwa Mungu.
Hayati Papa Francisko pia anawahimiza vijana kuwa na subira katika kutafuta tumaini hili. Anajua kuwa vijana wengi huishi katika utamaduni wa matokeo ya haraka na kuridhika papo hapo, lakini methali ya kale bado inabaki na ukweli wake: "Mambo mazuri hayataki haraka; mambo mazuri huja kwa wale wanaosubiri." Kama hija yoyote ya kiroho, ambayo huhitaji muda na juhudi, vivyo hivyo safari ya kuelekea kutimiza ndoto na malengo ya kweli mara nyingi huwa ndefu na yenye changamoto. Lakini Mwenyezi Mungu huangalia historia kwa mtazamo mpana—anaona mbele zaidi ya kile tunachoweza kuona sasa, hadi maisha ya milele. Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati (1901–1925), msimamizi wa vijana ulimwenguni, ambaye atatangazwa Mtakatifu pamoja na Mwenyeheri Carlo Acutis tarehe 7 Septemba 2025, aliwahi kusema: “Nadhani amani itachukua muda mrefu kuja. Lakini imani yetu inatufundisha kuwa lazima tuendelee kutumaini kwamba siku moja tutaifurahia.” — (Luciana Frassati, A Man of the Beatitudes: Pier Giorgio Frassati, 48). Kumbe, ikiwa tuna imani na tumaini kwa Bwana, basi tunaweza pia kuamini kwamba wema utaushinda uovu, kwa dunia nzima na kwa kila mmoja wetu binafsi.
Zaidi ya vijana 200 kutoka majimbo na vikundi mbalimbali nchini Tanzania wataungana na vijana kutoka katika kila kona ya dunia kwa ajili ya Jubilei ya Vijana hapa Roma. Hii ni nafasi ya Hija, ya kukua kiroho na vijana wanaitwa kuwa wahujaji wa tumaini kwa ajili ya Kanisa na ulimwengu mzima. Wanaweza kuonesha njia si tu kwa kusali, bali pia kwa kushuhudia juhudi na mapambano ya kulinda tumaini mioyoni mwao, wakiwa na matarajio makuu kwamba Mungu siku zote hutimiza. Hata hivyo, tumaini si jambo la mtu mmoja tu. Tunahitaji kuungana, kusaidiana na kuimarishana kwa safari ndefu iliyo mbele yetu. Papa Francisko anatualika “kutembea pamoja, vijana na wazee,” tukitazama siku za mbele, “ili kuhuisha shauku yetu, kuzalisha ndoto, kuamsha unabii, na kufanya tumaini lichanue.” (CV199.) Je, baadhi ya wawakilishi wa vijana kutoka Tanzania wanajisikiaje kuwa miongoni mwa vijana wanaokuja Roma kwenye Jubilei ya Vijana? Nini matumaini yao? Na wangependa kuishi vipi yale watakayojifunza katika Hija hii ya Matumaini? Bernad Shayo, Parokia ya Kibwegere, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, anasema: “Nasikia furaha sana kuwa miongoni mwa mahujaji wa Jubilei ya miaka 2025 ya Ukristo. ?Kupitia kutembelea mahali patakatifu matumaini yangu ni kukua katika neema na imani yangu. ?Nitayaishi yale nitakayojifunza kwani nikirudi nyumbani nitatoa ushuhuda na elimu kwa vijana wenzangu kupitia yale niliyojifunza na kuyaona.”
Joanita Pastory, Parokia Maria Immaculata – Upanga, anasema: “Kwenda Roma katika Jubilei ya Vijana ni kama ndoto inayotimia! Ninajisikia mwenye heshima kuu kuwa sehemu ya historia hii takatifu. Hii si tu safari ya kimwili, bali ni hija ya kiroho inayotugusa mioyo kwa kina. Ninatumaini kupata mwanga mpya wa imani, mshikamano na ujasiri wa kuwa shuhuda hai wa Kristo katika dunia ya leo. Naamini kuwa nimetumwa hapa si kwa bahati, bali kwa kusudi la Mungu. Nitaishi kile tulichojifunza kwa matendo ya upendo, mshikamano, na matumaini yasiyotikisika. Niko tayari kuwa taa kwa wengine, na kupaza sauti ya matumaini katika kizazi chetu! Katika ujumbe wake kwa vijana wa Chicago na vijana wote ulimwenguni Papa Leo XIV anasema: “Katika Mwaka huu wa Jubilei ya Matumaini, Kristo, ambaye ndiye tumaini letu, anatuita sisi sote tukusanyike pamoja, ili tuwe mfano hai wa kweli: nuru ya tumaini katika dunia ya leo.” Hivyo, vijana wanakuwa ishara kubwa ya tumaini kwa dunia yetu ya leo iliyogawanyika. Tunawatakia kheri na baraka tele vijana wote watakaoshiriki Jubilei hii, na hasa wale wote watakaotuwakilisha hapa Roma.