Askofu John Kiplimo Lelei Jimbo Katoliki la Kapsabet, Kenya!
Sarah Pelaji, -Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV ameanzisha rasmi Jimbo Jipya Katoliki la Kapsabet nchini Kenya, kwa kulitenga kutoka Jimbo Katoliki Eldoret. Jimbo hili jipya litakuwa chini ya Jimbo Kuu Katoliki la Kisumu kama mojawapo ya majimbo yanayounda Jimbo hilo kuu. Katika hatua hiyo hiyo, Baba Mtakatifu amemteua Monsinyo John Kiplimo Lelei kuwa Askofu wa Kwanza wa Jimbo jipya la Kapsabet. Kabla ya uteuzi huu, Askofu John Kiplimo Lelei alikuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki la Eldoret, nchini Kenya.
Wasifu wa Askofu Mteule John Kiplimo Lelei alizaliwa tarehe 15 Agosti 1958 huko Soy, Jimbo Katoliki Eldoret. Alisomea Falsafa katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Augustino huko Mabanga na Taalimungu katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Thomas Aquinas, Jijini Nairobi. Alipewa Daraja Takatifu ya Upadri tarehe 26 Oktoba 1985 na kuwa Padre wa Jimbo Katoliki Eldoret. Tangu hapo, amewahi kushika nafasi mbalimbali za kichungaji na kitaaluma, na pia kufanya masomo ya elimu ya juu ikiwemo; shahada ya Uzamivu (PhD) katika Taalimungu akibobea katika Liturujia kutoka Chuo Kikuu cha Vienna (Universität Wien) nchini Austria. Alikuwa Paroko-usu wa Parokia ya Suwerwa na Chepterit mnamo mwaka 1985-1987 na baadaye aliteuliwa kuwa Paroko katika parokia mbalimbali kati ya mwaka 1987-1996. Alifanya utume huko Austria katika Parokia za Mtakatifu Brigitta na Zum Göttlichen Erlöser mnamo mwaka 1996-2002. Mwaka 2002- 2003 alikuwa Paroko wa Parokia ya Kapcherop na Tindinyo 2003-2007. Alikuwa jalimu katika taasisi mbalimbali za kitaaluma na kichungaji ikiwa ni pamoja na AMECEA Pastoral Institute 2003-2004, Institute of Development Studies Kobujoi 2004-2009) na Seminari Kuu ya Mtakatifu Matthias Mulumba, Tindinyo 2003-2008.
Pia alihudumu kama Paroko wa St. Peter's Kapsabet 2007-2008 akawa pia Mwalimu na mlezi katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Matthias Mulumba 2008-2017. Na hatimaye kuwa Gambera wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Thomas Aquinas mjini Nairobi 2017-2023 kabla ya kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki Eldoret. Tarehe 27 Machi 2024 aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki Eldoret. Aliwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 25 Mei 2024. Jimbo jipya la Kapsabet, lenye jina la Kapsabetensis kwa Kilatini, linajumuisha eneo la kiutawala la Kaunti ya Nandi. Jimbo hili limewekwa chini ya Jimbo Kuu la Kisumu. Makao makuu ya Jimbo ni mjini Kapsabet, ambapo Kanisa kuu litakuwa ni Parokia ya sasa ya Mtakatifu Petro (St. Peter), lililopo mjini humo. Kwa hatua hii, Kanisa Katoliki linaimarisha zaidi uwepo na huduma zake katika eneo hilo la Bonde la Ufa, kwa kujibu mahitaji ya kiroho na shughuli za kichungaji kwaa waamini wa kitongoji cha Nandi.