Sr Mary Lembo:"Ni muhimu kuzungumza juu ya nyanyaso hata kama si rahisi"
Na Anne Preckel - Vatican.
“Wanawake wa Imani, Wanawake Wenye Nguvu.” ni mada ya Kongamano la Kimataifa lililofanyika siku za hivi karibuni, kuanzia tarehe 17 hadi 19 Juni 2025, kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, mjini Roma, lililojikita katika masuala ya wanawake na ulinzi kwa ujumla. Miongoni mwa wazungumzaji wakuu, alikuwa ni Sista Mary Lembo, Mtawa kutoka nchini Togo, na mwanzilishi wa kuhamasisha utambuzi wa tatizo la nyanyaso, na ambaye alizungumzia suala la ukatili unaofanyiwa watawa mikononi mwa mapadre barani Afrika. Mwanasaikolojia na profesa jijini Roma katika Taasisi ya Gregorian ya Ulinzi( IADC,) Sr Lembo aliandika kazi yake (thesis) ya Udaktari juu ya fundisho hilo ambalo linajumuisha pia ushuhuda kutoka kwa waathiriwa katika nchi tano za Kiafrika. Mtawa huyo alieleza kuwa ni vigumu kubainisha jinsi tatizo hilo lilivyoenea katika bara la Afrika, “kwa sababu hakuna tafiti za kiasi”; Hata hivyo, alisema “aina hii ya nyanyaso ni uhalisia ambao lazima ushughulikiwe: "Ni tatizo linalohitaji usaidizi na kutiwa moyo kwa wanawake kujitokeza, kulizungumzia na kuripoti kesi hizo, kata kama kama si rahisi."
Hamasa kutoka kwa Papa Francisko
Alipokuwa akikamilisha utafiti wake mnamo 2019, suala la nyanyaso kwa wanawake waliowekwa wakfu barani Afrika lilikuwa ukweli uliofichwa. Katika muktadha huo alisisitiza kuwa , alitiwa moyo kwamba Papa Francisko alikuwa amezungumza hadharani kuhusu hilo kwa mara ya kwanza. “Nilikaribia kuchoka, haikuwa rahisi kuzungumzia jambo hilo. Kwa hiyo maneno yake yalinitia moyo niendelee. Unyanyasaji huu ni ukweli ambao lazima tukabiliane nao katika Kanisa, ili Kanisa liishi katika ukweli.” Pia mnamo 2019, mkutano wa kwanza wa kimataifa juu ya ulinzi wa watoto ulifanyika mjini Vatican uliowakutanisha Marais wote wa mabaraza ya Maaskofu Ulimwenguni. Muda mfupi baadaye, Papa Francis alitoa kanuni mpya za kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto wadogo na watu walio katika mazingira hatarishi. Katika hati iitwayo "Vos estis lux mundi," neno "mtu aliye katika mazingira magumu" pia lilijumuisha watu wazima ambao utashi wao au "uwezo wa kupinga kosa" ni mdogo.
Ukweli uliofichwa
Ilimchukua Sr Lembo miaka kupata waathiriwa wa kutosha kwa ajili ya utafiti wake, tayari kuweza kushirikisha uzoefu wao. Sio kwa sababu kuna waathiriwa wachache, lakini ni kwa sababu ya woga na aibu huzuia wanawake wengi kutoa siri kwa mtu yeyote. Kanisani na katika jamii za Kiafrika, suala la kujamiiana karibu halijadiliwii kamwe, mtawa huyo alieleza: kuhusu “wanawake waliowekwa wakfu kwa Mungu na kuchukuliwa kuwa watakatifu”, na kwa hiyo mada hiyo ni mwiko mzito na maradufu. Kwa ombi la waathirika wenyewe, Sr Lembo hakutaja majina au nchi wanazotoka watawa hao walionyanyaswa kwa sababu alisema: “Waliogopa kitakachowapata wao, familia zao, mashirika yao na hata jumuiya zao. Hata hivyo kuzungumza nami, ni kama walihatarisha kila kitu ili kusaidia wanawake wengine. Kwa hivyo hakuna majina, na lazima niwaheshimu," alisisitiza Mtawa huyo.
Kuelewa muktadha
Wakati wa mahojiano, na Sr Lembo alielezea kwamba alisikia mazungumzo ya “aina mbalimbali juu ya nyanyaso kuhusiana na usindikizwaji wa kiroho.” Yote huanza, mara nyingi, na matumizi mabaya ya mamlaka, kwa sababu kuna uhusiano usio na ulinganifu kati ya mtu anayetoa ushauri na mtu anayeomba mwongozo wa kiroho au ungamo." Mapadre fulani pia walikuwa wametumia vibaya utegemezi wa kiuchumi wa watawa kutoa mkazo, kuanzisha au kulazimisha ngono,” alisema Mtawa huyo. Waathiriwa pia walimwambia mwanasaikolojia huyo juu ya nynyaso za mwili na kiroho.
Sr Mary pia alisisitiza jambo lingine muhimu, yaani, ukweli kwamba hakuna hata mmoja wa watawa walionyanyaswa ambaye alikuwa na nia ya kukiuka nadhiri zake. Wanyanyasaji mara nyingi hutoa shinikizo la kisaikolojia kwa waathiriwa wao, kuendesha au kupuuza mapenzi yao; katika hali kama hizo, si watoto tu bali pia watu wazima, hasa katika hali tete, wanaweza kuwa waathirika. Hii pia inapendelewa katika unyonyaji wa kazi na utegemezi kwa mapadre. Kwa kazi yake hiyo ya kuongeza uelewa, Sr Lembo alitaka kuchangia katika kuboresha mafunzo ya waseminari na watawa. Kwa sababu ikiwa unajua mazingira ya unyanyasaji, unaweza kubadilisha.
Ishara chanya katika Afrika
Sr Lembo alieleza kufurahi kwamba leo hii, kuzungumza juu ya mada hii katika Afrika ni rahisi kuliko ilivyokuwa miaka michache iliyopita. Watawa wengine wa Kiafrika nao wameanza kuleta mada katika mjadala wa kikanisa, ambao unaanza kupanuka. Hivi karibuni, Mkutano wa Viongozi Wakuu wa Afrika na Madagascar (COMSAM) nchini Zambia uliomba Kanisa la Afrika kuingilia kati tatizo hilo kwa uwazi na haki. COMSAM ni shirikisho lililoanzishwa na SECAM (Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar) na linafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Baraz la Kipapa kwa ajili ya Taasisi za Maisha ya Wakfu na Mashirika ya Maisha ya Kitume. Aidha, mwaka huu 2025, kwa mara ya kwanza, wawakilishi wa Mashirika ya Kitawa wa Kiafrika walialikwa kuwakilisha hoja zao moja kwa moja katika Mkutano Mkuu wa SECAM.
Na katika miaka ya hivi karibuni, Mabaraza mengi ya Maaskofu wa Kiafrika yametoa au kukazia miongozo ya Ulinzi wa Watoto wadogo na Watu wazima katika mazingira hatarishi na yanaongeza ufahamu miongoni mwa mapadre na wahudumu wa kichungaji kuhusu suala la nyanyaso. Hii inatoa msingi mzuri wa kuchukua hatua pia dhidi ya unyanyasaji wa wanawake watawa. "Lazima tusonge mbele na kuunga mkono hatua zote zilizopitishwa na Kanisa katika eneo la ulinzi, ni mchakato,” alisema Sista Mary Lembo.