Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba ya Imani, Matumaini na Mapendo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, katika Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa imani, Dominika tarehe 29 Juni 2025, anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kuwapatia Pallio Takatifu, Maaskofu wakuu walioteuliwa katika kipindi cha Mwaka 2024-2025. Pallio takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachotengenezwa kwa manyoya ya kondoo wachanga; na kinavaliwa na Baba Mtakatifu pamoja na Maaskofu wakuu wa majimbo makuu ya Kanisa Katoliki pamoja na Mapatriaki wa Makanisa ya Mashariki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, Mchungaji mwema, hata Maaskofu wakuu wanahamasishwa kuwabeba kondoo wao kama kielelezo cha wachungaji wema; wakumbuke kwamba, wameteuliwa si kwa ajili ya mafao yao binafsi, bali kwa ajili ya kondoo wa Kristo Yesu. Maaskofu wakuu wapya wanapaswa pia kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Pallio takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kama sehemu ya utangulizi wa maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wafanyakazi wa Vatican. Amesema, swali la Kristo Yesu kwa Mtakatifu Petro, Je, wanipenda mimi? Kilikuwa ni kipimo cha upendo wa Kiinjili aliokuwa nao Mtakatifu Petro kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Hawa ni mashuhuda wa kweli wa Kristo Yesu, Kanisa na Injili yake; Walikuwa ni wadhambi, waliotubu na kumwongokea Yesu; kiasi hata cha kuwezeshwa kukirimiwa wito wa kichungaji, bila hata ya mastahili yao! Wakaonjeshwa huruma na upendo wa Kristo Yesu na hatimaye, wakaimarishwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo.
Kumbe, Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, yanabeba ndani mwake: amana na utajiri mkubwa wa maisha na historia ya watakatifu hawa. Hii ni changamoto kwa wafanyakazi wa Vatican kusadaka maisha na utume wao, kwa kuiga mfano wa Watakatifu Petro na Paulo, ili hatimaye, waweze kuwa ni marafiki na wandani wa Kristo Yesu katika maisha na huduma yao: watekeleze dhamana na majukumu yao kwa bidii, weledi, uadilifu mkubwa, ubunifu mkubwa na waoneshe upendo kwa Kanisa ili kuleta tija na mafanikio katika huduma mbalimbali zinazotolewa na Vatican katika ujumla wake. Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo inajikita katika mambo makuu matatu: Mitume hawa walikuwa ni mashuhuda wa maisha, msamaha na mashahidi wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Ni Mitume waliojisadaka kutangaza, kushuhudia na kuishi utume wao, hija ambayo imewafikisha hadi Roma, na hapa wakayamimina maisha, kielelezo makini cha ushuhuda kwa Kristo Yesu, maisha na msamaha! Mitume Petro na Paulo walikuwa ni mashuhuda wa maisha ambayo yalisimikwa katika maisha ya kiroho kwani walikuwa ni wachamungu!
Ni watu ambao walionesha udhaifu mkubwa wa kibinadamu, kiasi hata cha Mtakatifu Petro kumkana Kristo Yesu mara tatu wakati ambapo Mtume Paulo, alilidhulumu Kanisa la Kristo. Lakini wote hawa wakaoneshwa na kuonjeshwa huruma na upendo wa Kristo hasa pale Yesu alipomuuliza Mtume Petro mara tatu, ikiwa kama alikuwa anampenda, Petro akasononeka sana. Mtume Paulo akaulizwa kwanini alikuwa analidhulumu Kanisa lake? Wote wawili waliitwa kwa majina yao, hali ambayo iliwaletea toba na wongofu wa ndani. Hawa ni wadhambi wawili waliotubu na kumwongokea Mungu; ni watu ambao walitambua kwamba, ni wadhambi na Yesu akachukua fursa hii kuwafanyia miujiza, kielelezo cha: huruma na upendo wake, kwa wale wote wanaothubutu kumfungulia hazina ya nyoyo zao, kwa kujiweka mbele ya Kristo, ili aweze kuwatumia kama vyombo na mashuhuda wake. Ni watu walioonesha moyo wa unyenyekevu hadi dakika ya mwisho wa maisha yao, kiasi hata cha Mtume Petro kusulubiwa miguu juu, kichwa chini! Jina Paulo maana yake ni “mtu mdogo”, kielelezo cha unyenyekevu uliomfanya hata watu kusahau jina lake la asili yaani Saulo, aliyekuwa Mfalme wa kwanza wa Israeli.
Mitume hawa wakatambua kwamba, utakatifu wa maisha unafumbatwa katika unyenyekevu, kwa kutambua na kukiri udhaifu na umaskini wao, kiasi cha kujiaminisha kwa Kristo Yesu, aliyewatendea miujiza kwa kuwanyanyua juu, kwa njia ya Msamaha unaoganga na kuponya! Mitume Petro na Paulo ni mashuhuda wa msamaha wa Kristo Yesu, uliowajalia toba na wongofu wa ndani, wakabahatika kuwa watu wapya, wenye furaha na amani ya ndani. Wakasahau ya kale na kuanza kuyaambata maisha mapya yaliokuwa yameboreshwa kwa: huruma na upendo wa Kristo uliokuwa na nguvu kubwa kupita hata mapungufu na makosa yao ya kibinadamu. Huruma ya Mungu inawajalia waamini kuwa na maisha mapya, changamoto na mwaliko kwa waamini kukimbilia Sakramenti ya Upatanisho katika maisha yao! Mitume Petro na Paulo walikuwa ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka; mashuhuda wa msamaha unaoganga na kuponya na hatimaye, wakawa ni mashuhuda wa Masiha, Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Kristo Yesu ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, nyakati zote ni zake; chemchemi ya upendo wa kweli. Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda hai wa Kristo Yesu katika ulimwengu mamboleo. Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani yanahudhuriwa pia na ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Costantinopol wamwendelezo wa mapokeo kwa Makanisa haya mawili. Hii ni changamoto ya kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili kuweza hatimaye, kufikia umoja kamili katika ngazi zote. Kwa sababu, wote wakiwa wamepatanishwa na Mwenyezi Mungu na kusamehewa dhambi zao; wanaitwa kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu kwa njia ya maisha yao yenye mvuto na mashiko!