Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo Akutana na Papa Leo XIV mjini Vatican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi tarehe 28 Juni 2025 amekutana na kuzungumza na Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Guinea ya Ikweta, ambaye baadaye alibahatika pia kukutana na kuzungumza na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa.
Katika mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Leo XIV na mgeni wake, walipongeza ushirikiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili, sanjari na mchango wa Kanisa Katoliki katiks ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Guinea ya Ikweta, hususan katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo: kijamii na kitamaduni. Baadaye, Baba Mtakatifu Leo XIV na mgeni wake walijielekeza katika masuala ya Kikanda na Kimataifa kwa kuchangia mawazo yao, na hasa zaidi kuhusu kinzani, migogoro na vita, bila kusahau usalama wa baadhi ya nchi Barani Afrika.