Rais Carlos Manuel Vila Nova Akutana na Papa Leo XIV Mjini Vatican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV Jumatatu tarehe 30 Juni 2025 amekutana na kuzungumza na Rais Carlos Manuel Vila Nova wa Sao Tome na Prince na baadaye akakutana na kuzungumza na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Baba Mtakatifu Leo XIV katika mazungumzo na mgeni wake, wamepongeza uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati ya nchi hizi mbili, na baadaye wakajielekeza katika masuala ya kisiasa na kiuchumi, sanjari na mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hususan katika huduma ya afya, elimu; malezi na majiundo kwa vijana wa kizazi kipya.
Katika mazungumzo yao, wamebadilishana mawazo kuhusu mada mbalimbali za Kikanda na Kimataifa, kwa kukazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na ushirikiano wa Kimataifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.