杏MAP导航

Tafuta

Padre John Baptist Matovu kutoka Jimbo Katoliki la Masaka, Uganda, Padre Joseph Mutisya kutoka Jimbo Katoliki la Kitui, Kenya pamoja na Padre Erick Francis Mgombera kutoka Jimbo Katoliki la Ifakara, Tanzania. Padre John Baptist Matovu kutoka Jimbo Katoliki la Masaka, Uganda, Padre Joseph Mutisya kutoka Jimbo Katoliki la Kitui, Kenya pamoja na Padre Erick Francis Mgombera kutoka Jimbo Katoliki la Ifakara, Tanzania.   (@Vatican Media)

Padre Erick Francis Mgombera Mtanzania wa Kwanza Kupewa Upadre na Papa Leo XIV

Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 32 kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Kanisa Barani Afrika limepata Mapadre wapya 13 na Kanisa Afrika Mashariki limebahatika kuwapata Mapadre 3 nao ni: Padre John Baptist Matovu kutoka Jimbo Katoliki la Masaka, Uganda, Padre Joseph Mutisya kutoka Jimbo Katoliki la Kitui, Kenya pamoja na Padre Erick Francis Mgombera kutoka Jimbo Katoliki la Ifakara, Tanzania. Wazazi wake wamefurahi!

Na Padre Erick Francis Mgombera, na Sarah Pelaj - Vatican.

Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre, Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 32 kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Kanisa Barani Afrika limepata Mapadre wapya 13 na Kanisa Afrika Mashariki limebahatika kuwapata Mapadre 3 nao ni: Padre John Baptist Matovu kutoka Jimbo Katoliki la Masaka, Uganda, Padre Joseph Mutisya kutoka Jimbo Katoliki la Kitui, Kenya pamoja na Padre Erick Francis Mgombera kutoka Jimbo Katoliki la Ifakara, Tanzania. Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilelel cha maisha na utume wa Kanisa; Mapadre wajitahidi kuishi upendo wa shughuli za kichungaji; Upadre ni huduma ya kuwatakatifuza watu wa Mungu, Upatanisho na Umoja katika upendo. Kwa kuwekewa mikono na kushukiwa na Roho Mtakatifu, Mashemasi wanakuwa ni Mapadre, changamoto na mwaliko wa kuwa ni Mapadre wenye upendo kwa Mungu na jirani; waadhimishaji waaminifu wa Mafumbo ya Kanisa, watu wa Sala na hasa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.

Papa Leo XIV akiwa na Mapadre wapya 32 kutoka sehemu mbalimbali za dunia
Papa Leo XIV akiwa na Mapadre wapya 32 kutoka sehemu mbalimbali za dunia   (ANSA)

Mapadre wachuchumilie utakatifu wa maisha; wajisadake bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu na waendelee kujifunza kutoka kwa watu wanaowahudumia, Mapadre, Mashuhuda wa imani, Mitume, Wamisionari pamoja na mashuhuda wa Injili ya upendo. Padre Erick Francis Mgombera kutoka Jimbo Katoliki la Ifakara, katika maisha na utume wake anaongozwa na kauli mbiu ya Kipadre “Bwana ana haja naye.” Mk 11:3: Na “Ole wangu nisipohubiri Injili”: “Vae enim mihi est si non evangelizavero" 1Kor 9:16. Padre Erick Francis Mgombera ni Mtanzania wa kwanza kabisa kupewa Daraja takatifu ya Upadre na Baba Mtakatifu Leo XIV, Ijumaa tarehe 27 Juni 2025 kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Ifuatayo ni historia fupi ya maisha na wito wa Padre Erick Francis Mgombera kutoka Jimbo Katoliki la Ifakara.

Padre Erick Francis Mgombera, amepadrishwa na Papa Leo XIV
Padre Erick Francis Mgombera, amepadrishwa na Papa Leo XIV   (@Vatican Media)

Mimi ninaitwa Padre Erick Francis Mgombera, nilizaliwa tarehe 17/01/1994 katika kijiji cha Ipinde, kata ya masagati, tarafa ya Mlimba wilaya ya Kilombero, Mkoa wa Morogoro Tanzania. Kikanisa ni kigango cha Ipinde, parokia ya Maria Konsolata Taweta Jimbo la Mahenge (kwa zamani) kwa sasa ni Jimbo Katoliki la Ifakara. Wazazi wangu wanaitwa Francis Alfonce Mgombera na Aghatha Aghathon Lyabonga. Natokea katika familia ya watoto sita kwa majina (1. Christabela Mgombera 2. Erick Mgombera 3. Jimmy Mgombera 4. Prodensiana Mgombera 5. Lonaldo Mgombera 6. Ronadihno Mgombera {Lonaldo na Ronadihno ni mapacha na wao ndio wa mwisho kuzaliwa). Nilianza shule ya awali Ipinde mwaka mwaka 2000-2001, katika shule ya msingi Ipinde. Na shule ya msingi darasa la kwanza hadi la saba Mwaka 2002 hadi mwaka 2008. Masomo ya Sekondari katika shule ya awali ya Seminari ya Mtakatifu Patrick Sofi Ulanga Jimbo la Mahenge mwaka 2009. Sekondari Ordinali levo Katika Seminari ndogo ya Mt. Fransisko Kasita mwaka 2010- 2013. Masomo ya “Advanced Level” katika Seminari ndogo ya Mtakatifu Francisko Kasita mwaka 2014 hadi mwaka 2016.

Papa Leo XIV akiingia kwenye Ibada ya Misa Takatifu
Papa Leo XIV akiingia kwenye Ibada ya Misa Takatifu   (@Vatican Media)

Masomo ya Falsafa katika Seminari kuu ya Mtakatifu Augustino Peramiho, Jimbo kuu la Songea, Tanzania mwaka Novemba 2016 hadi Juni 2019. Na masomo ya Taalimungu Mungu katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Augustino Peramiho Songea Tanzania kuanzia Septemba 2019 hadi Juni 2025. Uchungaji mwaka 2022 Juni hadi Septemba 2024. Sakramenti: Sakramenti ya Ubatizo mwaka 1997, Komunyo ya kwanza September 2004 Kigango cha Ipinde na padre Ockavian Linuma. Kipa-Imara 09.09.2007 Parokia ya Maria Konsolata Taweta na Mhashamu Askofu Agapiti Fidelis Ndorobo wa Jimbo la Mahenge. Safari yangu Wito ilianza nikiwa mdogo maana nilipenda kuigiza mara kwa mara kufanya Misa Nyumbani nikijiita Padre. Kwa sababu nilikuwa mfupi na mnene (kibonge) kwa kipindi hicho paroko msaidizi alikuwa pia mnene basi nilipenda zaidi kuitwa kwa jina lake. Nilipofika darasa la saba Katekista alinishawishi nichukue fomu ya kujiunga na Seminari. Nikichaguliwa na kujiunga na Seminari ya awali ya Mtakatifu Patrick Sofi jimbo Katoliki la Mahenge baadae niliendelea na masomo katika seminari ndogo ya Kasita Jimbo la Mahenge kwa masomo ya ordinari levo na Advanced level. Safari hii ya wito katika hatua za mwanzo za kujinga na seminari kuu zimechangiwa sana na Paroko wangu. Nawashukuru walimu wote walionifundisha wamepalilia wito wangu kwa namna ya pekee kila mmoja. Magombera wote wa Seminari zote nilizosoma. Maparoko wote walionisaidia katika uchingaji mdogo na mkubwa. Watawa wote, waseminari wadogo kwa wakubwa na mwisho waamini wote wana mchango mkubwa katika maisha yangu ya wito na Mungu awabariki. Kwa namna ya pekee napenda kumshukuru sana Mhashamu Askofu Salutaris Merchior Libena kwa kunipokea katika Jimbo lake Katoliki la Ifakara na kunilea kiroho na kimwili hadi Kufikia hatua hii ya Daraja Takatifu ya Upadre, Mungu ambariki.

Papa Leo XIV ametoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 32
Papa Leo XIV ametoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 32   (@Vatican Media)

Daraja Takatifu: Kabla ya kupewa daraja takatifu ya ushemasi, nilipata huduma ya usomaji (lector) Okotba 2018 na Mha: Askofu Mstaafu Emmanuel Mapunda wa Jimbo Katoliki la Mbinga (Kwa sasa mwenyezi Mungu amemwita katika makao yake ya Milele) apumzike kwa Amani. Na huduma ya usindikizi altareni (acolyte) Okotba 2019 na Mha: Askofu John Ndimbo wa Jimbo Katoliki la Mbinga. Daraja Takatifu ya Ushemasi nilipata Tarehe 03/01/2025 katika kuu la Mtakatifu Andrea Jimbo Katoliki la Ifakara. Na Mha: Askofu Salutaris Merchior Libena Askofu wa Jimbo Katoliki la Ifakara. Daraja takatifu ya Upadre nimepewa tarehe 27/06/2025 kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, mikononi mwa Baba Mtakatifu Leo XIV. Mwenyezi Mungu awabariki wote walionisaidia kuijongea Altare yake Takatifu. Amina.

Upadre ni huduma kwa watu wa Mungu
Upadre ni huduma kwa watu wa Mungu   (@Vatican Media)

Yaliyojiri Baada ya Misa Takatifu: Wakati huo huo, Mhashamu Askofu Salutaris Melchior Libena Askofu wa Jimbo Katoliki Ifakara, aliungana na wazazi, ndugu jamaa na marafiki wa Padre mpya Erick Francis Mgombera wakiwemo mahujaji zaidi ya 30 kutoka Tanzania kwa ajili ya mashangilio mafupi katika Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kisha kupata mlo wa mchana kwa pamoja. Padre mpya Mgombera alimshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai na wito wa upadre. Pia alimshukuru Askofu Salutaris Libena kwa malezi katika safari yake ya wito kisha kuamua na kumruhusu afike Roma kwa ajili ya kupata Daraja Takatifu ya Upadre. “Nimejawa na moyo wa shukrani na mshangao wa kutendewa haya na Mungu kwani sikuwahi kuwaza kwamba siku yangu ya kupata upadri itakuwa hivi. Namshukuru Papa Leo XIV kwa kunipa Daraja Takatifu katika madhabahu ya Mtakatifu Petro,” amesema. Askofu Libena alielezea namna ambavyo jimbo lake lilipata bahati ya kuleta shemasi ili apate Daraja la Upadri siku ya Hija Takatifu ya Mapadri Vatikani Roma, kwamba Maaskofu Katoliki walitangaziwa kwamba Papa anaalika angalau kila Baraza la Maaskofu Katoliki liwakilishe shemasi atakayepata Daraja Takatifu la Upadri siku ya Hija ya Mapadri katika Mwaka huu Mtakatifu. Hivyo Jimbo Katoliki Ifakara likapata bahati ya kuchaguliwa kuwakilisha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa kupeleka Shemasi ili apewe Daraja Takatifu na Papa Leo XIV katika mwaka wa Jubilei Kuu. “Hivyo Jimbo la Ifakara likawa na Shemasi ambaye alikuwa anamaliza masomo yake katika Seminari Kuu ya Peramiho ambaye angepata Daraja Takatifu la Upadri mwaka huu wa 2025, hivyo Jimbo likamchagua yeye awakilishe wengine katika maadhimisho hayo makuu. Nami ninamshukuru Mungu kwa ukuu wake,” amesema.

Pd Erick Francis Mgombera
27 Juni 2025, 17:14