Mons.Formica kwa UN:“Maendeleo ni jina jipya la amani”na amani sio tu kukosekana kwa vita
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Umoja wa Matiafa, Askofu Mkuu Marco Formica, alitoa hotuba yake katika mjadala wa wazi wa Baraza kuhusu Usalama, umaskini, Maendeleo duni na migogoro” huko Jijini New York, Marekani tarehe 23 Juni 2025. Askofu Mkuu Formica awali ya yote alipenda kutoa shukrani zake kwa Urais wa Guyana wa Baraza la Usalama kwa kuitisha mjadala huo wa wazi, ambao kiukweli ulilenga kuvutia changamoto zilizounganishwa za umaskini, maendeleo duni na mjadala. Mambo haya ambayo mara nyingi yanachocheana, yanaleta vikwazo vizito katika amani na usalama wa kimataifa. Kama jumuiya ya kimataifa inavyokiri katika Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu, kutokomeza umaskini katika aina na vipimo vyake vyote ni "changamoto kubwa zaidi ya kimataifa na hitaji lazima kwa maendeleo endelevu." Ahadi hii ya pamoja inasisitiza uwajibikaji wa haraka wa kimaadili wa vyanzo vya umaskini, ambavyo mara nyingi vinahusishwa na ukosefu wa haki, kutengwa, na kunyimwa haki za msingi.
Maendeleo ni jina jipya la amani
Mapema kunako mwaka 1967, Papa Mtakatifu Paulo VI alitangaza kiunabii kwamba: “maendeleo ni jina jipya la amani.” Maono haya yanatukumbusha kuwa amani sio tu kukosekana kwa vita, bali ni kukuza udugu wa binadamu, uimarishaji na ustawi wa pamoja kwa wote. Katika roho hiyo, Vatican inashikilia kwamba maendeleo fungamani ya binadamu hayawakilishi hitaji la kimaadili tu kwa wanadamu wote, bali pia njia madhubuti kuelekea amani ya haki zaidi, sheria, na ya kudumu. Katika suala hili, Vatican bado inajali na kuwa na wasiwasi kuhusu matumizi ya kijeshi yanayoongezeka kila mara, ambayo yanaondoa rasilimali kubwa kutoka katika uwekezaji katika sekta za maendeleo kama vile afya, elimu na miundombinu. Katika muktadha huo, Vatican inasasisha pendekezo lake la kuanzishwa kwa mfuko wa kimataifa, ambao kwa sehemu unafadhiliwa kwa kuelekeza rasilimali zilizotengwa kwa sasa kwa silaha.
Mfuko wa Kimataifa unaoweza kutokomeza umaskini na njaa na kukuza maendeleo
Mfuko wa Kimataifa unaweza kutoa mchango wa maana katika kutokomeza umaskini na njaa, na kukuza maendeleo katika maeneo yenye hali duni zaidi duniani. Hii ingeendeleza njia ya haki zaidi na endelevu kuelekea amani, na kulinda na kukuza utu wa binadamu. Amani ya kudumu inahitaji kujitolea kwa maendeleo fungamani ya binadamu, kudumisha hadhi aliyotolewa na Mungu wa kila mtu na kuendeleza hali zinazohitajika kwa ajili ya haki, mshikamano na ustawi wa wote. Katika suala hili, Kiti Kitakatifu kinasisitiza umuhimu wa kuweka maendeleo fungamani ya binadamu katikati ya mapitio yanayoendelea ya Usanifu wa Ujenzi wa Amani, na kukuza ushirikiano ulioimarishwa kati ya Nchi Wanachama katika huduma ya amani.