Maaskofu wa Marekani:Kukuza uhuru wa kidini kwa sala,tafakari na matendo!
Na Christopher Wells – Vatican.
Kuanzia tarehe 22 Juni,ambapo kwa mwaka huu 2025 ni Sherehe ya Mwili na Damu ya Yesu sambamba na siku kuu ya Mtakatifu Yohane Fisher na Thomas More, Kanisa Katoliki nchini Marekani linaadhimisha Uhuru wa Kidini, itakayohitimishwa kwenye Maadhimisho ya Watakatifu Petro na Paulo, tarehe 29 Juni. Mpango wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani (USCCB), katika Juma la Uhuru wa Kidini linawaalika waamini wote kuendeleza “haki muhimu ya uhuru wa kidini kwa Wakatoliki na wale wa dini zote.”
'Mashuhuda wa kutumaini'
Mada ya maadhimisho ya mwaka huu ni, “Mashahidi wa Kutumaini”, inayojengwa juu ya ripoti ya mwaka, ya Mkutano wa 2025 kuhusu hali ya uhuru wa kidini nchini Marekani,( ,) ambayo inaakisi “matokeo ya mgawanyiko wa kisiasa katika uhuru wa kidini" pamoja na masuala kuanzia mamlaka ya urutubishaji wa ndani, vitisho kwa huduma za Kikatoliki zinazohudumia wahamiaji, na uchaguzi wa wazazi juu ya elimu. Kauli mbiu ya mwaka huu inahusishwa na Mwaka wa Jubilei 2025 unaoendelea uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko, kwa mujibu wa Askofu Thomas Paprocki, wa Jimbo la Springfield huko Illinois, ambaye alipendekeza Juma la awali la Uhuru, ambapo tangu wakati huo limebadilika na kuwa Juma la Uhuru wa Kidini.
Akiwa na msukumo kutoka katika msemo wa Mtakatifu Paulo "tumaini halikatishi tamaa", Askofu Paprocki aliviambia vyombo vya habari Vatican News, kwamba “tumaini linatupatia uhakika katika siku zijazo na katika mambo ambayo Mungu anaahidi kuhusu uzima wa milele." Alifafanua kuwa Juma la Uhuru wa Kidini ni mwaliko kwa Wakatoliki kuombea uhuru wa kidini ulindwe nchini Marekani na duniani kote; kutafakari maana ya uhuru wa kidini; na kuchukua hatua katika kutetea uhuru wa dini. Katika hilo Askofu wa Jimbo la Springfield alisema "Kwa hivyo ni hatua hizi tatu za: kuomba, tafakari, na kutenda kwa njia ambazo tunaweza kuwa mashahidi wa kutumaini katika suala la uhuru wa kidini."
Uhuru na ukweli
Katika mahojiano yake na Vatican News, Askofu Paprocki alisema suala la uhuru wa kidini lazima lieleweke kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa kuhusu uhuru. Akitoa mfano wa mafundisho ya Papa Mtakatifu Yohane Paulo II, Askofu huyo anaeleza kwamba uhuru wa kweli unahusiana na ukweli, na lazima utofautishwe na “leseni”, uwezo wa kufanya chochote anachopenda mtu. "Kanisa limefundisha kwamba uhuru upo ili tuwe huru kutekeleza imani yetu, ili kufuata yaliyo sawa na kuweza kusema ukweli", alisema Askofu Paprocki. Aliendelea kusisitiza kwamba "upande wa pili wa sarafu kuhusu haki ni wajibu, si tu katika Kanisa lakini pia katika muktadha wa kiraia. Sio tu suala la uhuru wetu na haki zetu, lakini tuna wajibu wa kuwa raia wema," na kwa njia hiyo Askofu alisema, "kusaidia kukuza manufaa ya wote na taifa letu, na kutetea uhuru wa nchi yetu."