Kumbukizi ya Miaka 60 Tangu Kuanzishwa Kwa IUISG- Watawa
Sr. Bridgita S. Mwawasi – Roma, Italia.
Wito wa watawa ni kuambatana na watu wa Mungu kwenye safari ya Maisha wanapotafuta maana halisi na lengo la maisha yao hapa duniani. Watawa wanaalikwa kuendelea kuwatia moyo watu wa Mungu ili kutokata tamaa kwenye safari hiyo. Nalo Kanisa linahimizwa kuendelea kutilia mkazo hadhi ya kila mwanadamu kama kiumbe kilichoumbwa kwa sura na mfano wake mwenyezi Mungu. Hayo yalijitokeza bayana kwenye Mkutano Mkuu wa Viongozi wa Mashirika ya Watawa Wanawake duniani uliomalizika hivi karibuni hapa mjini Roma, nchini Italia. Mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Kimataifa, Ergife uliopo njia kuu ya Valle Aurelia na kuwakusanya pamoja viongozi wa watawa wa Mashirika zaidi ya mia tisa (900) kutoka pande zote za dunia. Viongozi hao walijadiliana maswala mbalimbali na muhimu yanayoukabili ulimwengu mamboleo likiwemo suala la Kanisa na Maisha ya imani na ya kitawa katika ujumla wake. Kwenye ulimwengu uliojaa vita na chuki na utengano unaosimikwa kwenye misingi ya: rangi, ukabila, utaifa, kiuchumi, kisera na hata kijinsia, watawa wanaalikwa kuuiga mfano wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko ambaye alisisitiza umuhimu wa kuzingatia: utu, heshima na haki msingi za binadamu na kutilia maanani mshikamano na ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaowawezesha wanadamu kushirikiana bila kujali mipaka ya utengano iliyoko kati yao. Mada ya mkutano huo mkuu wa watawa wa kike duniani uliofanyika kuanzia tarehe 5 hadi 9, Mei, 2025 ilikuwa Maisha ya Kitawa: Tumaini lenye kupyaisha/ kuunda upya – “Consecrated life: A hope that transforms.” Watawa hao pia waliadhimisha kwa mbwembwe miaka sitini (60) tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Kimataifa la Mashirika ya Kike ya Kitawa na Kazi za Kitume, “International Union of Superiors Genera, lUISG.”
Huu ni mchakato uliotoa kipaumbele cha kuwasaidia watawa wa kike kujijenga na kujiimarisha kiroho, kielimu, kitaadhima na hata kitaaluma, ili kuweza kusafiri na watu wa Mumgu kiimani kwenye safari yao ya kiroho na kimaisha kwa ujumla. Kwenye majadiliano yao, viongozi hao wa mashirika ya kitawa ya wanawake duniani walitumia mfumo wa mazungumzo katika roho (conversations in the spririt), uliopendekezwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwenye safari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Hii pia ilikuwa njia mojawapo ya kumuenzi Hayati Papa Francisko ambaye aliwapenda na kuwaheshimu sana watawa pamoja na kuthamini mchango wao ndani ya Kanisa kwa kuhakikisha kwamba aliwateua watawa kadhaa kama viongozi kwenye ngazi mbalimbali za uongozi mjini Vatican, kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya Kanisa Katoliki. Huu ulikuwa ni wakati mwafaka wa kuisikiliza sauti ya Roho Mtakatifu kupitia kazi za kitume wanazofanya watawa hao sehemu mbalimbali za dunia. Itakumbukwa kuwa watawa wana nafasi ya kipekee kuendeleza utume na maendeleo ya jamii kwani kwa njia ya ushuhuda wa imani yao kuu, watawa wa kike huendeleza utume hasa kwenye sehemu ambazo hata serikali za nchi mbalimbali huenda hazijaweka miundo mbinu muhimu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa siku nne mfululizo, watawa hawa walishirikishana umuhimu wa utume wao, matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zilizoko mbele yao. Watawa kutoka sehemu mbalimbali za dunia waliwashirikisha wenzao baadhi ya y le yanayojiri kwenye sehemu zao za utume, kama vile Amazonia, mipakani mwa Amerika na Amerika ya Kusini, nchi kadhaa za Afrika na hata kutoka Barani Ulaya. Ni wazi kuwa watawa wanaendelea kuwa ishara ya matumaini kwenye sehemu zote wanapofanya utume wao. Hii ni pia ishara ya tumaini ndani ya Mama Kanisa ambaye tangu jadi ameendelea kuwahimiza wanae kuimarika kiimani ili waweze kuutambua, kuuthamini na kuushirikisha kwa wengine, wema wa Mungu ambaye alimtuma Kristo Mwanaye wa pekee, ili kuupatia ulimwengu matumaini.
Kwenye ripoti yao ya miaka mitatu ya Shirikisho la Kimataifa la Mashirika ya Kike ya Kitawa na Kazi za Kitume, “International Union of Superiors Genera, lUISG” lenye Makao yake makuu mjini Roma, Rais wa Shirikisho hilo, Sr. Mary Barron, na Katibu wake Sr. Patricia Murray walikazia mwito wa Hayati Papa Francisko wa ushirikiano na mshikamano katika utume. Mashirika ya Masista Wakatoliki yamekuwa yakishirikiana kwa karibu sana kwa miaka mingi na kuunda Mabazara ya Mashirika mbalimbali kwenye kila nchi, kanda, Bara na hata katika ulimwengu mzima. Hayati Papa Francisko naye alithamini ushirikiano huo na kuwaenzi watawa popote duniani. Alihakikisha kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya Sinodi za Maaskofu, Watawa walishiriki kwenye majadiliano yote kwenye Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuanzia mwaka 2021 hadi 2024. Shirikisho la Kimataifa la Mashirika ya Kike ya Kitawa na Kazi za Kitume, “International Union of Superiors Genera, lUISG,” sasa linashirikiana na Mashirikisho ya watawa kikanda, kama vile ACWECA, yaani Shirikisho la Mabaraza ya Watawa wa Kike Afrika Mashariki na ya Kati. Hii ni kwa ajili ya kuwafunda na kuwaunda watawa watakaoshirikiana na wadau wengine ndani ya Mama Kanisa ili kushirikisha matunda ya Sinodi duniani kote. Kilele cha uwepo pamoja wa watawa hawa mjini Roma kilikuwa tendo la kihistoria la kuwepo Roma wakati wa uchaguzi wa kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki. Watawa waliandamana na Kanisa zima kuombea Makardinali waliokuwa kwenye Kikanisa cha Sistine wakimsikiliza Roho Mtakatifu na kumchagua kiongozi mpya kama Roho angeliwaongoza. Nao moshi mweupe uliposhuhudiwa kwenye siku ya pili ya uchaguzi huo, watawa waliokuwa kwenye Misa walishindwa kuizuiya furaha yao na kuimba na kushangilia pamoja na ulimwengu mzima, kuchaguliwa kwake aliyekuwa Robert Kardinali Francis Prevost kama Mchungaji mkuu mpya wa Kanisa Katoliki, Baba Mtakatifu Leo wa kumi na nne. Huu ukawa mwanzo wa utume mpya, nao watawa wakauombea na kuuweka chini ya ulinzi na maombezi ya Mama Bikira Maria kwa kufunga mkutano wao kwa ibada ya Misa takatifu iliyoongozwa na Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ya Kiume, Padre Mauro Giuseppe, kwenye Kanisa Kuu la Bikira Maria mkuu, mahali anapolala usingizi wa amani, Hayati Papa Francisko.