Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Akutana Na Papa Leo XIV Mjini Vatican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 11 Juni 2025 amekutana na kuzungumza na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Manuel de Oliveira Guterres, ambaye baadaye amekutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Katika mazungumzo ya viongozi hawa wawili, Baba Mtakatifu ameonesha nia ya kuendelea kuunga mkono jitihada za Umoja wa Mataifa katika ujenzi wa amani duniani.
Baba Mtakatifu Leo XIV pamoja na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wamezama zaidi katika maandalizi ya mikutano ya Umoja wa Mataifa, matatizo na changamoto zinazoendelea kuukabili Umoja wa Mataifa katika medani mbalimbali za maisha, sehemu mbalimbali za dunia. Katika mazungumzo yao, wamegusia pia vita, kinzani na migogoro inayoendelea kupekenya utu, heshima na haki msingi za binadamu.