Askofu Msaidizi Mamiarisoa M. Randrianifahanana Jimbo Kuu la Antananarivo Madagascar
Sarah Pelaji, -Vatican
Baba Mtakatifu LeoXIV tarehe 26 Juni 2025 amemteua Padre Mamiarisoa Modeste Randrianifahanana kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Antananarivo Madagascar. Hadi Uteuzi huo, Padre Randrianifahanana alikuwa Makamu wa Askofu wa Jimbo Kuu la Antananarivo na kumpangia Jimbo la Kihistoria la Giocondiana. Wasifu wa maisha na utume wake wa Kipadre: Askofu Mteule Mamiarisoa Modeste Randrianifahanana alizaliwa tarehe 18 Juni 1967 huko Fiakarana. Alijiunga na Seminari Kuu ya Antsirabe kwa masomo ya Falsafa na Taalimungu katika Seminari Kuu ya Ambatoroka, Antananarivo. Alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 6 Septemba 1997.
Katika maisha yake kama Padri ameshika nyadhifa mbalimbali za kulitumikia Kanisa kama: Mlezi wa maisha ya kiroho wa Chama cha Kitume cha Vijana wa Ekaristi na Mkuu wa Liturujia (1997-2003), Mkuu wa nyumba ya malezi ya Jimbo Katoliki Antananarivo (1998-2003); Mlezi wa mapadre wa zawadi ya Imani kwenye visiwa vya Réunion (2003-2017), Paroko wa Parokia ya Ambatolampy (2017-2020), Mlezi na Mwalimu katika Seminari Kuu ya Antsirabe (2020-2023); Alishika nafasi ya kuwa Makamu wa Askofu wa Jimbo kuu la Antananarivo tangu 2023 hadi 2025 alipoteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa jimbo kuu la Antananarivo.