杏MAP导航

Tafuta

Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania, tarehe 29 Mei 2025 ametabaruku Kanisa la Mtakatifu Paulo VI, Bweri Nyabange, Musoma. Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania, tarehe 29 Mei 2025 ametabaruku Kanisa la Mtakatifu Paulo VI, Bweri Nyabange, Musoma. 

Askofu Msonganzila: Simameni Kidete Kutetea Injili ya Uhai!

Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo ni kati ya mafundisho mazito ya Papa Paulo VI aliyetangazwa kuwa Mtakatifu hapo tarehe 14 Oktoba 2018. Anakita mawazo yake katika dhamana na wajibu wa kazi ya uumbaji, malezi, makuzi na elimu ya watoto. Wanandoa wanapaswa kufikiri, kujiandaa kikamilifu, kusindikizana na hatimaye, kupokea mtoto kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, dhamana inayowawajibisha! Simameni kidete kulinda Injili ya Uhai!

Na Sarah Pelaji- Vatican na Veronica Modesti - Jimbo la Musoma

Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania, tarehe 29 Mei 2025 ametabaruku Kanisa la Mtakatifu Paulo VI, Bweri Nyabange. Hii pia ilikuwa ni kumbukumbu ya Mtakatifu Paulo VI aliyesimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu” ni Waraka wa kinabii unaobainisha dhamana na wajibu wa wanandoa wanaoushiriki katika kazi ya uumbaji, ili kuendeleza zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni dhamana ambayo inapaswa kumwilishwa katika furaha ya maisha na utume wao ndani ya familia. Mtakatifu Paulo VI alikuwa na upeo mpana na uwezo wa kuona mbali, akagundua changamoto na vikwazo vinavyowakabili wanandoa; akabainisha wajibu wa Kanisa kama Mama na Mwalimu na kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo ni kati ya mafundisho mazito ya Papa Paulo VI aliyetangazwa kuwa Mtakatifu hapo tarehe 14 Oktoba 2018. Anakita mawazo yake katika dhamana na wajibu wa kazi ya uumbaji, malezi, makuzi na elimu ya watoto. Wanandoa wanapaswa kufikiri, kujiandaa kikamilifu, kusindikizana na hatimaye, kupokea mtoto kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, dhamana inayowawajibisha! Hizi ni changamoto zilizoibuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, zinazowataka waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema, sadaka na majitoleo binafsi. Mtakatifu Paulo VI alikuwa mwamba wa Injili ya familia na kamwe hakutikisika katika maamuzi na mafundisho yake ya kina! Ndiyo maana anakumbukwa kama “Papa wa familia” aliyekita mafundisho yake katika tasaufi ya Kikristo, wito na dhamana ya wazazi ndani ya familia, ili waweze kuwa mashuhuda wa upendo wa Kikristo, changamoto iliyovaliwa njuga pia na Hayati Baba Mtakatifu Francisko.

Tarehe 29 Mei ya Kila Mwaka ni Kumbukumbu ya Mtakatifu Paulo VI.
Tarehe 29 Mei ya Kila Mwaka ni Kumbukumbu ya Mtakatifu Paulo VI.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Waraka huo wa kitume ulikabiliwa na changamoto kubwa kwa wakati huo baada ya kuibuka “dhana ya kudhibiti uzazi” ili kupunguza idadi ya watu duniani na baadhi ya wanataalimungu wakajikuta wakitumbukia katika mtego huu kwa kulitaka Kanisa kusoma alama za nyakati kwa kusahau kwamba, walikuwa wanakwenda kinyume cha Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Injili ya uhai, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Paulo VI katika changamoto hii, alionesha hekima na busara ya kichungaji na kuungwa mkono na Kardinali Karol Wojtyla, aliyekuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia, Poland, ambaye baada ya kuteuliwa kwake kuliongoza Kanisa, akasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Mtakatifu Paulo VI amewawezesha waamini kutambua kwamba, Mafundisho ya Kanisa ni endelevu na ya daima, Kanisa linapenda kusoma alama za nyakati kwa kuzingatia amana na utajiri wa Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Kwa bahati mbaya, wanasiasa wamejichukulia madaraka makubwa ya kuamua hatima ya: heshima, utu wa binadamu na maisha yake, jambo ambalo anasema Kardinali Parolin, si sahihi ingawa linaendelea kutendeka hadi leo hii. Katika unyenyekevu wa kichungaji, Mtakatifu Paulo VI alitafuta ushauri kwa viongozi mbalimbali wa Kanisa na hatimaye akaibuka na ushuhuda wa Kanisa kwa kusema kwamba, uchungu na fadhaa ya mwanadamu anayeteseka hasa maskini ni furaha, matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia.

Simameni kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo
Simameni kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha huu, Askofu Michael Msonganzila ameendeleza mafundisho tanzu ya Kanisa akisisitiza jamii kuona thamani ya uhai wa mwanadamu ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ameiasa jamii kukataa kutumika katika kukatisha maisha ya mwanadamu yeyote kwani hakuna mwenye dhamana juu ya uhai wa mtu mwingine. Wakumbuke kuwa kifo ni lazima kwa kila mtu ili kumfikia Mungu katika kusudi alilomuumbia mwanadamu, lakini Mungu mwenyewe aliyemuumba mwanadamu ndiye mwenye dhamana ya uhai na kifo cha mwanadamu. Fedha wanazopewa kwa ajili ya kuwaua binadamu wenzao kamwe haziwezi kumaliza umaskini walionao bali kuwasababishia mahangaiko ya dhamiri na umaskini wa hali huku wakiwa chukizo kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Hivyo waache tabia hiyo mara moja kwa kutubu na kumwongokea Mungu. Aidha ameiomba jamii kuhakikisha kwamba, inashikamana na inasimama imara katika kudumisha amani na hata wanaopona viashiria vya uvunjivu wa amani wakemee mara moja na kutoa taarifa katika mamlaka husika ili kuchukua tahadhari au kuzuia kabisa. Papa Paulo VI aliyechaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro Tarehe 21 Juni 1963 ndiye aliyeanzisha Siku ya Kuombea Amani Duniani ambapo, tarehe Mosi, Januari 1968 kwa mara ya kwanza akaadhimisha Siku ya Kuombea Amani Duniani. Tarehe 24 Desemba 1974 akafungua lango la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kama ishara ya kuzindua Mwaka wa Imani. Papa Paulo wa sita ni kiongozi wa Kanisa Katoliki aliyethubutu kufanya mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya nyaraka, hija za kichungaji ndani na nje ya Italia pamoja na fursa ya kukutana na viongozi mbalimbali wa kidini na kiserikali, kama kielelezo cha majadiliano ya kina kati ya Kanisa: Dini, Madhehebu, Serikali na Tamaduni. Papa Paulo wa sita katika Mafundisho yake ya Jumla kwa njia ya Nyaraka anakazia kwa namna ya pekee umuhimu wa Kanisa, kukuza na kudumisha majadiliano ndani ya Kanisa lenyewe; Kanisa na Ulimwengu.

Askofu Msonganzila asema, simameni kidete kulinda Injili ya Uhai
Askofu Msonganzila asema, simameni kidete kulinda Injili ya Uhai

Kutabarukiwa kwa Kanisa ni kielelezo kwamba, Kanisa hili sasa limewekwa wafu kwa ajili ya kumtolea Mungu: sifa, shukrani na sala, ili waamini waweze kutakatifuzwa. Kanisa hili kwa sasa ni nyumba ya Sala, Nyumba ya Mungu na Nyumba ya Ibada. Ni mahali ambapo waamini wanalishwa kwa Neno la Mungu na kushibishwa kwa Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu. Altare imetabarukiwa na hivyo kuwekwa wakfu, inapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa kwa sababu Altare ni kielelezo cha Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu anayejisadaka kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Ni mahali ambapo waamini wanatolea sala na sadaka zao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa. Kanisa pawe ni mahali pa: amani, usalama na utulivu wa ndani. Waamini wajifunze kutumia vyema nyumba ya Mungu na wala si mahali pa kwenda kupiga picha au kuperuzi kwenye mitandao wakiwa Kanisani. Kuta za Kanisa zimetabarukiwa kwa kupakwa Mafuta ya Krisma ya Wokovu yanayobarikiwa Siku ya Alhamisi Kuu. Haya ni mafuta matakatifu yanayotumika kwa ajili ya Ubatizo, Kipaimara na Daraja Takatifu. Mapadre wanapakwa Krisma ya wokovu viganjani mwao kama alama ya baraka na huduma kwa watu wa Mungu. Askofu anamiminiwa Krisma ya wokovu utosini kama kielelezo cha ukamilifu wa Daraja Takatifu na hivyo kufanywa kuwa ni mrithi na mwandamizi wa Mitume wa Kristo Yesu. Altare ni mahali patakatifu sana ndani ya Kanisa paheshimiwe na kuthaminiwa kwa ajili ya kuadhimisha Mambo Matakatifu, mahali pa kutolea sadaka ya haki na kulishwa kwa Neno la Mungu. Kumezikwa Masalia ya watakatifu ndani ya Kanisa kama kielelezo cha ushirika wa watakatifu unaosimikwa katika mema ndani ya Kanisa ambayo kimsingi ni amana na hazina ya pamoja.

Waamini wa Parokia ya Mt. Paulo VI, Bweri, Musoma
Waamini wa Parokia ya Mt. Paulo VI, Bweri, Musoma

Huu ni ushirika wa mambo matakatifu kwa ajili ya watakatifu. Kimsingi huu ni ushirika wa imani, Sakramenti za Kanisa, Karama na mapendo. Maadhimisho ya Mafumbo Matakatifu ndani ya Kanisa yananogeshwa na Neno la Mungu anayejifunua kwako, ili kuwatakatifuza na kuwatuma kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kama ilivyokuwa kwa Nabii Isaya, Mwenyezi Mungu anapenda kuonesha wema, huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka. Kristo Yesu Mfufuka bado anaendelea kukutana na wafuasi wake, kila mmoja katika Galilaya yake. Hapa ni mahali pa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo; Imani, Shukrani na Ibada katika kweli na roho. Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, amesisitiza amani katika jamii hasa ya Tanzania huku akiwapongeza waamini wa Parokia Teule ya Bweri, Nyabange kwa mshikamano wao tangu mwanzo wa ujenzi wa Kanisa hilo mpaka lilipokamilika na kutabarukiwa Mnamo Tarehe 29 Mei mwaka 2025. Hakika majitoleo yao Mungu ameyaona na kamwe hawatapungukiwa pale walipotoa.

Askofu Msonganzila

 

03 Juni 2025, 15:00