杏MAP导航

Tafuta

Tanzania inakabiliwa na ongezeko la matukio ya biashara haramu ya binadamu waathirika wakiwa wanawake na wasichana wadogo. Tanzania inakabiliwa na ongezeko la matukio ya biashara haramu ya binadamu waathirika wakiwa wanawake na wasichana wadogo.   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Watawa Katika Mapambano Dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu!

Lakini ukweli wa mambo, wanapofika huko wanakopelekwa, wanajikuta wakiwa wametumbukizwa kwenye biashara ya binadamu na viungo vyake sanjari na utumwa mamboleo kiasi kwamba, hawana tena uwezo wa kurejea nchini mwao. Ni watu wanaotoka katika maeneo ya vita, njaa na magonjwa; watu walioathirika kutokana na mipasuko ya: kiuchumi, kidini, kijamii, hali ngumu ya maisha. Lakini, sababu kubwa zaidi ni watu kufilisika kimaadili, kiutu na kijamii!

Sarah Pelaji, - Vatican.

Sababu nzito zinazopelekea watu kujikuta wanatumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na viungo vyake sanjari na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo ni umaskini wa hali na kipato, unaowawadanganya watu hawa kwamba, watapata fursa za ajira na hivyo kuondokana na hali yao duni. Lakini ukweli wa mambo, wanapofika huko wanakopelekwa, wanajikuta wakiwa wametumbukizwa kwenye biashara ya binadamu na viungo vyake sanjari na utumwa mamboleo kiasi kwamba, hawana tena uwezo wa kurejea nchini mwao. Ni watu wanaotoka katika maeneo ya vita, njaa na magonjwa; watu walioathirika kutokana na mipasuko ya: kiuchumi, kidini, kijamii, hali ngumu ya maisha pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Lakini, sababu kubwa zaidi ni watu kufilisika kimaadili na kiutu, kutokana na kuelemewa na uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka na madaraka! Mapambano haya yalipewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Biashara ya binadamu si wazo la kufikirika bali ni hali halisi inayogusa mamilioni ya watu duniani. Hawa ni wale watu wanaotumbukizwa kwenye biashara na utalii wa ngono; biashara ya viungo vya binadamu; ndoa shuruti na kazi za suluba kwa watoto wadogo, ambao wakati mwingine wanapelekwa mstari wa mbele kama chambo cha vita. Watoto hawa wakati mwingine wamekuwa ni kafara wa imani za kishirikina sehemu mbalimbali za dunia. Wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa mara nyingi wamejikuta hata wao pia wakitumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo.

Watawa katika mapambano dhidi ya utumwa mamboleo
Watawa katika mapambano dhidi ya utumwa mamboleo   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Ni katika muktadha huu, Tanzania inakabiliwa na ongezeko la matukio ya biashara haramu ya binadamu waathirika wakiwa wanawake na wasichana wadogo. Wanawake wengi husafirishwa kutoka vijijini kwenda mijini, kutoka Tanzania hadi nchi za nje kwa ajili ya biashara ya ukahaba, kufanya kazi za ndani na vijana wa kiume wanajihusisha na vikundi vya kigaidi. Serikali ya Tanzania inaendelea kupambana na usafirishaji huo haramu huku ikitoa mwaliko kwa mashirika ya kidini na ya kiraia kuimarisha juhudi za msingi kuzuia na kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu. Katika kukabiliana na hali hiyo, Umoja wa Watawa wa Kike Kikatoliki Tanzania “Tanzania Catholic Association of Sisters (TCAS) umechukua jukumu kubwa katika kupambana na janga hilo kupitia programu ya Talitha Kum. Juhudi za TCAS za kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu zimefanywa kupitia kampeni dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu tangu 2021 hadi 2025 katika kanda sita zikiwemo Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Magharibi, Kanda ya ziwa, Kanda ya Kusini Magharibi na Kanda ya Kusini mwa Tanzania. TCAS, kupitia Mpango wa Talitha Kum wamejikita katika kukuza uelewa na kujenga uwezo wa jamii ili kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu, ufikiaji wa jamii, mafunzo, juhudi za uokoaji, na kutibu wahanga hao kisaikolojia. Mratibu wa Programu hiyo ya Talitha Kum Tanzania SR. Eugenia Mshana alisema Dhamira ya mpango huo ni kuongeza uelewa na kuzuia biashara haramu ya binadamu kupitia elimu, utetezi na ushirikiano.

Hayati Papa Francisko alipambana na biashara ya utumwa mamboleo
Hayati Papa Francisko alipambana na biashara ya utumwa mamboleo   (Vatican Media)

Jukumu la   programu hiyo ni kutoa mafunzo katika Jamii kupitia parokia, Misikiti, shule na vyuo vikuu. Kutoa elimu juu ya usafirirshaji haramu katika mikoa ya mipakani ikiwemo mipaka Sirari na Namanga. Uhamasishaji wa Jamii katika Majimbo Katoliki ambayo yapo kwenye jamii hatarishi ya usafirishaji haramu wa binadamu yakiwemo majimbo ya Musoma, Iringa, Kahama, Dodoma, Mtwara, Dar es Salaam, Arusha, kigoma, Tabora, Singida, Tanga, Moshi na Same. Kuokoa wahanga kwa kuwatoa katika mazingira hatarishi na kuwapatia msaada wa kisaikolojia. Kuunda vilabu vya shule na vikundi vya ufuatiliaji wa jamii kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu na Ushirikiano na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania. Alielezea mafanikio kadhaa ya programu ambayo Watawa wa Kike nchini Tanzania chini ya TCAS wameyapata kupitia program hiyo akisema kuwa, wameweza kufikia jamii Zaidi ya watu 32,000 katika kanda sita zilizohamasishwa. Kujenga Uwezo Kupitia Semina kwa watawa, wanawake hususani wasichana, viongozi wa dini mbalimbali, viongozi wa jumuiya ndogondogo za Kikristo, Operesheni za Uokoaji, kutoa msaada wa kurejesha nyumbani na kuwaunganisha na familia wahanga makwao kutoka nchi za ughaibuni kama Malaysia na mataifa mengine ya Afrika. Wamekuwa watetezi wa Usafirishaji Haramu wa Binadamu hivyo kuzindua Siku ya Kitaifa dhidi ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu Julai 31, 2024 na mwaka huu Februari wakati wa Sikukuu ya Mtakatifu Bakhita. Wamefanikiwa kuboresha Ushirikiano wa Dini Mbalimbali kwa kuwa walikuwa na juhudi za Pamoja na viongozi wa Kikristo na Kiislamu wakati wa semina, utetezi na kampeni. Walikuwa na Ushirikiano wa Vyombo vya Habari ambao uliboresha usambazaji mpana wa ujumbe za kupinga usafirishaji haramu wa binadamu kufikia mamilioni ya watazamaji.

Watawa wakiandama kupinga biashara ya binadamu na utumwa mambo leo
Watawa wakiandama kupinga biashara ya binadamu na utumwa mambo leo   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

SR. Eugenia alisema programu hiyo inakabiliwa na Changamoto mbalimbali katika utekelezaji ikiwa ni pamoja na Muda Mdogo wa Kampeni. Kulingana na tathmini ya kampeni ya Talitha Kum hapakuwa na muda wa kutosha wa kuwafikia watu wengi na kufanya ufwatiliaji. Ukosefu wa Makazi kwa waathirika waliookolewa kwamba hakuna nyumba maalumu ya kuwahifadhi, ulinzi wa waathirika na matibabu yao. Miundombinu mibovu kwamba ilikuwa vigumu kufikia vijiji vya mbali vilivyo na barabara mbovu na kuwepo kwa makundi yenye silaha na Wanyama wakali. Hapakuwa na ufuatiliaji wa kina ili kuelewa namna program hiyo ilivyoleta mabadiliko katika jamii. Jumuiya zinaomba ufuatiliaji ufanyike, tathmini na mafunzo ya M&E. Ushirikishwaji wa Watu Wenye Ushawishi ambapo iligundulika kwamba wapo watu wenye majina mashuhuri wanaohusika na usafirishaji haramu wa binadamu uwepo wa makundi ya Kigaidi ambayo yanahusika katika kuwasafirisha vijana kwa mafunzo ya kijeshi. Hii ni changamoto kwa watawa hao na wote wanaoshiriki katika kampeni dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu. TCAS chini ya Mpango wa Talitha Kum ina mkakati wa Kuanzisha Nyumba Salama ili Kutoa makazi na usaidizi kamili kwa waathirika waliookolewa. Kudumisha Programu za Mafunzo kwa Kutoa elimu endelevu ya Ufuatiliaji, Tathmini, uhamasishaji na uwekezaji katika miundombinu ili kuboresha upatikanaji wa barabara na usalama katika maeneo ya mbali. Kuimarisha na kupanua ushirikiano na serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na mashirika wa kimataifa yanayopambana na usafirishaji haramu wa binadamu kwa ajili ya kufikia jumuiya pana na Kuimarisha Ushirikiano wa Vijana na Kuongeza vilabu vya shule na elimu.

TCAS inaendelea kujipambanua katika mapambano dhidi ya utumwa mamboleo
TCAS inaendelea kujipambanua katika mapambano dhidi ya utumwa mamboleo   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Juhudi za TCAS chini ya mpango wa Talitha Kum zimeleta mabadiliko ya maana katika vita dhidi ya ulanguzi wa binadamu. Kwa msaada unaoendelea, uratibu na ugawaji wa rasilimali, juhudi hizi zinaweza kupanuliwa na kudumishwa ili kuwalinda wanyonge na kurejesha utu kwa waathirika. Mkurugenzi wa Idara ya Kukuza Maendeleo Fungamani ya Mwanadamu ya Shrikisho la Mabaraza ya Maaskofu Ukanda wa Afrika Mashariki AMECEA Padri Paul Igweta wakati wa mahojiano maalum alieleza jinsi Kanisa Katoliki linavyojidhatiti na kutoa huduma ya kichungaji kwa wakimbizi na wahamiaji ambao wamesafirishwa katika njia zisizo salama. Alinukuu ujumbe wa Hayati Papa Francisko katika Siku ya Wakimbizi Duniani kwa Mwaka 2024, akisema kuwa suala la uhamiaji limekuwa suala muhimu kwake tangu siku za mwanzo za utume wake. Papa Francisko hakuona biashara haramu ya binadamu kama tatizo la kijamii bali kama dhambi kubwa inayoathiri mwili mzima wa Kristo. Aliuita "utumwa mamboleo" na mara kwa mara amelaani miundo ya kiuchumi na kijamii inayosababisha usafirishaji haramu wa binadamu. Aliitaja changamoto ya nchi za Afrika katika kupambana na biashara haramu ya binadamu kuwa ni Ukosefu wa Utashi, Sera na Kanuni dhaifu, Ukosefu wa Maarifa na Takwimu sahihi zinazochochea kuchukua hatumadhubuti, majibu yasiyoratibiwa wala kufanyiwa kazi, Kutozingatia Usafirishaji Haramu wa Binadamu kwenye Mikutano ya AMECEA. Pia alitaja sababu za biashara haramu ya binadamu akisema ni kuyumba kwa siasa katika nchi za Afrika, Umaskini, Ukosefu wa Ajira, Kutokuwa na elimu ya kutosha. Ushawishi wa mitandao ya kijamii, adhabu dhaifu kwa wahalifu, ufisadi (kwa mfano, katika uhamiaji, viwanja vya ndege na mipaka) na malezi duni katika ngazi ya familia.

Biashara Haramu ya Binadamu
23 Mei 2025, 13:44